Habari za Punde

Dk. Shein Amewataka Viongozi wa Mikoa ya Pemba Kuwatowa Hofu Wananchi Juu ya Maradhi ya Corona Waendelee Kujikinga na Kufuata Maelekezo ya Wataalam wa Afya.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Mikoa Miwili ya Kaskazini na Kusini Pemba katika ukumbi wa Ikulu Ndogo Chakechake Pemba akiwa katika ziara yake ya siku mbili Kisiwani Pemba.  


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka viongozi wa Mikoa ya Pemba kuwatoa hofu wananchi  juu ya maradhi yanayosababishwa na virusi vya KORONA na badala yake waendelee kujikinga kama walivyopewa maelekezo na wataalamu wa afya.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika Ikulu ndogo, Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, wakati alipofanya mazungumzo na Viongozi wa Mikoa ya  Pemba.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein aliwasisitiza viongozi hao kuendelea na mikakati yao waliyoiweka kisiwani humo katika mapambano ya janga hilo na kuwataka kuendelea kuhakikisha wanatoa maelekezo kwa wananchi kama vile yanayotolewa na wataalamu wa avya.

Alisema kuwa viongozi hao wa Mikoa yote ya Pemba wamefanya kazi kubwa na nzito hasa ikizingatiwa kuwa dunia imepata mtihani mkubwa wa janga la vizurisi hivyo vya KORONA na ndio maana WHO limetangaza kuwa hilo ni jaanga la dunia.

Rais Dk. Shein aleleza namna Serikali zote mbili zilivyolifanyia kazi suala la kupambana na maradhi ya virusi vya KORONA na kuonggeza kuwa kuwa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake ilitoa taarifa zake yakiwemo mambo kumi pamoja na kutoa taarifa kwa kuwaeleleza wananchi juu ya ukweli wa janga hilo.

Alieleza jinsi tahadhari zote zilizotolewa na Serikali kupitia wataalamu wake wa afya ikiwa ni pamoja na uvaaji wa barakoa kwa wananchi wote na kutoa pongezi kwa wananchi kisiwani humo kwa kuitikia wito huo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa yeye na Rais John Pombe Magufuli hawakuwa tayari kuzuia wananchi kusafiri na kufanya shuhuli zao za kimaisha na badala yake waliwataka wananchi kuendelea kuelimishwa juu ya kujikinga na janga hilo.

Aidha, Rais Dk. Shein alipongeza juhudi zilizochukuliwa na viongozi hao wa Mikoa ya kisiwani Pemba na kusisitiza kuwa ni vyema juhudi zikaendelezwa katika kuwaelimisha watu hasa wale wa vijijini.

Alieleza kuwa wapo baadhi ya watu ambao hawatoi ushauri mzuri kwa Serikali na wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii vibaya kuilazimisha Serikali jambo ambalo Serikali haiko tayari kulazimishwa katika kufanya wanavyotaka wao.

Hivyo aliwataka viongozi hao kutowasikiliza watu wa aina hiyo na kuwataka kuendekea kuisikiliza Serikali yao huku akiwataka kuendelea kutoa maelekezo sahihi kwa wananchi.

 Rais Dk. Shein alisema kuwa jambo la msingi ni kuzingatia afya na nidhamu katika kujikinga, kuwaelekeza wananchi namna ya kujifunza pamoja na kujikinga kwani Tanzania bado haijafikia hatua ya kuwafungia wananchi kutotoka nje.

Alieleza kuwa SMZ na SMT haikatai kushauriwa lakini anaetaka kutoa ushauri ama maoni yake atoe kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo na sio kuandika mitandaoni kwani Serikali zote mbili zitafanya lile ambalo  zitahakikisha zitawasaidia wananchi.

Alileza kuwa nchi nyingi duniani zikiwemo za Ulaya zimekuwa zikishirikiana katika kupambana na maradhi hayo na ndio maana Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kushirikiana.

Dk. Shein alisisitiza haja ya kuendelea kuwasisitiza wananchi kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji ya kutiririka, kutumia vitakasa mikono pamoja na kufuata taratibu zote za kinga zinazotolewa na wataalamu wa afya pamoja na viongozi wa Serikali.

Akieleza haja kwa Kamati ya Ulinzi na usalama kisiwani Pemba, Dk. Shein alisisitiza haja kwa Kamati hiyo kufanya kazi zake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutumia taratibu za kisheria katika kuwaelekeza wananchi juu ya mapambano ya janga hilo na atakaekaidi ni vyema akachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, alieleza kuwa Serikali haitowaonea wananchi bali itaendelea kuwaelekeza ukweli juu ya janga hilo.

Alieleza kuwa ni lazima viongozi hao wakawapongeza wananchi kwa kuendelea kuiamini Serikali yao kwani wengi wao wanafuata  taratibu na maelekezo ya Serikali na yale maeneo ambayo bado hayajafanya vizuri katika kufuata maelekezo ya kinga elimu iendelezwe ikiwa ni pamoja na kuwapeleka wataalamu wa afya kwenda kuielimisha jamii hiyo.

Rais Dk. Shein aliwataka viongozi hao kuendelea kuwasisitiza wananchi kufanya kazi kwa kasi kubwa ikiwa ni pamoja na kuwataka wakulima kuzitumia vyema mvua za masika ili chakula kiendelee kupatikana hapa nchini.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka viongozi hao kuwaelekeza wafanyabiashara kuuza bidhaa zao kwa kufuata misingi yote ya biashara kama ilivyowekwa na Serikali bila ya kuwawekea wakati mgumu wananchi katika kupata bidhaa muhimu.

Alieleza kuwa kutokana na kasi kubwa ya mapambano ya janga hilo zinavyoendelea hapa nchini anamatumaini makubwa katika kufanikiwa kuyapiga vita maradhi yanayosababishwa na virusi vya KORONA.

Aliwataka viongozi kutojenga hofu na badala yake waendelee kupambana hasa ikizingatiwa kuwa maradhi hayo ni thakili na ni adui asiyeonekana huku akisisitiza haja ya kutowafanyia unyanyapaa wale waliokumbwa na maradhi hayo.

“Nakupongezeni kwa kufanya kazi kubwa na nzito  kwa mafanikio na hapana hata mmoja aliyekuwa hajasikia namna viongozi wa Pemba mlivyofanya jitihada na sote tumeridhika na juhudi zenu....dunia imepata mtihani, dunia imepata msukosuko”,alisema Dk. Shein.

Aliwapongeza kwa dhati viongozi hao kwa jitihada kubwa sana wanazozichukua viongozi hao katika kupambana na janga hilo na kusisitiza kuwa hakuna wa kulaumiwa na kuwataka kupeleka salamu zake kwa wananchi, viongozi wote wa Wizara ya Afya.

Pia, aliwapongeza Walinzi wa Vikosi vya ulinzi na Usalama viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi wote pamoja na wafanyabiashaara na wasiofanya biashara kwa kutoa misaada Unguja na Pemba katika kusaidia mapambano hayo.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kumpongeza Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd akiwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar na Wajumbe wake pamoja na Kamati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kupambana na janga hilo kwa kufanya kazi vizuri.

Mapemba Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu, akimkaribisha Rais Dk. Shein alimpongeza Rais Dk. Shein kwa hatua yake hiyo ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi hao wa Mikoa ya Pemba. 

Nao Wakuu wa Mikoa   ya Pemba wakiwasilisha taarifa za mikoa yao walieleza kuwa wananchi wanaendelea kushirikiana katika shughuli mbalimbali za maendeleo na Serikali inaendelea kuwapelekea maendeleo wananchi wake.

Walieleza kuwa Mikoa yao inaendelea kupambana na suala zima la Udhalilishaji, rushwa pamoja na kupambana na maradhi ya virusi vya KORONA, huku akisisitiza kuwa hali ya siasa katika Mikoa hiyo vizuri.

Waliongeza kuwa wananchi wanaendelea kushirikiana kama kawaida pamoja na  kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama iko vizuri sambamba na kuhakikisha wafanyabiashara hawapandishi bei za vyakula hasa kutokana na visingizio vya KORONA.

Aidha, walimpongeza Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Rais Dk. Shein kwa kulisimamia vyema janga hilo kwa kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kimaisha bila ya kusitishwa usafiri, na kutowekwa karantini ya kutokutoka ndani na kufunga mipaka.

Viongozi hao walielza mafanikio yaliopatikana ikiwa ni pamoja na muitikio mkubwa wa wafanyabishara kwa kuweka maji na vitakasa mikono, muitikio mkubwa kwa kujali muda wa huduma za masoko, kuvaa barakoa, kuwapatia vyakula wagonjwa walioko makambini pamoja na kutoa taaluma.

Walipongeza mashirikiano makubwa wanayopata kutoka katika Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuhakikisha wananchi wanaosafiri kwenda kisiwani Pemba wakitokea Unguja wote wanavuaa barakoa.

Pia, viongozi hao walieleza hatua zinazochukuliwa kuhakikisha wananchi wanavaa barakoa, kuondosha mikusanyiko, kusimamia na kufuatilia watu wote waliopata maradhi hayo na wale waliokuwa karibu na wagonjwa pamoja na wanaoingia katika Mkoani hiyo kwa kuwaweka katika uangalizi maalum wa siku 14 wasafiri wanaoingia katika Mikoa hiyo ili kujiridhisha iwapo hawajaambukizwa na maradhi hayo.

Pamoja na hayo, wakuu wa Mikoa hao walieleza maafa ya mvua yalioathiri nyumba pamoja na mazao katika Mikoa hiyo huku wakieleza kuwa licha ya athari hizo mvua hizo hazikuathiri sana miundombinu ya barabara na madaraja hali iliyopelekea njia zote kuendelea kupitika vizuri.

Viongozi hao kwa pamoja  walimpongeza Rais Dk. Shein kwa hatua aliyoichukua yeye mwenyewe ya kwenda kisiwani Pemba na kuwapongeza kwa juhudi zao wanazozichukua katika kupamabana na janga hilo kisiwani humo

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.