Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akimsalimia Msanii Mkongwe wa Taarab Zanzibar.Bi. Mwanajuma Ali Hassan, aliyeimba wimbo wa "Mpunga Kinuni" wakati wa hafla ya Taarab ya Kikundi cha Taifa Zanzibar Kuadhimisha Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar iliofanyika katika ukumbi wa Sheikh. Idrisa Abdulwakili Kikwajuni Zanzibar jana 12-1-2020 usiku.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein jana usiku alijumuika na wananchi mbali mbali kwenye taarabu
rasmi ya maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hafla hiyo iliyofanyika Ukumbi
wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni, magwiji wa sanaa ya taarab kutoka
Kikundi cha Taifa hapa nchini, walimudu vyema kukonga nyoyo za wananchi
waliohudhuria kutokana na umahiri wao wa kucharaza ala pamoja kughani nyimbo mbali
mbali, ikiwemo zenye kuleta hamasa ya Mapinduzi.
Wasanii nguli, akiwemo Profesa Mohamed
Elias, Profesa Gogo, Al-anisa Sada Mohamed, Ustadh Idd Sued, Ustadh Makame Faki
(sauti ya zege), Al-anisa Sharia Issa na wengineo, walitawala vyema jukwaa
kiasi cha kuwafanya wasikilizaji kushindwa kujizuia na kuibua vifijo na
nderemo.
Miongoni mwa nyimbo zilizovuta hisia
na kushangiliwa muda wote ni ile ya ‘Tumbili hafugiki’ aliyoimba msanii mahiri
Profesa Gogo ambapo kiitikio chake kilisikika, ’hafugiki Tumbili mnyama mkorofi,
umpe kile na hiki bado yeye hatosheki, kazoweya Tumbili kuchapiachapia miti’.
Nae, Al-anisa Fatuma Issa, (mwimbaji
mualikwa) akadhihirisha thamani ya sauti yake, pale alipoimba wimbo maarufu wa
‘haya maumbile yangu’, wimbo aliouimba miaka kadhaa iliyopita na kumpatia sifa
kubwa.
Kwa ujumla, usiku wa Januari 12,
ulikuwa ni usiku maalum kwa wapenzi wa sanaa ya taarabu waliohudhuria, nyimbo
mbali mbali zilizoghaniwa zilitosha kuwaburudisha na kukonga nyoyo zao.
Nyimbo nyengine zilizoimbwa usiku huo
zilikuwa ni pamoja na ‘Mpewa hapokonyeki’ iliyoyoghaniwa na Al-anisa Mariam
Juma, Wakwezi na wakulima (Ustadh Makame Faki), Dunia ina fisadi (Al-anisa Sharia
Issa), Tarehe 11 (Ust. Iddi Sued), Nnavyokupenda (al-anisa Hilda Mohamed),
Anaetowa ni mola (Al-anisa Sada Mohamed) na Waliosema hatuwezi iliyoimbwa na Ustadh
Hafidh Abdusalami.
Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Vijana,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Omar Hassan ‘King’ alisema Wizara imetekeleza agizo
la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dk. Ali Mohamed
Shein la kikundi hicho kupatiwa vifaa
ili kufanikisha vyema shughuli zake, na kubainisha kuwa baadhi ya
vifaa hivyo vimeanza kutumika.
Aidha, alisema utekelezaji wa agizo la
kuwakumbuka na kuwaalika wasanii wa zamani katika hafla kama hizo
limetekelezwa, na kuainisha kuwa baadhi ya wasanii walioalikwa, kuwa ni pamoja na Mwajuma Ali
Hassan ambae alitajika kutokana na
nyimbo ya ‘mpunga na kiwanja’.
Wengine ni mtunzi/muimbaji Mariam Hamdani, Salum Kassim aliesifika kwa
nyimbo ya ‘macho yake’, Ali Masoud Suleiman anaekumbukwa kwa wimbo wa’kinu’,
Fatma Issa alietamba na wimbo wa ‘umewashuka’ pamoja msanii na muigizaji
Borafia Silima Juma.
Taarab hiyo ilihudhuriwa na viongozi
mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluhu Hassan, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Idd pamoja na viongozi mbali mbali.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment