Habari za Punde

MBINU ZA MATUMIZI YA ZANA BORA KUINUA SEKTA YA KILIMO

Na Ismail Ngayonga. Maelezo Jijini Dar es Salaam.                                                          KILIMO ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, hii ni kutokana na ukweli kuwa sekta hii huzalisha nusu ya uchumi wa nchi, robo tatu ya mazao yote yanayouzwa nje ya nchi na ni tegemezi la chakula na kutoa ajira ya karibu asilimia 80 ya Watanzania.                          
Hata hivyo kwa kipindi cha miongo miwili iliyopita, jumla ya uzalishaji wa bidhaa na huduma kitaifa kwa sekta ya kilimo ya kilimo imekuwa ikiongeza kwa wastani wa asilimia 3.5 tu kwa mwaka.
Inaelezwa kuwa ukuaji huu umekuwa ukiathiriwa zaidi na teknolojia duni ya kilimo, hali ya hewa isiyotarabiriwa na kushuka kwa kiwango uzalishaji upande wa ardhi, kutokana na asilimia 70 ya maeneo ya kilimo nchini kutegemea kilimo cha jembe la mkono.
Kuna baadhi ya vikwazo vinavyozuia kuenea kwa kwa matumizi ya teknolojia ya kisasa za kilimo na hivyo kukwamisha uwezo uliopo wa kuongeza uzalishaji katika kilimo, ikiwemo gharama kubwa za kupata huduma za zana za kisasa za kilimo kwa kukodi na ukosefu wa utaalamu na huduma za kufanyia matengenezo zana husika.
Aidha wakulima wadogo wadogo kwa ujumla hawana uelewa, umoja na ari ya kujipanga ili kushughulikia mahitaji yao na changamoto mbalimbali ili waongeze uzalishaji katika Kilimo.
Katika jitihada zake za kukuza matumizi ya zana bora za Kilimo, Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wakulima katika kubuni mbinu mpya za matumizi ya utafiti, elimu na teknolojia mpya ili kuwa na shughuli za biashara zinazohusiana na kilimo zenye faida ya kuridhisha.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa kilimo, Japhet Hasunga anasema  takwimu zinaonesha kwamba matumizi ya zana bora za kilimo yanaongezeka miongoni mwa wakulima nchini ambapo kwa mwaka 2018 wastani wa kitaifa umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa wanyama kazi.
Naongeza kuwa kutokana na ongezeko hilo, matumizi ya jembe la mkono yamepungua na kufikia asilimia 53 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 62 kwa mwaka 2013, juhudi zilizotokana na Serikali kuhamasisha sekta binafsi kuingiza matrekta na zana zake nchini.
“Kati ya mwaka 2016/2017 na 2017/2018, jumla ya matrekta makubwa 2,476 na matrekta madogo 586 yaliingizwa nchini, na Wizara kwa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), TIB Corporate Bank na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa mafunzo kwa waendesha mitambo 76 kuhusu uendeshaji na matengenezo ya matrekta aina ya URSUS” anasema Waziri Hasunga.
Waziri Hasunga anasema viongozi 108 wa Vyama vya Msingi na 53 wa Vyama vya Mazao (AMCOS) wamepatiwa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji wa matrekta na kati ya AMCOS hizo, 50 ni za Mkoa wa Mwanza na 3 za Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara.
Anaongeza kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) imetoa mafunzo ya uendeshaji wa mitambo ya kuvunia na mashine za kukoboa mpunga kwa maopareta 28 na mafunzo ya usimamizi na uendeshaji mradi wa zana kwa wakulima viongozi katika skimu 14 za umwagiliaji.
Anazitaja Skimu hizo kuwa ni pamoja na Skimu za Mbuyuni, Uturo, na Ipatagwa (Mbarali), Nakahuga (Songea), Magozi (Iringa), Mkindo (Mvomero), Kilangali (Kilosa), Bagamoyo BIDP (Bagamoyo), Mombo (Korogwe), Kivulini (Mwanga), Musa Mwinjanga (Hai), Lekitatu (Arumeru), na Muungano (Babati).
Aidha Waziri Hasunga anasema Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) Wizara yake inaendelea kutoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo ambapo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994 jumla ya mikopo yenye thamani ya Tsh Bilioni 82 imetolewa.
Akifafanua zaidi Waziri Hasunga anasema katika kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019, mikopo 33 yenye thamani ya Shilingi 1,495,362,060 ikiwemo 22 ya mitambo ya mashambani, sita (6) ya pembejeo za kilimo na mitano (5) ya umwagiliaji imetolewa na vilevile Serikali imeendelea na ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo ya nyuma ambapo katika mwaka 2018/19 jumla ya Tsh Bilioni 1.8 zimerejeshwa.
Matumizi ya zana bora za kilimo unasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi na faida pamoja na kupunguza gharama za muda na rasilimali fedha ambazo kwa kiasi kikubwa zimewasaidia wakulima wengi kuongeza ukubwa wa mashamba yao angalau kwa robo hekta hadi kufikia hekta 1 hadi 4.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.