Habari za Punde

Wanafunzi wa Kidatu Cha Sita Kuanza Masomo Yao 1/6/2020 na Ligi Kuu ya Zanzibar Nayo Kuanza 5/6/2020

 
Uongozi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} ukimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Kituo cha Matangazo Karume House kutoa Taarifa ya Serikali kuhusu kuregeza masharti yaliyowekwa kuhusiana na Ugonjwa wa Corona.
Mtayarishaji wa Vipindi vya Afya katika Kituo cha Matangazo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} Bibi Mwanakhamis Sose akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kumaliza kutoa Taarifa ya Serikali.
Balozi Seif Ali Iddi akiagana na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Nd. Chande Omar Omar na Naibu Wake Bibi Nasra Mohamed mara baada ya kumaliza kutoa taarifa ya Serikali kuhusu Corona.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukuwa uamuzi wa kuregeza baadhi ya mambo mambo kumi yaliyowekwa baada ya kufanikiwa kukabiliana kwa kiasi kikubwa na mripuko wa Virusi vya Coroma vilivyoleta mtafaruki katika Mataifa mbali mbali Duniani.
Uamuzi huo wa SMZ Unaungana na ule uliochukuliwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuviruhusu Vyuo vyote vya Elimu ya juu kuendelea na Programu zao kama kawaida kwa upande wa Zanzibar kuanzia Tarehe 1 Juni 2020.
Akitoa Taarifa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Umma kupitia Vyombo vya Habari Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uamuzi huo unakwenda sambamba na Wanafunzi wa Kidato cha Sita nao kuanza masomo yao Tarehe 01 Juni 2020 ili kuwawezesha kujitayarisha na Mitihani yao ya Taifa.
Alisema kufuatia maamuzi hayo Serikali imeiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya  Amali kushirikiana na kikamilifu ya Wizara ya Afya katika kuandaa miongozo ya Kiafya itakayopaswa kuzingatiwa ili kuepuka maambukizo pamya ya Virusi vya Corona.
Balozi Seif alibainisha kwamba Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza hadi cha Tano pamoja na Wanafunzi wa Skuli za Msingi, Maandalizi na Madrasa, Skuli na Vyuo vyao zitaendelea kufungwa hadi pale yatakapotolewa maelekezo mengine na Serikali Kuu.
Kuhusu Mchezo wa Soka Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Ligi Kuu ya Zanzibar itaendelea kuanzia Tarehe Tano Juni 2020 ambapo Wizara inayosimamia Sekta ya Michezo kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar {ZFF} pamoja na Wizara ya Afya ziandae Muongozo na namna bora ya kuendesha Ligi hiyo.
Kwa upande wa Michezo mengine yote inayochezwa na Vilabu, Vikundi au Makundi ya Wananchi na hata Mtu Mmoja Mmoja ikiwemo Mazoezi, Mashindano ya Viwanjani na Ufukweni Balozi Seif alisema Makundi yote hayo yatasubiri hadi itakapotolewa Taarifa nyengine hapo baadae.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba tokea kuripotiwa kwa rasmi kwa Ugonjwa wa Corona mnamo Tarehe 19 Machi 2020, Serikali imekuwa ikifuatilia kwa karibu muenendo wa Ugonjwa huo.
Alisema hadi kufikia leo Tarehe 27 Mei 2020 Watu wapatao 134 wamethibitishwa kuambukizwa Virusi vya Ugonjwa wa Corona , kati yao Wagonjwa 109 wamepatikana Unguja na Wagonjwa 25 wameripotiwa Kisiwani Pemba  wakati Wagonjwa Sita walifariki Dunia.
Balozi Seif alifafanua kwamba jumla ya Wagonjwa 115 wamepona ambapo hadi sasa  wamebakia Wagonjwa 19 wakiendelea na huduma za Afya katika  Kambi za matibabu za Kidongo Chekundu, Skuli ya Sekondari ya JKU Mtoni, Kihinani na Kidimni kwa Upande wa Unguja wengine katika Kituo cha Vitongoji kwa upande wa Kisiwa cha Pemba.
Alisema jitihada hizo zote zimefanikiwa kutokana na utekelezaji wa maelekezo na maagizo ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa akiwemo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein ambao wanastahiki kupongeza kwa dhati.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Jamii Nchini kwa jitihada inazochukuwa za kuitikia wito na Ushauri wa Serikali pamoja na Wataalamu wa Sekta ya Afya katika suala zima la mapambano dhidi ya Virusi hatari vya Corona { CAVID – 19}.
Alisema Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeridhika na juhudi hizo zilizoleta faraja kubwa kwa kila Mwananchi kuendelea kuishi kwa matumaini na kuwataka waondoe hofu kutokana na janga hilo lililoiathiri Dunia hivi sasa.
Hata hivyo Balozi Seif  alitahadharisha kwamba pamoja na Serikali Kuu kuregeza masharti yaliyotolewa ya kukabiliana na Maradhi yanayotokana na Virusi vya Corona aliwasisitiza Wananchi kwamba lazima waelewe kuwa maradhi hayo bado yapo na ni tishio linaloendelea kutishia Afya za Wanaadamu Ulimwengu mzima.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa Tamko Rasmi mnamo Tarehe 19 Machi 2020 na kulekeza Mambo Kumi ya kutekelezwa katika kuhudumia Waathirika wa Virusi vya Corona sambamba na udhibiti wa Maradhi yanayosababishwa na Virusi hivyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.