Habari za Punde

WAZIRI UMMY ATAKA WATAALAM WA MAENDELEO YA JAMII WALETEA MABADILIKO

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwahutubia wahitimu wa Astashahada, Stashahada na Shahada katika Mahafali ya Tisa ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru yaliyofanyika leo mkoani Arusha.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akifungua Kusanyiko la Mahafali ya Tisa ya Taasisi ya Maendeleo ya jamii Tengeru yaliyofanyika leo mkoani Arusha.
Baadhi ya Wahitimu kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru wakisiliza hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) wakati wa Mahafali ya Tisa ya Taasisi ya hiyo yaliyofanyika leo mkoani Arusha.


Na Mwandishi Wetu Arusha
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amewataka wahitimu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kuleta mabadiliko katika jamii zinazowazunguka kwa kuzihamasisha kutafuta fursa za maendeleo.

Ameyasema hayo leo mkoani Arusha wakati akiwatunuku wahitimu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada katika mahafali ya tisa ya Taasisi hiyo.

Amewaambia wahitimu hao kuwa wataalam wa Maendeleo ya Jamii ni watalaam muhimu sana katika kuhamasisha jamii katika kujiletea maendeleo yao hivyo wakatumike katika jamii zao kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na taifa.

"Mkatumike katika jamii zenu mkalete mabadiliko lazima muoneshe kama mnaweza msibaki mnalalamika fanya jambo linaloonekana fursa zitakuja" alisema Mhe. Ummy

Waziri Ummy amewaasa wahitimu hao kuanza kwa kujitolea katika kazi na kuzingatia maadili katika maeneo watakayokuwa wanafanya kazi au kuisaidia jamii kwani hakuna njia ya moja kwa moja ya uhakika wa kupata ajira kama hawatojitolea.


Pia Waziri Ummy amewataka Wahitimu hao kuonesha utaalam wao katika maisha yao na maisha ya jamii inayowazunguka katika kutatua changamoto zao na za jamii zao kwa kuleta mawazo chanja kwa wananjamii ikiwa na jinsi ya kufanya changamoto kuwa fursa za kimaendeleo.

Aidha Waziri Ummy ameitaka Taasisi ya Maendeleo ya Jamii kuongeza nguvu katika kuhakikisha wanashirikiana na jamii inayowazunguka katika kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili na kuazisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Tuoneshe namna gani wataalam wa maendeleo ya jamii tunaweza kusaidia jamii katika kufikia kipato cha kati na kuwa na Tanzania ya uchumi wa viwanda” amesema Mhe. Ummy.

Pia Waziri Ummy aliwataka wahitimu hao waliopata mikopo ya Serikali kuhakikisha wanarudisha mikopo ili kuwezesha watanzania wengine wanaohitaji elimu kupata mikopo kama Serikali ilivyowapatia wao mikopo iliyowasaidia kufikia kuhitimu.

Naye Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewataka wahitimu hao kuitumia elimu walioipata kuwa nyenzo, zana na funguo ya fursa mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za kimaisha ili kutumia utaalamu wao kupata majawabu ya changamoto na suluhisho la matatizo mbalimbali kwa maendeleo yao na jamii zao.

Ameongeza kuwa Kada ya Maendeleo ya Jamii ni nyenzo muhimu sana katika maendeleo ya nchi yoyote na Serikali inathamini sana Taaluma ya Maendeleo ya Jamii kwani imekuwa msaada mkubwa katika kutekeleza miradi mbalimbali hapa nchini.

"Msiwe na hofu wahitimu kwani nyinyi ni watu muhimu katika jamii yetu na elimu mliyoipata ikawe nyenzo, funguo na fursa ya maendeleo katika nchi yetu" alisema Dkt. Jingu

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Dkt. Bakari George amewasa wahitimu hao kwenda kuleta mabadiliko katika jamii na kuhakikisha wanakuwa chachu ya mabadiliko na kutengeneza fursa za ajira kwa wengine.

"Vyeti mtakavyopata sio njia au mlango wa ajira nikielelezo cha kusoma sasa mkaitumie kuhamasisha jamii katika kukabiliana na changamoto za maisha" alisema Dkt. Bakari

Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru katika mahafali ya tisa kwa mwakawa masomo 2018/2019 imewatunuku jumla ya wahitimu 918 wa Astashahada, Stashahada na Shahada mbalimbali ikiwemo za Maendeleo ya Jamii, jinsia na upangaji wa miradi. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.