Habari za Punde

Waziri Mwakyembe Azitaka Ofisi za Umma kutoa Taarifa Kwa Wanahabari

  Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza na uongozi wa Arusha Press Club  kuhusu namna bora ya kutekeleza majukumu yao  kwa kuzingatia Sheria na kanuni za Habari  leo Jijini Dodoma.
 Mwenyekiti wa Arusha Press Club Bw.Claud Gwandu akizungumza jambo wakati wa kikao na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe (kulia)  ambapo walijadiliana masuala mbalimbali yanaohusu  tasnia ya habari  leo Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Hassan Abbas akizungumza katika kikao cha Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Harrison Mwakyembe (kushoto) pamoja na Uongozi wa Arusha Press Club kuhusu namna bora ya kutekeleza majukumu yao ya kutoa habari sahihi kwa wananchi leo Jijini Dodoma.

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe akipokea kipeperushi cha majukumu ya  Uongozi wa Arusha Press Club mara baada ya kumaliza kikao na Uongozi huo kuhusu namna bora ya kutekeleza majukumu yao ya  kihabari  leo Jijini Dodoma.

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imezitaka ofisi za Umma kutoa taarifa kwa wanahabari kwa kuwa siyo hisani na siyo hiyari, bali ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 (d).

Kauli hiyo imetolewa na Waziri mwenye dhamana ya tasnia ya Habari Dkt. Harrison Mwakyembe alipokutana na ujumbe wa viongzi wa Chama cha Waandishi wa Habari kutoka mkoani Arusha pamoja na Asasi ya Vyombo vya Habari Mbadala (Alternative Media) leo jijini Dodoma.

“Serikali haina ugomvi na vyombo vya habari, bila vyombo vya habari hatutaweza kuwahabarisha wananachi masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu” amesema Dkt. Mwakyembe.

Aidha, amewakumbusha wanahabari kuwa kazi wanayofanya ni muhimu sana ambapo nchi zilizoendelea bado wanatumia vyombo vyao vya habari ikiwemo Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambalo lina miaka zaidi ya 90 na linatangaza habari zake kwa lugha zaidi ya 40 ili kuwafikia wananchi wake na dunia kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari kutoka mkoa wa Arusha Bw. Claud Gwandu amemshukuru Waziri Dkt. Mwakyembe kwa mapokezi, majadiliano yenye tija kwa uwazi na ukweli na kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya katika sekta anazozisimamia.

“Tunamshukuru Waziri kwa kutupa nafasi ili tuweze kushirikiana katika kuimarisha tasnia ya habari iwe bora kwa mustakabali wanchi yetu” amesema Gwandu.

Aidha, Mwenyekiti huyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya kwa kutekeleza miradi mingi kwa manufaa ya Watanzania na kusisitiza kwa mwenye macho haambiwi tazama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.