Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Aifariji Famiulia ya Mzee Borafia Kwa Kuunguliwa Nyumba Yao na Moto Juzi.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia baadhi ya sehemu ya Nyumba ya Familia ya Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa Mjini Mzee Borafia Silima Juma iliyoungua na kuteketeza vitu vyote vilivyomo ndani hapo Mtaa wa Muembe Rikunda Michenzani.
Mwanafamilia ya Mzee Borafia Nd. Salum Borafia Kushoto akimueleza Balozi Seif  moto ulivyoteketeza kila kitundani ya Nyumba yao majira ya saa 1.00 Usiku Jumapili iliyopita.Kati kati yao ni Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Mjini Mzee Borafia Silima Juma.
Mzee Borafia Silima Juma wa Kulia akielezea faraja yake kufuatia ujio wa Viongozi, Wanchama wa Chama cha Mapinduzi na Wananchi wanaofika nyumbani kwao kuifariji Familia yake kutokana na janga iliyopata la kuungua kwa Nyumba yao.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema vyombo vya Dola kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo wakati wote hubeba dhima ya kufanya uchunguzi dhidi ya hujuma zinazoibuka na hatimae kuleta hatari ya uvunjifu wa Amani ndani ya Jamii.
Alisema uchunguzi wa hujuma zozote zile pale unapokamilika na kupatikana ushahidi kamili vyombo hivyo havitasita  kuchukuwa hatua za kisheria katika kutoa haki kwa muhusika.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara fupi ya kuipa pole Familia ya Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Mzee Borafia Silima Juma kufuatia Nyumba yake kuwaka moto na kuteketeza vitu vyote vilivyomo ndani hapo Mtaa wa Muembe Rikunda nyuma ya Jumba Nambari Mbili Michenzani.
Balozi Seif alisema Wananchi wanapaswa kuendelea kufuata Sheria na taratibu zilizopo Nchini kwa kuviamini vyombo vya Dola  vilivyopewa jukumu kubwa na Serikali la kulinda Mali na Maisha yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliitaka Familia ya Mzee Borafya kuwa na subra katika kipindi hichi cha mpito kufuatia mtihani uliowapata na kuithibitishia kwamba Serikali itaangalia utaratibu wa kuihami Familia hiyo kutokana na mazingira halisi ya Nyumba hiyo ilivyo hivi sasa.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed alisema utafiti wa awali uliofanywa na Wataalamu wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Zanzibar muda mfupi baada ya tukio hilo umebaini kwamba huo ulikuwa ni moto wa kutiwa kwa makusudi.
Waziri Aboud alisema Wataalamu hao hivi sasa wanaendelea na uchambuzi wa kina wa utafiti wa tukio hilo na baadae kuona jinsi gani Kamisheni hiyo inaweza kuisaidia Familia hiyo kwa njia za Kitaalamu.
Mapema Mmoja wa Wanafamilia wa Nyumba hiyo Bwana Salum Borafia Silima alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wanafamilia hao wanaamini kwamba tukio hilo ni hujuma ya makusudi kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha saa Ishirini na Nne.
Bwana Salum alisema hujuma ya kwanza ilitokea Jumamosi majira ya saa moja ya Usiku  pale Mmoja miongoni mwa Wanafamilia hao ambae ni mgonjwa alipobaini harufu ya moshi dirishani na kupiga kelele zilizosaidia kubaini moto huo ambao uliunguza waya na pazia la Dirisha hilo.
Alisema tukio hilo likatokea tena Siku ya Pili ya Jumapili muda unaolingana ambalo ni kubwa zaidi lililopelekea moto mkubwa kuripuka na kusababisha kuunguza kila kilichomo ndani ya Nyumba hiyo ambapo baadae akalazimika kutoa Ripoti kituo cha Polisi kwa hatua zinazofaa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.