Habari za Punde

WAZIRI KAIRUKI ARIDHISHWA NA UWEKEZAJI WA KIWANDA CHA MAFUTA YA ALIZETI CHA MAGID - KONDOA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (wa tatu kushoto) akiwa kwenye ziara ya kukagua kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha MAGIN Ltd Kilichopo Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma iliyofanyika Mei 21, 2020.    Wa pili kushoto ni Mkuu wa hiyo Mhe. Sezaria Makota.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akitoa maelekezo ya ufuatiliaji kwa Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Kanda ya Kati Bw. Revocatus Rasheli wakati wa ziara ya kukagua kiwanda hicho cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha MAGIN Ltd Kilichopo Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akitoa maelekezo kwa timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, mkoa na wilaya wakati wa kuhitimisha  ziara yake  leo Mei 21, 2020 Wilayani Kondoa Mkoani Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akimsikiliza Kaimu Meneja Mkuu wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha MAGIN Ltd Bi. Aisha Suleiman alipofanya ziara ya kukagua maeneo ya uwekezaji leo (Mei 21, 2020) kilichopo Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota akitoa taarifa fupi ya masuala ya uwekezaji katika wilaya hiyo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipofanya ziara ya kukagua maeneo ya uwekezaji Wilayani humo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akitoa majumuisho wakati akihitimisha ziara yake leo Mei 21, 2020 Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma.
                             (PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
NA. MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki ameeleza kuridhishwa na hatua za uwekezaji wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula cha MAGIN kilichopo Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma kwa kuwa na mitambo yenye ubora na chenye nia ya kuzalisha mafuta kwa tija nchini.
Ameeleza hayo mapema hii leo (21 Mei, 2020) alipotembelea maeneo ya uwekezaji katika Wilaya za Mkoa wa Dodoma ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake katika mkoa huo ili kujionea mazingira ya wawekezaji nchini na kusikiliza na kutatua kero zao.
Waziri Kairuki alikipongeza kiwanda hicho kuzalisha mafuta yenye ubora na kupatikana kwa urahisi kwa kuzingatia uwepo wa malighafi za kutosha zinapatikana nchini na kueleza imeongea motisha kwa wawekezaji hao.
 “Ninawapongeza kuona fursa ya kuwekeza katika mafuta ya kula na hii ni sahihi kwa kuzingatia ukanda huu una alizeti nyingi na kuwa na uhakika wa malighafi ya uzalishaji,”
Waziri kairuki aliongezea kuwa, uwekezaji huo umekuwa na tija kwani ni zao linalolimwa kwa wingi ukanda huo na hii itasaidia kutatua changamoto ya uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi na kuwaasa kutumia fursa hiyo kuzalisha kwa wingi na ubora wa hali ya juu.
“Kama nchi tumekuwa tukizalisha mafuta kwa asilimia 40 tu na alilimia 60 kuagiza mafuta kutoka nje ambapo imekuwa ikitumia fedha nyingi, uwepo wa kiwanda hiki utasaidia kuokoa fedha hizo na kuongeza tija katika uchumi wa taifa letu,”alisema Waziri Kairuki
Alieleza kuwa, uamuzi wa kuwekeza katika mafuta ni sahihi kwani taifa limekuwa likipoteza zaidi ya shilingi Bilioni 443  kwa mwaka kwa uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi.
Aidha, alieleza kuwa Serikali itaendelea kuweka nafuu za kikodi kwa wawekezaji ili kuziangalia sekta zenye upungufu ikiwemo ya mafuta ya kula na sukari, na kuendelea kutoa rai kwa benki kuendelea kusaidia vyama vya wakulima kuhakikisha kunakuwa na mnyororo wa thamani katika sekta ya uwekezaji nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Sazaria Makota alimpongeza waziri kwa ziara yake na kuendelea kuahidi kutekeleza maagizo na ushauri wake hasa katika kuhakikisha wanatatua changamoto za wawekezaji ikiwemo suala la ukosefu wa umeme wa uhakika, maji pamoja na huduma muhimu za kijamii zinazozunguka maeneo ya wawekezaji.
“Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikifuatilia wawekezaji nchini akiwemo Mzee Mavere ambaye amekuwa na tija katika nchi yake na kuonesha uzalendo na tutaendelea kumuunga mkono kwa vitendo,”alisema Sazaria
Aliongezea kuwa, awali alikuwa anazalisha tani 24 kwa siku na kufikia kuwa na mtambo wa kisasa wa solvent destruction plant unaotumika kukamua na kutoa mafuta yenye ubora ambapo kwa sasa anazalisha kwa siku tani 50 na kulenga kufika tani 100.
Aidha aliahidi kuendeleza jitihada zilizopo za kuhakikisha wawekezaji wazawa wanawezeshwa na mamlaka za kifedha ikiwemo wepesi wa upatikanaji wa mikopo na kwa kusaidia katika kukuza na kuendeleza shughuli za uwekezaji wao.
“Nitoe wito kwa mabenki yote ikiwemo CRDB ambao wamekuwa bega kwa bega tangu kuanzishwa kwa kiwanda hiki cha mafuta hadi hatua hii, kuendelea kuwasaidia kwa ushauri na kifedha,”alisisitiza Sazaria
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Bi, Aisha Suleiman alishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inasikiliza na kutatua kero zinazowakabili na kuomba kuendelea kuwaunga mkono katika uwekezaji wao hapa nchini.
Aidha Meneja wa Tawi la CRDB Kondoa, Juma Mshihiri alionesha nia ya kuendeleza jitihada za Serikali katika kuwapatia huduma za kifedha wawekezaji kwa kadri iwezekanavyo na kuhakikisha wana wahudumia kwa kuzingatia mazingira yaliyopo.
“Tupo tayari kutoa ushauri wa kifedha katika kuendesha miradi, tumekuwa na wafanyabiashara wadogo tukiwatoa ngazi za chini hadi kuyafikia malengo yao ili kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha inatimiza azma ya uchumi wa viwanda kwa kuwapatia mikopo yenye tija na riba nafuu ,”alisema Juma

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.