Habari za Punde

Mahakama Kamilisheni Ujenzi wa Miundombinu -Mhe. Majaliwa.

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Wilaya ya ruangwa, baada ya kuzindua Jengo la Mahakama ya Wilaya Ruangwa, mkoani Lindi, Januari 13, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa uongozi wa Mahakama nchini uhakikishe unakamilisha ujenzi wa miundombinu ya Mahakama ili kuwapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa katika kutafuta haki zao.

Amesema kuna wilaya 139 Tanzania Bara, kati ya wilaya hizo wilaya 111 zilizo na huduma ya Mahakama za Wilaya na wilaya nyingine 28 bado zinahudumiwa na Mahakama za Wilaya za jirani ambazo zimepewa mamlaka ya kisheria kuhudumia Mahakama zisizo na majengo ya Wilaya.

Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Januari 13, 2020) wakati akizindua jengo la Mahakama ya wilaya ya Ruangwa. Amesema ni vema uongozi wa Mahakama uhakikishe kuwa yale yote waliyojipangia kwenye mpango wao wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama 2016/17 – 2020/21 unatekelezwa kwa wakati.

Waziri Mkuu amesema kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Wilaya Ruangwa mwaka 2009, wananchi wa wilaya hiyo walilazimika kusafiri umbali wa kilomita 180 kufuata huduma za mahakama wilayani Lindi. Mahakama hiyo itarahisisha upatikanaji wa haki wilayani Ruangwa.

“Umbali huo mrefu ulisababisha wananchi wengi kupoteza muda mwingi ambao wangeutumia kwa shughuli za uzalishaji mali.  Wakati mwingine wananchi hao walikosa haki zao kwa kushindwa kumudu gharama za usafiri kuhudhuria mashauri yao wilayani Lindi.”

Waziri Mkuu amesema Mahakama ni muhimu katika kudumisha amani na kuleta maelewano ndani ya nchi au jamii ambayo huwa ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi, hivyo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuamua kujenga Mahakama hiyo Wilayani Ruangwa pamoja na sehemu nyingine nchini.

Amesema kupitia Mahakama, migogoro mingi hupata usuluhishi na hivyo kuimarisha hali ya amani na utulivu.  “Kwa lugha nyingine,Mahakama inapokuwa imara Taifa letu huvutia uwekezaji kwa kuwa wawekezaji wanakuwa na uhakika na usalama wao pamoja na mali zao. 

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na Mahakama kuhakikisha kuwa mipango yake iliyojiwekea inatekelezwa kama ilivyokusudiwa, kwani bado kuna kazi kubwa mbele yao.

Wakati hu huo, Waziri Mkuu ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kukusanya mapato kupitia mfumo wa Kielekitroniki wa Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali (Government electronic Payment Gateway, GePG) kwani Serikali ilielekeza kila taasisi itumie mfumo huo ili kupunguza mianya ya rushwa na upotevu wa fedha.

Amesema amefurahi kusikia kuwa kwa kutumia mfumo wa GePG, Mahakama iliweza kuongeza kiwango cha makusanyo kutoka sh. bilioni 1.6 mwaka 2017 hadi sh. bilioni 2.5 mwezi Desemba 2019 baada ya kuanza kutumia GePG. “Fedha hizi zitatumika kuchangia ujenzi wa mahakama na miundombinu mingine ya kiuchumi unaoendelea katika kila kona nchini.”

“Ni ukweli usiofichika kwamba hata wananchi nao wanafarijika kuona kuwa kile mnachowatoza kinaenda moja kwa moja kwenye mfuko mkuu wa Serikali, na baadaye kiasi fulani kinarudi kwenu kujenga miundombinu ya kisasa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.”

Waziri Mkuu amesema kuwa hayo ndiyo malengo na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli. “Aidha, kwa kufanya hivyo, mnachangia utekelezaji wa malengo yaliyoainishwa vema kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.”

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma amesema kwa muda mrefu, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba, na uchakavu wa majengo katika ngazi zote za Mahakama, yaani Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi (Mahakamaza Mikoa), Mahakama Kuu na hata Mahakama ya Rufani.
Amesema ili kukabiliana na ukubwa wa changamoto ya upungufu na uchakavu wa majengo yake, Mahakama ya Tanzania ilitayarisha Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu (2016-2021). “Mpango huu umetathmini hali ya majengo ya Mahakama katika Mikoa na Wilaya zote za Tanzania Bara.”
Jaji Mku amesema mpango huo umelenga kupunguza au kuondoa kabisa uhaba na uchakavu. Jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa ni kielelezo cha utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama ya Tanzania. 
Pia, Jaji Mkuu ametumia ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa watumishi wa Mahakama, majengo kwamba hayo ya kisasa na miundombinu bora, iambatane na upatikanaji wa huduma bora kwa mwananchi. 
“Kila mtumishi wa Mahakama (kama walivyo watumishi wote wa umma) anao Mkataba na watumiaji wa huduma za Mahakama. Kipimo chetu cha kutimiza masharti ya Mkataba huu, ni nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama ambayo ni ‘Upatikanaji na Utoaji wa Haki kwa Wakati’, hivyo siku zote watumishi wa Mahakama tukumbuke kuwa Mahakama hii ni mali ya wananchi na wananchi wana haki ya msingi ya kupata huduma iliyo bora kwa wakati.” 
Amewasihi watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ruangwa na Mahakama nyingine hapa nchini kuacha kabisa mienendo na tabia ambazo zinakiuka miiko na maadili ya kazi kwa watumishi wa umma. “Jengo hili lisiwe na mianya au viashiria vya ukosefu wa maadili.”

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATATU, JANUARI 13, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.