Na Mwashungi Tahir - Maelezo.
Makamo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi UVCCM Taifa Bi.Tabia Mwita amewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kukilinda Chama cha Mapinduzi na kuhakikisha kinapata ushindi wa kishindo ifikapo 2020.
Hayo ameyasema huko Tawi la CCM Kombeni Wadi ya Maungani wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya darasa la itikadi na kuwakabidhi vijana kadi za Chama cha Mapinduzi pamoja na vyeti baada ya kumaliza mafunzo hayo.
Alisema kwamba sasa tunakaribia kuingia kwenye uchaguzi mkuu na tunatarajiya kupata ushindi hivyo ni lazima vijana kwa kila alofikia umri wa miaka 18 kuhamasishana kujiandikisha katika daftari la kudumu.
Pia amesema lengo la kuanzishwa madarasa ya itikadi kwa vijana ni kujua historia ya nchi yao na kujua wapi ilipotoka na inapoelekea kwani nchi hii wazee waliipata kwa taabu hadi kufika kufanyika Mapinduzi na kuwataka vijana hao wasidanganywe.
Aidha amesema kutokana na umuhimu wa vijana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein tunampongeza kwa kutoa fursa mbali mbali za vijana Serikalini ikiwemo kuunda baraza la vijana Taifa.
Nae msoma risala Haitham Ahmad Said amesema darasa la itikadi limeanzishwa likiwa na jumla ya wanachama 200 wanawake 115 wanaume 85 ndani ya darasa hilo limezaa vikundi 7 ikiwemo upambaji, uvuvi,ukulima, kutengeneza sabuni , vipochi kushona nguo na ufumaji.
Pia amesema mafanikio yalopatikana katika darasa la itikadi ni pamoja na kuunganisha vijana na kuwa karibu na Chama cha Mapinduzi , kujua historia ya ya nchi pamoja na CCM, kujifunza ujasiriamali, kujuana na kupendana .
Vile vile akielezea kwa upande wa changamoto ni pamoja na uhaba wa vitendea kazi kama vile charahani , vitambaa , nyuzi , vifaa vya kutengenezea vipochi na malighafi ya kutengenezea sabuni ya maji, ukosefu wa vifaa vya uvuvi na ukulima jambo ambalo linawakatisha vijana tamaa.
Miongoni mwa vijana aliyepata fursa hiyo ya kusoma darasa hilo Sabra Mohamed Shiru amesema amefaidika kupata mafunzo hayo ikiwemo darasa la ujasiriamali kwani ameweza kujua mambo mengi na anatarajia kujiendeleza kwa kujiingiia kipato .
Pia amesema ameweza kupata ujasiri wa kufanya mambo mengi ikiwemo kuweza kuzungumza mbele ya jamii katika kukiimarisha na kukitetea Chama cha Mapinduzi na ametoa wito kwa vijana wenziwe kujitokeza kwenye darasa hilo ili waweze kuhamasika kwenye Chama.
No comments:
Post a Comment