Habari za Punde

Uislamu Haukatazi Waumini Wake Kujifunza Elimu ya Dunia.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa Tatu wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu Duniani akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Manidat Al – Bahr Mbweni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.
Na.Othman Khamis OMPR.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein amewataka Wahadhiri na Wataalamu wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu kuhakikisha kwamba Mitaala wanayoitumia katika kufundishia Taaluma ya Dini haitaleta athari kwa wanafunzi ndani ya mfumo wa  Mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia  yaliyopo hivi sasa Duniani.
Alisema Uislamu haukatazi Waumini wake kujifunza Elimu ya Dunia lakini kinachopaswa kuzingatiwa zaidi na Wahadhiri na Wataalamu hao ni kufuata Sheria na Miongozo ya Uislamu kwa vile Dini yenyewe tayari imeshakamilika katika nyanja zote kwa ajili ya kutekelezwa na Wanaadamu.
 Dr. Ali Mohamed Shein alisema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufungua Mkutano wa Tatu wa Siku mbili wa  Kimataifa wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu unaofanyika katika Hoteli ya Madinat  Al – Bahr  iliyopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema Mwanafunzi wa Chuo Kikuu anapaswa kujengewa mazingira  sahihi ya Mfumo wa Kisasa yatakayomuwezesha kushajiika na kujifunza masomo ya Sayansi, Ufundi na Ustawi wa Jamii ili atakapomaliza awe kiungo na maendeleo katka Umma unaomzunguuka.
Dr. Shein alisema Vyuo vya Kiislamu katika kipindi hichi cha utandawazi vina kazi kubwa kwa Wataalamu wake kufanya Utafiti wa kina katika masuala ya Ustawi na sayansi utakaowawezesha kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili Waumini wa Dini hiyo.
“ Vyuo Vikuu vya Kiislamu vichukuwe jukumu la kuieneza elimu  ya DSini ya Kiislamu sambamba na kujenga hoja za kujibu itikadi zisizo sahili zinazotolewa dhidi ya Dini hiyo”. Alisema Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alieleza kwamba ufundishaji wa sasa ni vyema ukazingatia matumizi ya Tekonojia ya Habari na Mawasiliano ambayo inamuharakisha Mwanafunzi kujifunza kwa haraka  Quran Tukufu na Mafundisho ya Kiongozi wa Dini hiyo Mtume Muhammad {SAW}.
Alisema Teknolojia hiyo ya kisasa ya Habari na Mawasiliano ni rahisi kwa vile Mwanafunzi anayeamua kutumia mfumo huo ana uwezo wa kutafuta kumbukumbu za Vitabu anavyovihitaji katika mafunzo yake  zikiwemo pia tafiti za Wahadhiri tofauti.
Dr. Ali Mohamed Shein ameupongeza Uongozi wa Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al – Sumait  chukwani kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu Duniani.
Aidha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  na aliushukuru pia Uongozi wa Taasisi ya Kimataifa ya Vyuo Vikuu vya Kiislamu {IIIT} kwa uamuzi wake wa Mkutano huo  wa Tatu kuufanyia  Visiwani Zanzibar.
Mapema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al – Simait Chukwani Profesa Amran Rasli alisema Zanzibar imepata Heshima kubwa kutokana na kufanyika kwa Mkutano huo wa Tatu wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu Duniani ikitanguliwa na ile iliyofanyika Morogoro na Uganda.
Profesa Amran alisema hii ni fursa ya pekee kwa Wahadhiri na Wataalamu wa Zanzibar  kuitumia nafasi ya uwepo wa Mkutano huo kuchota fikra kutokana na kuwasilishwa kwa Mada na Tfiti 50 kutoka kwa wenzao wa Mataifa shiriki katika Mkutano huo.
Naye  Mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya Mtandao waMawasiliano ya Kiislamu {IIIT} Profesa Omar Kasule alisema lengo la kuanzishwa kwa Taasisi yao ni kujikita zaidi katika kutoa Elimu sahihi katika Umma wa Kiislamu.
Profesa Omar alisema Wataalamu wanaelewa na kufahamu fika kwamba Elimu ndio inayosogeza maendeleo mahali popote pale Duniani iwe kwa Taifa na hata Jamii za kawaida.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika hafla hiyo ya Ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu Duniani Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amnali Zanzibar Mh. Simai Mohammed Said alisema hadhara hiyo itasaidia kuleta mashirikiano baina ya Wahadhiri na Wasomi mbali mbali.
Mh. Simai alisema ushirikiano huo wa Kitaaluma katika masuala zaidi ya Dini ya Kiislamu utaongeza upeo wa uelewano katika kuendeleza mbele Dini ya Kiislam katika maeneo  tofauti Duniani.
Mkutano huo wa Tatu wa wa Siku Mbili wa Kimataifa wa Vyuo Vikuu vya Kiislamu Duniani umeshirikisha Wahadhiri, Wataalamu na Wasomi wa Vyuo Vikuu kutoka Mataifa ya Afrika Mashariki, Afrika Magharibi pamoja na Mashariki mwa Bara la Asia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.