Habari za Punde

WAZIRI KAIRUKI: MFUKO WA KUKOPESHA WAWEKEZAJI KUKOMBOA WENGI

 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiteta jambo na Balozi wa Tanznaia nchini Sweden Mhe. Dkt. Wilibrod Slaa wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Machi, 2020
Rais wa TCCIA Bw. Paul Koyi akihutubia wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na Wanachama wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Uswidi na Afrika Mashariki kaika Ukumbi wa Mikutano Serena Hotel Jijini Dar es Salaam.

NA. MWANDISHI WETU
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imewezesha kuanzisha mfuko maalum wa kukopesha watu wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kati na vikubwa lengo likiwa ni kuwanufaisha Watanzania waliokosa mitaji na wenye nia ya kuwekeza nchini.
Mfuko huo ulioanzishwa Februari 22 mwaka huu utakuwa ukikopesha Watanzania kuanzia kiwango cha shilingi  milioni 8 hadi 50 kwa wenye nia ya kuwekeza viwanda vya kati na shilingi milioni 50 hadi 300 kwa wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vikubwa.
Aidha, ofisi hiyo inashirikiana na taasisi nyingine kuendesha mfuko huo ikiwepo Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Shirika la Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Hayo yamebainishwa hii leo (Machi 12, 2020) Jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki wakati akizungumza na Waandishi wa Habari  mara baada ya kufungua Kongamano la pili la Biashara na Uwekezaji la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Sweden linaloendelea kwa siku mbili Jijini humo.
Kairuki amesema Tanzania hivi sasa imeimarisha Mazingira ya Uwekezaji ambapo tangu kuingia kwa Rais Magufuli Madarakani hakuna kodi yoyote iliyoongezwa kwenye biashara na uwekezaji huku kodi zaidi ya 168 zikifutwa katika kipindi cha miaka miwili zikiwepo kodi 105 za kilimo.
Wakati akifungua Kongamano hilo Waziri Kairuki aliwataka Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza nchini Tanzania kwa kueleza kuwa Sera, Sheria na miundombinu yake imeboreshwa kwa kiwango kikubwa.
"Tunazo fursa nyingi za uwekezaji hapa Tanzania, tuna fursa kwenye Kilimo cha mazao ya chakula na biashara pamoja na mnyororo wake wa thamani kwenye sekta hiyo, tunahitaji uwekezaji wa viwanda mbalimbali vikiwepo vya Dawa na  vifaa tiba, mafuta ya kula na vinginevyo vingi" alisema Waziri Kairuki.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dkt Wilbrod Slaa amesema Wafanyabiashara wa NORDIC wameisifu Serikali ya Tanzania  kwa kuondoa rushwa na kuimarisha utendaji wa wazi Serikalini suala ambalo awali lilikuwa likuwapa changamoto kubwa.
"Nimekuwa nakutana na wafanyabiashara na wawekezaji wengi wa Sweden jambo kubwa nililolipata kutoka kwao ni kwamba wanashukuru tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani mambo ya chini ya meza hayapo tena, angalau sasa wanafanya biashara juu ya meza wengine walifikia hatua ya kufunga biashara zao, lakini pia naomba nishauri tu vibali vya wawekezaji viharakishwe ili kwenda na wakati", alisema Dkt. Slaa.
Kongamano hilo ambalo kwa mara ya kwanza lilifanyika Stockhom Sweden mwaka 2012 lilikuja ma naadhimio kadhaa ya kushirikiana katika kuimarisha uchumi wa nchi hizo kibiashara na uwekezaji lilileta matokeo chanya kufuatia kuwepo kwa wawekezaji wengi wa Sweden kuwekeza kwenye nchi za Afrika Mashariki.
Mkutano huo umehudhuriwa na zaidi ya makampuni makubwa 20 toka Sweden kupitia Chama chao cha Wafanyabiashara na Wawekezaji wa Afrika Mashariki (SWEACC) ambapo Mwenyekiti wake Bw. Jan Furuvald amesema uwekezaji kwenye nchi hizo umekuwa na manufaa kutokana na kuwa na soko kubwa la watumiaji wa bidhaa zao na kuwataka wawekezaji wengine kutoka nchini kwake kuja kuwekeza Afrika Mashariki.
"Sisi Wafanyabiashara na wawekezaji mara nyingi tunaangalia mazingira mazuri ya uwekezaji, kuwekeza kwenye nchi za Afrika Mashariki kunatuhakikishia soko kubwa kwani licha ya kuwa kwenye jumuiya hii pia kuna fursa nyingine za SADC", alisema Furuvald.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu ya "Green Solutions in East African Cities" Suluhisho la Kijani kwenye Majiji ya Afrika Mashariki linalenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwenye majiji yaliyopo kwenye Jumuiya hiyo ambapo kwa Tanzania, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Zungu amesema ili kukabiliana na hali hiyo hatua kadhaa zimechukuliwa.
Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja  na kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo ilikuwa ikichafua mazingira na kuharibu mazalia ya viumbe hai ambapo pia kwa sasa Serikali inahamasisha matumizi ya gesi viwandani, majumbani na kwenye magari ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira na ukataji miti hivyo kwa ajili ya matumizi ya nishati za mkaa na kuni.
Waziri Zungu amesema katika kuhakikisha nishati mbadala inapatikana kwa urahisi Serikali inajenga Bwawa kubwa la kufua umeme la Nyerere ili kuwe na umeme wa uhakika.
Aidha Zungu aliwataka wawekezaji wote waliokwama kupata vibali vya mazingira kutokana na mazingira ya rushwa kufika ofisini kwake kwa ajili ya kupata vibali hiyo.
"Kwa Wawekezaji waliokwama kupata vibali vya mazingira wanione, tutawapatia vibali vyao bila kuhangaika, hakuna jambo baya Duniani kama kumnyima mtu haki yake ili upate pesa, tunathamini wawekezaji na tunathamini uwekezaji katika nchi yetu" alisema Zungu.
Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stellah Manyanya akasema Serikali ya Tanzania imekuwa ikiweka mazingira mazuri ya biashara kwa kuimarisha miundombinu Sera na miundombinu ambapo kwa sasa ujenzi mkubwa wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge unaendelea lengo likiwa ni kuzifanya nchi hizo kunufaika kwa usafirishaji kauli inayoungwa mkono na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro.
"Kazi ya Serikali yetu ni kuweka mazingira mazuri ya Biashara na Uwekezaji yakiwepo ya Sera, Sheria na Miundombinu, kuimarisha Blue print na hali ya kisiasa ambayo ina tija kubwa kiuchumi", alisema Mhandisi Manyanya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.