Habari za Punde

Jeshi la Polisi laagizwa kuwadhibiti madereva wasiofuata sheria za barabara

Na Ali Issa na Wahida Juma Maelezo Zanzibar   

Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Khamis Juma Mwalimu ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kuwadhibiti madereva wanaoendesha vyombo vya moto kwa mwendo wa kasi ili kuepuka ajali barabarani.

Kauli hiyo ameitoa huko Muwanda Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja katika hafla ya uzinduzi wa Barabara ya Donge-Muwanda ikiwa ni shamra shamra za miaka 56 ya mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema kuna baadhi ya madereva wasiokuwa waangalifu hupuuza sheria za barabarani husababisha ajali na kupoteza maisha ya watu ni vyema kuchukuliwa hatua  za kisheria ili kujikinga na ajali hizo.

 "Madereva kama hawa wazembe wasiofuata sheria za barabarani wanaokwenda mbio ovyo bila ya kuzingatia sheria watiwe hatiani, wachukuliwe hatua za kisheria”, alieleza Waziri Khamis

Ameitaka mamlaka inayoshughulikia na ujenzi wa barabara kuweka alama elekezi zitakazo waongoza madereva ikiwa ni hatua ya kukinga ajali za barabarani kwa abiria na waendao kwa miguu.

aidha Waziri huyo amesema Serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Rais Dkt Ali Mohammed Shein imedhamiria kuwafikishia huduma za kijamii wananchi wake walioko mijini na vijijini ili kupata faida za matunda ya Mapinduzi pamoja na Utelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020. 

Waziri huyo alisema ufunguzi wa barabara hiyo ni faraja kubwa kwa wananchi wa Donge Muwanda na wageni kupata urahisi wa kusafirishia mazao yao ya biashara ukizingatia wananchi wa kijiji hicho wengi wao wanajishughulisha na shughuli za ukulima, uvuvi na ufugaji.

Akitoa taarifa ya kitaalam Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliani na Usafirishaji Mustafa Abudu Jumbe amesema barabara hiyo yenye ufefu wa kilomita (3.8) imejengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Mapinduzi Zanzibar chini ya kampuni ya kizalendo ya Salim Engineering Service ambayo imegharimu zaidi ya Bilioni 1 kukamilika kwake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.