Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (kulia) akimkaribisha Kamishna Rose Macharia kutoka Kenya alipofanya ziara katika ofisi za tume jijini Dodoma
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akiongea na wageni wake kutoka Kenya waliotembelea ofisi za tume kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya utawala bora na maadili ya viongozi.
Kamishna wa tume, Dkt. Fatma Halfan akisisitiza jambo katika kikao kifupi kilichaofanyika Dodoma baina ya tume na ujumbe kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na rushwa nchini Kenya Novemba 22,2019. Kushoto ni Mwenyekiti wa tume, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu.
Na Mbaraka Kambona
Kamishna wa Tume ya Maadili
na Kupambana na Rushwa nchini Kenya, Rose
Macharia ameikaribisha Tume ya Haki za
Binadamu na utawala bora (THBUB) kushirikiana nao kufundisha elimu ya maadili ya viongozi
katika chuo chao cha taifa cha maadili ili kukuza na kuimarisha utawala bora
katika nchi hizo.
Macharia alitoa kauli
hiyo katika ziara fupi aliyoifanya katika ofizi za Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora zilizopo Dodoma Novemba 22, 2019.
Akiongea katika kikao
baina yake na Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, Macharia alisema
kuwa wametembelea tume kwa sababu wanatambua kuwa hiyo ni taasisi kongwe katika masuala ya usuluhishi
na usimamizi wa utawala bora na ndio
taasisi ya kwanza barani Afrika iliyoanzishwa na Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kazi hiyo.
Macharia alieleza kuwa
kwa kutambua uimara na ukongwe wa tume katika masuala ya utawala bora ndio
maana wameona ni vyema kuja kujifunza na
kutafuta namna nzuri ya kushirikiana katika kujenga maadili ya viongozi na utawala
unaofaa kwenye jamii zao.
“masuala ya maadili ya
uongozi kwetu yalianzishwa mwaka 2011 kwa sheria ya maadili na mapambano dhidi
ya rushwa, hivyo taasisi yetu bado ni changa, tumekuja kujifunza kutoka kwenu ili tuweze
kushirikiana kwa njia tofauti kuhakikisha nchi zetu zinakuwa na utawala
unaofaa”,alisema Macharia
Macharia aliendelea
kusema kuwa katika chuo chao wanafundisha masuala ya maadili ya uongozi, hivyo
anawakaribisha tume kwenda kushirikiana nao katika chuo hicho kufundisha kwani
lengo la chuo hicho ni kukuza maadili ya viongozi.
“Lengo la chuo chetu ni
kukuza maadili ya viongozi ili kuwa na utawala unaofaa, siku zote tunasema ni
vyema kuzuia kuliko kusubiri jambo liharibike ndio muanze kulirekebisha”, alisisitiza
Macharia
Naye, Jaji Mwaimu
akiongea katika kikao hicho kifupi alisema kuwa ni kweli tume ni taasisi kongwe
sana katika masuala ya utawala bora ambayo ilianzishwa mwaka 1965 na Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati huo ikiitwa tume ya kudumu ya uchunguzi
kwa lengo maalumu la kusimamia maadili ya viongozi mpaka ilipobadilishwa
kikatiba mwaka 2001 kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
“Jambo hilo
mlilolifanya la kuwa na chuo cha maadili ni maamuzi mazuri, na hivyo sisi sote
kwa pamoja tuna mahala pa kujifunza pia kutoka kwenu”, alisema Mwaimu
“Japo sisi tume
hatufanyii kazi moja kwa moja masuala ya maadili ya viongozi lakini tumekuwa na
ushirikiano mzuri sana na Sekretarieti ya maadili ya viongozi na taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na rushwa (PCCB), na mara zote wananchi wanapoleta
malalamiko yanayohusu maadili ya viongozi au masuala yanayohusiana na rushwa
tumekuwa tukiyaelekeza huko kwani wao ndio taasisi zilizoundwa kusimamia
masuala hayo” Jaji Mwaimu alimueleza Kamishna Macharia
Akiongea awali, Jaji
Mwaimu alimueleza Kamishna huyo kuwa tume ni Idara huru ya serikali
iliyoanzishwa kikatiba na kupewa jukumu la kulinda, kuhifadhi na kutetea haki
za binadamu na kusimamia misingi ya utawala bora.
“Mimi na wenzangu tuliopewa
dhamana ya kuongoza taasisi hii tutajitahidi kuhakikisha tunafanya kazi zetu
kwa weledi mkubwa tukizingatia sheria na taratibu zilizowekwa na nchi”,alieleza
Jaji Mwaimu
Naye, Kamishna wa Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dkt. Fatma Halfan alisema katika kikao
hicho kuwa suala la ushirikiano ni jambo muhimu, hivyo waendelee kushirikiana, na
kuhusu suala la kwenda kufundisha katika chuo hicho cha maadili nchini Kenya ni
jambo linalowezekana na wako tayari kushirikiana nao katika kufanikisha hilo.
Aidha, Dkt. Fatma alimueleza
Kamishna Macharia kuwa tume ni taasisi ya muungano hivyo wakipata nafasi
wasisite kwenda Zanzibar pia ili kujifunza zaidi.
Katika ziara yake hiyo,
Kamishna Macharia aliambatana na maafisa kutoka tume hiyo ya Kenya ambao ni Kairishi
Marimba, Patrick Owinu na Stella Mbele.
Wengine ni Viongozi
waandamizi kutoka Sekretarieti ya Maadili nchini ambao ni Waziri Kipacha na
Jasmin Bakari.
No comments:
Post a Comment