Habari za Punde

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza jinsi alivyopokea kwa furaha taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kuendelea kukua kwa uchumi wa Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga ambapo katika mazungumzo hayo Cavana huyo alimueleza Dk. Shein jinsi uchumi wa Zanzibar unavyoendelea kuimarika.

Katika maelezo hayo Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa hiyo ni habari njema ambayo inatoa mwanga wa maendeleo ya uchumi hapa Zanzibar kwani juhudi za makusudi bado zinaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha uchumi unaimarika.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na uwepo wa uongozi bora sambamba na mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Serikali, wananchi pamoja na  na Benki kuu ya Tanzania (BoT).

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika suala zima la mfumko wa bei pia, amepokea kwa furaha  maelezo ya kuwa mfumko wa bei uko vizuri hapa nchini hali ambayo inaleta faraja kwa wananchi.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza neema ya chakula iliyopo Zanzibar na kusisitiza kuwa Zanzibar hakuna shida ya chakula na wananchi wamekuwa wakila chakula wanachokitaka.

Hivyo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hasa ikizingatiwa kwamba hiyo ni Benki ya wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na hayo, Profesa Luoga alitumia fursa hiyo kumueleza Dk. Shein mashirikiano mazuri yaliopo kati ya uongozi wa Wizara ya Fedha Zanzibar na Benki hiyo hatua ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa.

Rais Dk. Shein alimpongeza Gavana huyo kwa juhudi anazozichukua katika kuhakikisha Benki hiyo inaimarika na inaendelea kuwa tegemeo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akieleza matumaini yake kwa uongozi mpya wa Profesa Florens Luoga.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa (BoT), ni Benki ya Muungano ambayo imekuwa ikifanya vyema shughuli zake kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuendelea kuiunga mkono yeye na Serikali anayoiongoza.

Nae Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Florens Luoga alimthibitishia Rais Dk. Shein kuwa uchumi wa Zanzibar unaendelea kuimarika kila uchao na kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuisimamia hali hiyo.

Gavana huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unazidi kuimarika kutoka wastani wa asilimia saba hivi sasa.

Gavana wa benki kuu ya Tanzania Florens Luoga amesema kuwa bado benki kuu haijachapisha wala kuingiza pesa mpya kwenye mzunguko tangu mwaka 2009 na kwamba pesa iliyopo kwenye mzunguko inatosha kabisa kwa mahitaji ya soko.

Aidha, Gavana huyo alieleza kuwa Benki kuu ya Tanzania (BoT) inaendelea na mapambano kwa watengenezaji, wasaambazaji na watumiaji wa Noti bandia na kueleza hatua inazozichukua katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya kufanya utambuzi wa Noti bandia ili kuepuka utapeli.

Aliongeza kuwa mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika kupambana na hali hiyo ambayo katika kipindi hichi imeweza kujitokeza na (BoT) kuahidi kuendelea kudhibiti hali hiyo kwa kupambana na wahalifu wote

Pia, kiongozi huyo alieleza  benki kuu itaendelea kutekeleza Sera yake ya Sarafu Safi huku akiziomba benki zote kuhakikisha zinatoa huduma rafiki kwa wananchi ili waweze kutumia vyema huduma hizo.

Alieleza haja kwa Benki kufungua Matawi yake nje ya mji hapa Zanzibar ili wananchi waweze kupata huduma hizo kwa urahisi mkubwa na kusisitiza kuwa azma ya (BoT) ni kuhakikisha huduma hiyo inapatikana si zaidi ya kilomita tano ya makaazi ya wananchi.

Profesa Luoga alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ina fedha za kutosha katika kuendeleza shughuli zake za kibenki hapa nchini huku akieleza azma yake ya kuliimarisha Tawi lake la Benki la hapa Zanzibar.

Alimthibitishia Rais Dk. Shein kwamba mfumko wa bei hapa nchini uko vizuri na (BoT) inaendelea kuuthibiti ikiwa ni pamoja na kudhibiti kupanda kwa bei ya mazao ya chakula hiyo ni kutokana na mazao mengi hupatikana kwa miongo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.