Habari za Punde

Wananchi Wananufaika na Mpango wa Kaya Masini Nchini TASAF

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Panya Ali Abullah akizungumza na Wananchi wa Kaya Maskini Mkoa wa Kusini Unguja wakati Kamati yake ilipofanya nziara ya Kukagua Miradi yao.

Wananchi wanaonufaika na mpango wa kaya Maskani nchini  (TASAF) wametakiwa kuziunga mkono  serikali zote mbili kutokana na mchango mkubwa  zinazotoa kwa wananchi wake ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza umaskini nchini.
Kufanya hivyo kutapelekea serikali hizo kuongeza jitihada zaidi  katika suala zima la kuwawezesha wananchi  katika kuwaunganisha pamoja ili kushirikiana katika kuibua miradi mbali mbali itakayowasaidia kujiongezea kipato na kuimarisha maisha yao.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya baraza la wawakili inayoshugulikia Ofisi za viongozi wakuu Mhe. Panya Ali Abdalla alieleza hayo katika ziara maalum iliofanywa na kamati hiyo katika kuangalia na kukagua miradi iliobuniwa na walengwa wanaonufaika na mpango wa kaya maskini kwa upande wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya kudumu alisema kuwa mpango wa kunusuru kaya maskini umesaidia kwa kiasi kikubwa kuuleta umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wengi Tanzania hali inayopelekea urahisi wa utekelezaji wa mipango ya serikali.
Mhe. panya aliwataka viongozi wanaosimamia Mfuko wa TASAF Zanzibar kuongeza umakini katika kuhakikisha fedha zinazotolewa zinawafikia walengwa waliokusudiwa sambamba na kusimamia matumizi ya fedha hizo ili lile lengo la serikali la kuondosha changamoto zinazowakabili wananchi wake liweze kufikiwa.
Alifafanua kuwa mpango wa kunusuru kaya maskini umekuja kuleta ukombozi kwa wananchi wa Tanzania kwani kuna mafanikio makubwa yaliopatikana kwa walengwa hususani akina mama baadhi yao wamefikia hatua ya kujenga nyumba pamoja na kusomesha watoto kwa kukidhi mahitaji yao madogo madogo.
Nae mjumbe wa kamati hiyo ambae pia ni Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Mihayo Juma N’hunga  aliwashauri walengwa wanaonufaika na mpango huo pamoja na miradi walioianzisha ikiwemo mradi wa upandaji wa miti kuna haja sasa ya kuangalia uwezekano wa kuanzisha miradi ya mazao ya matunda.
Mhe. Mihayo alieleza endapo walenga watajikita katika uzalishaji wa mazao ya matunda wataweza kupata mavuno na mafaniko makubwa ndani ya kipindi cha muda mfupi kutokana na uzalishaji wa mazao hayo kuchukua kipindi kifupi katika utayarishaji hadi kufikia kipindi cha mavuno.
Aliwahakikishia viongozi wa shehia kwamba kupitia utekelezaji wa Mradi wa TASAF Awamu ya tatu Kipindi cha Pili  serikali itaangalia uwezekano wa kuwaorodhesha wananchi wengine ili nao waweze kunufaika na mpango huo kama waliovyonufaika wananchi wengine.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Unguja ndugu Makame Ali Haji alisema kufuatia ziara hiyo ya viongozi wa kamati ya kudumu ya baraza la wawakilishi yapo mapendekezo ya kufanywa kwa Tathimini ya utekelezaji wa mpango huo.
Mratibu Makame alisema Uongozi  unaosimamia Mfuko wa TASAF utayazingatia mapendekezo hayo yaliyotolewa na wajumbe wa kamati ya kudumu ili kufanikisha lengo la serikali hasa katika kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum hasa walemavu.
Akitoa shukrani kwa niaba ya walengwa wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini Sheha wa shehia ya Kikungwi Mohamed Haji Ushauri alisema mpango huo umewasaidia wananchi kuimarisha maisha yao kwa kushiriki katika kazi mbali mbali za ujasiriamali ambazo zimewasaidia kujiingizia kipato.
Ziara hiyo ya viongozi wa Kamati ya kudumu baraza la wawakilishi inayosimamia ofisi za viongozi wakuu imewatembelea walengwa katika shehia ya Kikungwi pamoja shehia ya kizimkazi Dimbani na kujionea shughuli mbali mbali zilizofanywa na wananchi.
Baadhi ya Wananchi wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini wa Mkoa wa Kusini Unguja waliotembelewa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi ya Viongozi wa Kitaifa.
Mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Mheshimiwa Mtumwa Suleiman akishawishika kushiriki kati za Ususi wa Mikoba na Ukili wakati Kamti yake walipotembelea Miradi ya Wananchi wa Kaya Maskini Mkoa wa Kusini Unaguja.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga akiwatsisitiza Wananchi wa Kaya Maskini kuzingatia umuhimu wa kuanzisha pia Kilimo cha Matunda.

Muonekano mzuri wa Shamba darasa la Wana Ushirikiwa wa Kikundi cha Mpango Tasaf kupitia  Kaya Maskini cha Kijiji cha Kizimkazi Dimbani.
Moja kati ya Nyumba ya Mwananchi aliyenufaikia na mpango wa Tafasi kupitia Kaya Maskini bibi Uchungu Mwinyi Ali wa Kijiji cha Kikungwi Mkoa wa Kusini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.