Habari za Punde

TASAF Yatowa Elimu kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya BLW Zanzibar Kusimamia Viongozi Wakuu wa Serikali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Viongozi wa TASAF na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili Vuga Jijini Zanzibar.


Na.Othman Khamis.OMPR.
Wakati Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} ukijikita kuingia katika Awamu ya Tatu sehemu ya Pili katika Mfumo  wa Kisasa wa Mawasiliano ya Habari juhudi zimechukuliwa kuwafunda zaidi Wataalamu wake  ili wawajibike vyema kwenye mabadiliko hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Tasaf  Nd. Ladislaus Mwamanga alitoa kauli hiyo wakati wa kuwapatia ufahamu zaidi Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar.
Nd. Ladislaus Mwamanga alisema upo ujanja  unaofanywa na baadhi ya wahalifu kwenye Mitandao ya Teknolojia ya Mawasiliano ambayo Wataalamu wa Tasaf wameshajipanga vyema ili kuhakikisha hakutakuwa na changamoto itayojitokeza wakati wa utekelezaji wa Tasaf Awamu ya Tatu Sehemu ya Pili.
Alisema Utekelezaji wa shughuli za Tasaf  tokea ilipoanzishwa Awamu ya kwanza umezingatia matumizi ya Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano {TEHAMA} inayoboreshwa ili kuweza kupokea na kutoa Taarifa zinazosaidia katika utekelezaji wa awamu mbali mbali za Tasaf.
Mkurugenzi Mwamanga alifafanua kwamba Tasaf ilianza kufanya majaribio ya malipo kwa njia ta Kielektroniki katika Mamlaka za Maeneo ya Utekelezaji 16 kuanzia Mwaka 2017 sawa na asilimia 10% ya Walengwa wa Mpango wa Kaya Maskini Nchini Tanzania.
Alisema malipo kwa njia ya Kielektroniki yanasaidia kutatua changamoto  za malipo kwa njia ya fedha taslim pamoja na kuunganisha Kaya na huduma za Kifedha ili kuleta maendeleo ya haraka kwenye kaya husika.
Nd. Mwamanga alieleza kwamba majaribio hayo yalianza kwa kufanya tafiti mbali mbali na kutembelea Nchi za Kenya na India ili kujifunza njia bora za malipo kwa njia ya Kielektroniki.
“ Malipo ya Kaya maskini yanatumwa moja kwa moja kwenye akaunti ya simu ya mkononi au Benki kwa Mwakilishi wa Kaya”. Alisisitiza Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Mfuko wa Tasaf.
Nd. Mwamanga alifahamisha kwamba jumla ya Kaya 55,350 kati ya Kaya 102,229 sawa na asilimia 54% kwenye majaribio zilikuwa zimelipwa kwa njia mpya ya Mtandao wa Teknolojia ya Mawasiliano hadi malipo ya Januari/Febuari 2019.
Alisema Kati ya Kaya zilizolipwa kwa njia ya kielektroniki, asilimia 95% wanalipwa kupitia mitandao ya simu na asilimia 5% hulipwa kwenye akaunti ya benki huku Tasaf ikibeba gharama za kuhawilisha na kutoa fedha ili kuihakikisha mlengwa anapata fedha iliyokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} aliwapongeza Viongozi wa ngazi mbali za Serikali na Wananchi wa Visiwaa vya Unguja na Pemba kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa Watendaji wa Mfuko huo na kupelekea Tasaf Awamu na Kwanza na Pili kufanikiwa vyema.
Naye  Meneja Uhawilishaji Fedha wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Nd. Selemani Masala aliwaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba  Wananchi wanapaswa kuhamasishwa katika kutoa malalamiko yao.
Nd. Selemani alisema mfumo huo wa kutoa malalamiko pale zinapotokea changamoto katika maeneo yao inakuwa rahisi kuchukuliwa hatua za haraka zitakazochangia kufanikiwa kwa amza ya kubuniwa mpango huo.
Wakitoa mawazo na michango yao  Wajumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  walisema Mfuko wa Tasaf  umefanya  kazi kubwa iliyotoa afueni kwa ustawi wa Wananchi waliowengi wenye kuishi katika Kaya Maskini.
Waheshimiwa Wajumbe hao wausisitiza Uongozi wa Tasaf  kufuatilia changamoto za Walengwa wa Mfuko wale wanaopambana na tatizo la upoteaji wa Simu zao za mkononi ambazo tayari zimeshasajiliwa katika mfumo huo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} kwa kuanzisha Mfumo wa Kielektroniki katika utekelezaji wa Tasaf Awamu ya Tatu sehemu ya Pili unaostahiki kuitwa  E –Tasaf.
Balozi Seif  aliwaeleza Wajumbe wa Mafunzo hayo kwamba mfumo huo unaorahisisha huduma kwenda kwa haraka na kwa wakati utaonyesha uwazi wa kuendesha mambo ya Mfuko huo kwa kujiamini zaidi.
Aliutaka Uongozi wa Mfuko huo usichoke kuendelea kutoa taaluma zaidi kwa walengwa ili kuona malengo ya Awamu ya Tati sehemu ya Pili unafanikiwa kwa asilimia kubwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akionyesha furaha yake kutokana na maendeleo makubwa ya Tafa Nchini Tanzania alisema Ulimwengu wa sasa uko kiganjani kutokana na Binaadamu kuendesha harakatiu zake za Kimaisha  kwa kutumia simu yake ya Mkononi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.