Habari za Punde

IMF KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUIMARISHA SERA ZA KIUCHUMI

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tatu kushoto) akieleza kuhusu agenda ya Serikali ya kujenga uchumi Jumuishi, wakati wa Mkutano kati yake na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke (wa tatu kulia), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.

Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali ya Tanzania inatarijia kukutana na Timu ya wataalamu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya kujadili Programu mpya ya Ushauri wa Kisera (PSI) yenye dhima ya kusimamia sera za kiuchumi kwa lengo la kutatua changamoto zitakazoonekana pamoja na namna ya kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini.
Haya yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi mpya wa IMF nchini, Bw. Jens Renke, aliyekuja kujitambulisha rasmi kwa Waziri huyo jijini Dodoma baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hapa nchini.
Dkt. Mpango alisema kuwa pamoja na kufanya majadiliano na wataalamu hao, Serikali inatarajia kuwa wataafikiana nao ili kuanzisha programu hiyo ya Serikali ambayo Shirika hilo limekuwa likishauri.
“Tumekuwa tukishirikiana na IMF kwa muda mrefu na imekuwa ikitushauri mambo mbalimbali ya kusimamia Sera za Kiuchumi katika kuondoa changamato ya umasikini na kuwa na maendeleo endelevu kwa usimamizi wa Sera za Uchumi “, alieleza Dkt. Mpango.
Aidha Dkt. Mpango alimueleza Mwakilishi huyo kuwa vipaumbele vya Serikali na juhudi mbali mbali zilizofanyika katika kukabiliana na tatizo la umaskini ni pamoja na kujenga uchumi jumuishi, kusimamia fedha za umma vizuri, kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwekeza katika kilimo pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kisasa.
Waziri Mpango alibainisha kuwa vipaumbele vingine ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa na kukusanya mapato ya ndani ipasavyo ili kuweza kutumia rasilimali zote za nchi vizuri na kuboresha huduma muhimu za wananchi kama elimu na afya.
Aidha, alimueleza mgeni huyo kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana nae katika kuleta maendeleo nchini.
Naye Mwakilishi Mkazi mpya wa IMF nchini, Bw. Jens Renke, aliahidi kuwa balozi mzuri wa Tanzania katika Shirika hilo na kuiomba Serikali ushirikiano katika kazi zake.
Aliiomba Serikali imtumie katika kutatua matatizo mbalimbali na yuko tayari kutoa ushauri wa kisera na kichumi, na kubainisha kuwa atafanya kazi kama sehemu ya Serikali katika kutatua matatizo na kuleta maendeleo nchini.
Bw. Renke alisema anapenda kujifunza mengi nchini na atatembelea katika mikoa, Serikali za Mitaa pamoja na vyuo mbalimbali ili kuona mambo ambayo Serikali imeyafanya katika kujikwamua kiuchumi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akipeana mkono na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke, aliefika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma kujitambulisha.
Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke, akieleza nia yake ya kushirikiana kwa dhati na Tanzania kwa kuisemea Serikali katika Shirika lake kuhusu vipaumbele vya Taifa, wakati alipofika katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma kujitambulisha.
Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBC), Dkt. Albina Chuwa (kulia) akieleza jambo wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke, jijini Dodoma.
Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBC), Dkt. Albina Chuwa (kushoto) akiwa na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke, baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya Mwakilishi huyo wa IMF na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani).
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tano kulia)  na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke (wa tano kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe waliohudhulia Mkutano kati ya Dkt. Mpango na mwakilishi huyo wa IMF nchini, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
 (Picha na Peter Haule, WFM, Dodoma)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.