Habari za Punde

NEWZ ALERT: JAJI MKUU MSTAAFU AUGUSTINO RAMADHANI AFARIKI DUNIA

Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani amefariki Dunia leo saa mbili Asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI-AMEN


CV ya Judge Ramadhani Mwaka 

Nimezaliwa Desemba 28, mwaka 1945 Zanzibar mjini nikiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto wanane, wa kike wanne na wanaume wanne. Ni Mkristo wa dhehebu la Anglikana.-


Nimesoma shule mbalimbali za msingi Mpwapwa mkoani Dodoma 1952 -1953 nikaenda Town School-Tabora nikasoma darasa la tatu hadi la nne mwaka 1954-1956 na darasa la sita na saba nilisoma Kazel Hill sasa inatwa Shule ya Msingi Itetemia mwaka 1957-1958. Na darasa la nane tu mwaka 1959 nikarudi kusoma Mpwawa.

Mwaka 1960-1965 nilijiunga na Tabora School kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha sita. Kwakuwa nilifaulu nilichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1966, na nilisoma shahada yangu ya Sheria na ilipofika Machi 1970 nilihitimu masomo.


Na mwishoni mwa Machi mwaka huo huo wa 1970 nikajiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), niliingia jeshini kama mwanasheria raia mpaka kipindi cha mafunzo ya kijeshi nikaenda kwenye mafunzo na kisha nikarudi kuitumikia JWTZ.

Ilipofika mwaka 1971 nikapewa kamisheni kambi ya Mgulani nikawa Luteni (nyota mbili). Nikaendelea na jeshi hadi mwaka 1977, nikahamishiwa Brigedi ya Faru-Tabora nikiwa na cheo cha Meja.

Mwaka 1978,ndiyo mzee Aboud Jumbe Mwinyi, wakati huo akiwa ni Rais akaniita Zanzibar na kuniteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kipindi hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva.

Aidha Oktoba 1978 niliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar. Na ilipofika Machi 1979 nilirudishwa JWTZ na baada ya muda mfupi nikapelekwa kwenye vita ya Uganda , nikiwa na cheo cha Luteni Kanali na kwenye vita hiyo nilikuwa naendesha Mahakama za kijeshi.

Vita ilipokwisha nikarudi Zanzibar. Januari 8 mwaka 1980 nikaapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, wakati huo nikiwa na cheo cha Luteni Kanali. Nikaendelea na Ujaji Mkuu Zanzibar hadi Septemba 1989 alipoapishwa Jaji Mkuu Zanzibar Hamid Mahamod Hamid.

Hata hivyo Juni 23 mwaka 1989 niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania hadi mapema wiki hii nilivyoteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Nilipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani hapa Bara ndiyo sababu ya kuacha ujaji Mkuu Zanzibar.

Januari 1993 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na niliendelea na nafasi hiyo hadi Januari 2003 na Oktoba 2002 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambapo kipindi changu cha miaka mitano katika tume ZEC kinamalizika Oktoba mwaka huu.

Novemba 2001, niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki nafasi ambayo natakiwa nimalize kipindi changu cha miaka sita Novemba mwaka huu.

Nina mke mmoja ambaye Mungu ametujalia tumebahatika kupata watoto wanne, wawili ni wasichana na wawili ni wavulana.

Mtoto wangu wa kwanza anaitwa Francis (30) huyu ni mwanasheria na anafanyakazi ya uwakili Manchester, Uingereza, Brigeth, huyu ana shahada ya Uandishi wa Habari na anafanyakazi ICAP hapa nchini, Marina ni mfamasia, yuko Liverpool, Uingereza na Mathew naye ni mfamasia, anafanya kazi Liverpool."

Buriani Jaji Mstaafu Agostino Ramadhani

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.