Habari za Punde

Dini Iendelee Kuota Ndani ya Vifuu na Muoyo ya Waumini Ili Kuwa Kinga Kuepuka Matamanio.

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akiyafungua mashindano ya kuhifadhi Quran kwa akina Mama wa Mkoa Kaskazini Unguja na kuungwa mkono na Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake wa Kiislamu Pemba yaliyofanyika Fiysabilillah Tablih Markaz Kaskazini Unguja.
 Amir wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Mkoa wa Kaskazini Unguja Sheikh Said Nyange akitoa nenola makaribisho kwenye hafla ya ufunguzi wa Mashindano ya Kuhifadhisha Quran.
Mwana Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Mkoa wa Kaskazini Unguja  Ukti Fatma akisoma Risala mbele ya mgeni Rasmi Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman hayupo pichani.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema licha ya kutanuka zaidi kwa Elimu ya Dini Nchini lakini bado wimbi la maovu linaendelea kushamiri miongoni mwa Waumini na hata Jamii.
Alisema ni vyema Dini iendelee kuota ndani ya vifua na mioyo ya Waumini ili iwe kinga madhubuti ya kuyaepuka matamanio ya nafsi yanayoleta balaa na fadhaa wakati mwengine.
Mama Asha Suleiman Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiyafungua mashindano ya kuhifadhi Quran kwa akina Mama wa Mkoa Kaskazini Unguja walioungwa mkono na Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake wa Kiislamu Pemba yaliyofanyika Fiysabilillah Tablih Markaz Kaskazini Unguja.
Alisema ipo mifano hai inayoonyesha Waumini hasa Walezi kukimbia jukumu lao la ulezi akitolea mfano udhibiti wa Watoto Yatima katika Familia baada ya kufariki Mmoja miongoni mwao na badala yake Watoto hao huishia kulelewa na Taasisi za Kuhudumia Mayatima.
Mama Asha aliwakumbusha Wazazi hasa akina Mama kutenga muda wa Malezi ya Watoto wao licha ya Mabadiliko ya harakati za kimaisha zinazotoa mwanya kwa wakorofi wachache wenye tabia chafu ya kuwafanyia vitendo viovu Watoto wao.
Alisema wimbi la udhalilishaji wa Watoto wadogo Mitaani hivi sasa limepamba moto na matokeo yake mimba zisizotarajiwa zinashuhudiwa na kuleta sura mbaya machoni mwa Waumini na Jamii nzima kwa ujumla.
Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaahidi akinamama hao wa Jumuiya ya kuhifadhisha Quran Mkoa Kaskazini Unguja  kuwapatia msaada wa Kompyuta ili kuwa na uhakika wa kuhifadhi kumbukumu zao za kila siku.
Akisoma Risala Mmoja wa Wanajumiya hao Ukti Fatma alisema yapo maendeleo makubwa yaliyopatikana tokea kuasisiwa kwa Jumuiya yao Mnamo Mwaka  2008 na kupata usajili rasmi Mwaka 2019.
Ukti Fatma alisema mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la Madrasa Mia Moja zinazochipua Wanachama wanaoongezeka kiwango cha ufahamu kutoka Juzuu Nne kwenda juzuu 19 ambapo miongoni mwao hivi sasa wameshafikia Juzuu zote 30.
Alisema Jumuiya imefikia hatua ya kujitegemea kwa Majaji wake ambapo tayari hivi sasa imeshaanzisha mfumo wa ziara za kuzikagua Madrasa zilizo wanachama wa Jumuiya hiyo ili kuangalia maendeleo yake.
Ukti Fatma alisema zoezi kama hilo litapangwa pia kwa kuzitembelea madrasa zilizo katika Mikoa mengine katika azma ya kuona Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Muungu { Quran }kinaendelea kubakia ndani ya vifua vya Waumini.
Mapema wakitoa salamu Mlezi wa Jumuiya ya Kuhifadhi Quran Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Vuai Mwinyi na Mlezi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiislamu Wilaya ya Mkoani Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri walisema ziara za Mashindano  ya kuhifadhi Quran  kati ya Kaskazini Unguja na Kusini Pemba zinaleta faraja katika uhifadhi wa Kitabu Kitukufu cha Quran.
Mh. Vuai ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja  na Mh. Mjengo Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi walisema Viongozi wataendelea kubeba dhima ya kusaidia nguvu ili kuziona Jumuiya hizo zinafikia malengo yake.
Walimuomba Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuendelea kuwaunga mkono akinamama hao katika matayarisho ya Ijitihai inayotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Mwezi wa Machi Mwaka 2020.
Alisema hatua hiyo ya kuungwa mkono itaendelea kuwapa moyo akinamama hao kwa vile asilimia 80% ya Waumini wanaoshiriki matayarisho na kuhudhuria katika Ijitihai zote ni Wanawake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.