Habari za Punde

TASAF Yatowa Elimu Kwa Wataalam Wanaowasimamia Wananchi Wanaonufaika na Mpango wa Kaya Masikini

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Mihayo Juma N’hunga akisisitiza jambo kwa wawezeshaji hao katika ukumbi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania TASAF hapo Mazizini Kando kidogo  ya Mji wa Zanzibar.
Na.Kassim Salum Abdi
Wawezeshaji na wataalamu wanaowasimamia Wananchi wanaonufaika na mapango wa kupunguza kaya Maskini Nchini wametakiwa kuwashauri vyema Walengwa wao kwa kubuni miradi imara inayoweza kutekelezeka kwa urahisi na wakati wote.
Kufanya hivyo kutawasaidia walengwa hao kuendeleza miradi hiyo sambamba na kuwaingizia kipato ili kulifikia lengo la serikali kuu la kuwapunguzia wananchi wake tatizo la ukali wa maisha pamoja na kuondosha umaskini Nchini.
Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga alieleza hayo wakati akifungua mafunzo rejea ya stadi za maisha  kwa wawezeshaji wa kuwasaidia walengwa wa kaya maskini Unguja katika ukumbi wa TASAF Mazizini Kando kidogo  ya Mji wa Zanzibar.
Mhe. Mihayo aliwataka wawezeshaji hao kutumia mbinu na maarifa yao walionayo katika kuhakikisha lengo la serikali la kuondosha kabisa umaskini kwa wananchi wake linafikiwa kwa kushauriana nao walenga juu ya miradi mizuri itakayowavusha kutoka hatua moja kwenda hatua nyengine ya mafanikio.
“Niwaombe tu Ndugu wawezeshaji baada ya mafunzo haya basi tukajitahidi  kutumia hekima na busara zetu pamoja na matumizi mazuri ya lugha katika   kuwashauri walengwa” Mhe. Mihayo alieleza.
Alisema itakua jambo la busara kwa kuwashauri walengwa kubuni miradi isiyofanana ili iwe rahisi kwao kuitekeleza kwa kipindi cha muda mfupi pamoja na kuhakikisha wanafanya ukaguzi kwa kuyapitia maeneo ambayo yamebuniwa kwa lengo la kujiridhisha na taarifa za mlengwa zilizo sahihi.
 Aidha, Naibu Waziri huyo alifafanua kwamba serikali kuwateuwa wao kuwemo katika mchakato huo imeonesha jinsi gani inavyowaamini hivyo hakuna budi kwao kufanyakazi kwa jitihada zote ili kuilinda heshima ya serikali kwa kujisusha kwa wananchi.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mafunzo hayo Mkurugenzi uratibu wa shughuli za serikali SMT na SMZ  Khalid Bakar Hamrani alisema wawezeshaji hao watakwenda katika shehia 126 kuwapatia mafunzo walengwa yanayohusiana na mambo ya Kibishara ili iwe rahisi na mahususi kwao kupunguza kasi ya umasikini
Mkurugenzi Khalid alieleza kwamba Zanzibar imepata heshima kubwa duniani kutokana na mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango  wa TASAF na zipo baadhi ya nchi zimekuwa zikifika Zanzibar kujifunza kwa vitendo.
Kwa upande wake mratibu wa TASAF Unguja Ndugu Makame Ali Haji  alisema utaratibu wa kuwapatia mafunzo wawezeshaji hao una lenga kuwajengea uwezo katika kuhakikisha lengo la serikali linafikiwa kwa kuwasaidia walengwa.
Alisema kuna umuhimu kwa wawezeshaji hao kujishusha zaidi kwa wananchi muda utakapofika kwea kukusanya mawazo ya miradi na pale inapobidi kuwashauri kitaalamu juu ya miradi yao na kuepuka kuwalazimisha kufanya miradi wanayoifikiria wao.
Wakiwasilisha mada wakufunzi  katika mafunzo hayo wamesema mpango wa Kunufaisha kaya maskini umekuwa ukiwashirikisha viongozi wa serikali katika kuhakikisha mchakato wa kuwafikia wananchi wake unafanikiwa.
Katika Mafunzo hayo ya siku tano jumla ya mada nane zinatarajiwa kuwasilishwa ikiwemo Boresha maisha yako, Nataka kuwa mjasiriamali, Buni wazo la biashara na mada nyenginezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.