Muwakilishi wa rais wa
TLS, Mary Munissi (kushoto) akimkabidhi baadhi ya Machapisho ya TLS Mwenyekiti
wa Tume, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu.
Muwakilishi wa rais wa
TLS, Mary Munissi akiongea katika kikao hicho kifupi mara baada ya kumkaribisha
Mwenyekiti wa THBUB.
Na
Mbaraka Kambona,
Mwenyekiti wa Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu
ametembelea Chama cha Wanasheria (TLS) jijini Dodoma na kuhimiza ushirikiano baina
ya taasisi hizo.
Jaji Mwaimu alitoa
kauli hiyo Januari 23, 2020 alipofanya ziara katika ofisi za chama hicho kwa
lengo la kufahamiana na kujenga mazingira mazuri ya ushirikiano.
Akiongea katika kikao
hicho kifupi, Jaji Mwaimu alimueleza Muwakilishi wa Rais wa TLS jijini Dodoma,
Mary Munissi kuwa tume inafahamu kuwa TLS imekuwa msaada mkubwa kwa jamii
katika utoaji wa msaada wa kisheria na
kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao.
“Majukumu yetu kwa
kiasi kikubwa yanafanana, hivyo itakuwa vizuri tukishirikiana katika kuwasaidia
wananchi kupata na kufurahia haki zao”, Jaji Mwaimu alieleza
“Ni jukumu letu sisi
sote kuwahudumia na kulinda haki zao wananchi,
na kuhakikisha kuwa wakati wote wanaweza kupata haki zao na kufikia kwa urahisi
vyombo vinavyohusika na utoaji haki nchini”, aliongeza
“Tumekuja hapa leo
kuonesha nia yetu ya kutaka ushirikiano, kushirikiana na wadau kwetu sisi ni
moja ya kipaumbele chetu, hivyo niwaeleze kuwa tupo pamoja, tuunganishe nguvu
zetu na tufanye kazi kwa dhumuni la kuwahudumia wananchi ”, alisisitiza
Akiongezea aliyoyasema
Jaji Mwaimu, Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Mohamed Hamad alisema kuwa tume wakati wote imekuwa na ushirikiano mzuri
na Asasi za Kiraia nchini na mpaka sasa wameshaingia mkataba wa ushirikiano na
Asasi ishirini na moja (21).
“Sisi tume tunaamini
haki za binadamu ni suala mtambuka ambalo linahitaji jitihada za pamoja
kutekeleza, tume peke yake haiwezi, jambo muhimu ni kuunganisha nguvu zetu ili
kutekeleza na kusimamia haki za binadamu nchini” aliongeza Mhe. Hamad
Kwa upande mwingine, Muwakilishi
wa rais wa TLS, Mary Munissi alisema kuwa amefurahishwa na ziara hiyo ya
viongozi wa juu wa tume kutembelea ofisi hizo na kuahidi kuwa salamu hizo
atazifikisha kwa rais, na kuahidi kuwa watatumia vyema ushirikiano huo ambao
utasaidia kurahisisha utendaji wa kazi.
Kwa kuongezea, Wakili
Isaac Mwaipopo wa TLS alisema kuwa chama hicho kwa wakati wote kimekuwa
kikijitahidi kutoa msaada wa sheria kwa wananchi, na pale wanapopata malalamiko
ambayo yanakuwa nje ya uwezo wao wanayawasilisha katika mamlaka husika.
Katika hatua nyingine,
TLS imeiomba tume kuwapa ushirikiano wa karibu hususan katika eneo la haki za
binadamu, na kuangalia uwezekano wa kuwasaidia kuwakwamulia vikwazo
wanavyokutana navyo wakati wa utekelezaji wa mradi wao wa upatikanaji wa haki.
Aidha, Wakili Mwaipopo aliishauri
Tume kutumia tafiti zao walizofanya katika masuala ya haki za binadamu kwani
kwa muda mrefu wamefanya utafiti katika eneo hilo na wana taarifa ambazo
zinaweza kuisaidia tume kujua ukubwa wa tatizo na kuweka mikakati ya kupata
ufumbuzi.
Mbali na kutekeleza
mradi wa upatikanaji wa haki, TLS inaendelea kusaidia kujenga mahusiano baina
ya wasaidizi wa sheria na serikali, na mpaka sasa wanafanya kazi kwa karibu na
Jeshi la Magereza, Polisi na Wizara ya Katiba na Sheria. Pia, TLS wamekiri kuwa
serikali imekuwa ikiwashirikisha katika michakato mbalimbali ya kuandaa miswada
ya kisheria na utungwaji wa sheria mpya.
Mwenyekiti wa Tume,
Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (katikati-mwenye koti la kijivu) akiwa katika picha
ya pamoja na viongozi wa tume na wa TLS. Kushoto kwake ni Muwakilishi wa rais
wa TLS, Mary Munissi
No comments:
Post a Comment