Habari za Punde

RC Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe Hassan Awataka Wenye Uwezo Kusaidia Wenye Mahitaji Mayatima

Meneja wa Benk of Africa (BOA) Tawi la Zanzibar Ndg.Juma Burhan Mohammed (kulia ) akimkabidhi  msaada wa Vyakula Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Hassan Khatib Hassan, kwa ajili ya familia za Watoto yatima, hafla hiyo imefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Vuga Jijini Zanzibar.
MKUU wa mkoa wa Mjini Magharibi Hassan Khatib Hassan (wa pili kushoto) akimkabidhi mmoja ya wazazi wanaolea watoto yatima maada wa vyakula uliotolewa na Bank of Africa (BOA) tawi la Zanzibar. wa kwanza kushoto ni Meneja wa tawi hilo Juma Burhan Mohamed
MENEJA wa Bank of Africa tawi la Zanzibar Juma Burhan Mohamed (wa pili kushoto) akimkabidhi Mlezi Mkuu wa kituo cha kulelea watoto yatima Mazizini msaada wa vyakula mbali mbali vilivyotolewa na benki hiyo kwa ajili ya futari.
 (PICHA NA MZEE GEORGE).
Na.Mzee Georg - Zanzibar.
WATU wenye uwezo, taasisi za biashara na jamii kwa ujumla imetakiwa kuwahudumia na kuwatunza watoto yatima ili kuwaondolea unyonge wa kuondokewa na wazee wao.
Akizungumza baada ya kupokea msaada wa vyakula vya futari kwa ajili ya watoto yatima wa majumbani na kituo cha kulelea yatima cha Mazizini, mkuu wa mkoa wa mjini magharibi hassan khatib hassan alisema kufanya hivyo kutasaidia kupata jamii bora na yenye maadili.
Alisema ili kuwa na jamii yenye maadili na kujali, ipo haja kwa kila mwenye uwezo kuwajali watu wasio na uwezo hasa mayatima kama inavyoelekezwa na vitabu vya dini.
“Msaada huu umekuwa na maana sana kwa kuwa mmewalenga mayatima kwani kufanya hivyo sehemu ya utekelezaji wa ibada kama alivyotuhimiza Mwenyezi Mungu kuwa tulisaidia kundi hili,” alieleza Hassan.
Aidha aliwataka wazazi na walezi kuzingatia wajibu wao kwa kuwalea watoto hao katika maadili mema sambamba na kuwalinda dhidi ya majanga yakiwemo maradhi ya covid 19 yanayosababishwa na virusi vya corona.
“Serikali imeweka mipango na mikakati ya ulinzi wa watoto, hivyo na nyinyi mnapaswa kuhakikisha wototo wanakuwa salama hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa corona,” alisema.
Alisema iwapo wazazi watashirikiana na kuwadhibiti watoto wao, kuna uwezekano kuwaepusha na maambukizi ya maradhi hayo yaliyoenea ulimwenguni.
“Iwapo wazazi hasa kina mama mkitukazania kina baba na watoto kujilinda dhidi ya corona, sote tunaweza kuwa salama,” alisema RC Hassan.
Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Meneja wa Bank of Africa (BOA) tawi la Zanzibar Juma Burhan Mohamed alieleza kuwa msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa benki hiyo kutumikia jamii.
Alisema benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kutoa misaada mbali mbali kwa jamii ikiwemo ya futari katika mwezi wa ramadhani, hivyo kwa mwaka huu iliamua kutoa kwa kundi hilo baada ya kuzingatia hali halisi ya maradhi.
“Kikawaida kila mwaka huwa tunafutari pamoja na wateja wetu sambamba na kutoa misaada kwa watu wenye mahitaji ila kutokana na maradhi tumeamua kutoa vyakula vikavu kwa watoto yatima ili nao waweze kufunga kwa urahisi zaidi,” alisema Mohamed.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi na walezi wengine, Mama Mlezi Mkuu wa kituo cha kulelea watoto yatima Mazizini pili saadalla mussa alieleza kuwa msaada huo umetolewa kwa watkati muafaka na kuahidi kuwa utatumika kama ulivyokusudiwa.
“Kwa niaba ya Idara ya Ustawi wa Jamii na wizara kwa ujumla tunaishukuru benki ya BOA kwa kutusaidia kwani licha ya kupata huduma kutoka serikalini, bado tuna mahitaji ambayo yanapaswa kutoka kwa watu binafsi kwani watoto hawa ni wa jamii nzima,” alieleza mama huyo.
Msaada huo ambao uliogawiwa kwa familia zinazolea watoto yatima wa mkoa wa Mjini Magharibi, BOA ilikabidhi mchele, sukari, unga wa ngano na mafuta ya kupikia katika hafla iliyofanyika katika ofisi za baraza la manispaa Magharibi ‘B’ na kituo cha kulelea watoto yatima Mazizini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.