Habari za Punde

ZAT na Royal Group watoa misaada wa vifaa kwa ajili ya Watu wenye Mahitaji Maalum (Walemavu)

 Mwenyekiti wa Makampuni ya ZAT na Royal Group Mh. Mohamed Raza Hassanali akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi msaada wa Vifaa mbali mbali kwa ajili ya Watu wenye Mahitaji Maalum {Walemavu }. 
Kati kati ya Mh. Raza na Balozi Seif ni Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni hayo Ndugu Hassan Mohamed Raza.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia Fimbo maalum kwa ajili ya Wananchi wasioona zilizotolewa na Mwenyekiti wa Zat na Royal Group Mh. Raza.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Uzini Ndugu Haji Shaaban Waziri Vyakula mbali mbali kwa Familia 218 za Wananchi wa Jimbo la Uzini zilizotolewa na Mwakilishi wao Mh. Mohamed Raza.
 Afisa Jinsia Maendeleo wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Nd. Foum Shaaban akitoa shukrani mara baada ya kupokea msaada wa Vifaa mbali mbali vilivyotolewa na Mwenyekiti wa Makampuni ya Zat na Royal Group.
  Mwenyekiti wa Makampuni ya ZAT na Royal Group Mh. Mohamed Raza Hassanali akizungumza kabla ya kukabidhi msaada wa vifaa mbali mbalki kwa ajili ya Wananchi wenye Mahitaji Maalum Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Zat na Royal Group Nd. Hassan Mohamed Raza akielezea msimamo wa Makampuni yake wa kuunga mkono jitihada za Serikali wakati wowote yatakapohitajika kufanya hivyo.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis , OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema mchango mkubwa wanaoendelea kutolewa na Wafanyabiashara Wazalendo Nchini utabakia kuwa kielelezo cha ukumbusho kwa Jamii inayowazunguuka pamoja na Taifa kwa Ujumla.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akipokea msaada wa Vifaa mbali mbali kwa ajili ya Watu wenye Mahitaji Maalum {Walemavu} hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar vilivyotolewa na Mwenyekiti wa Makampuni ya ZAT na Royal Group Mh. Mohamed Raza Hassanali.
Msaada huo ulikwenda sambamba na Mh. Raza ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini kukabidhi Maski 400 kwa Wananchi wa Jimbo la Uzini pamoja na Vyakula mbali mbali kwa ajili ya Familia 218 zilizokumbwa na Maafa ndani ya Jimbo hilo kufuatia Mvua Kubwa zilizokuwa zikinyesha hivi karibuni hapa Nchini.
Balozi Seif alisema Wananchi walio wengi Nchini wamekuwa wakipata fuaraja kutokana na nguvu kubwa zinazochukuliwa na Wafanyabaishara Wazalendo katika kuwaunga mkono hasa wakati wanapokumbwa na mitihani ya Majanga mbali mbali.
Aliupongeza Uongozi wa Makampuni hayo ya ZAT na Royal Group kwa jitihada unazochukuwa wa kuwa karibu na Wananchi sambamba na Serikali katika kuona ustawi wa Jamii unaendelea kubakia salama na furaha licha ya matukio ya changamoto zinazojichomoza kwa baadhi ya wakati.
Akizungumzia athari ya Mafuriko ya Mvua za Masika za Mwaka huu, Balozi Seif akiwa ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar aliwatahadhari Wananchi kuendelea kuepuka kujenga Makaazi yao ya kudumu katika maeneo hatarishi.
Alisema maeneo ya kilimo, sehemu za Mabwawa, Mito pamoja na misingi ya maji ya mvua ni vyema zikaepukwa mapema ili kujihakikishia usalama wa maisha yao sambamba na hasara kubwa inayoweza kuleta usumbufu wa mchanganyiko wa mawazo yasiyokwisha ndani ya maisha yao.
Mapema Mwenyekiti wa Makampuni ya ZAT na Royal Group Mheshimiwa Mohamed Raza Hassanali alisema Uongozi wa Taasisi hizo umefikia hatua ya kutoa msaada huo kufuatia changamoto mbali mbali zinazowakumba Watu wenye Mahitaji Maalum.
Mh. Raza alisema changamoto hizo zilijitokeza Mwezi Disemba Mwaka uliopita wakati wa dhifa Maalum aliyowaandalia Wananchi wenye Mahitaji Maalum           {Walemavu} ambapo aliahidi kutoa Baskeli 20 za Walemavu, Vyarahani 20 pamoja na Fimbo 20 zitakazogaiwa na kusambazwa kwa Visiwa vyote viwili vya Unguja na Permba.
Mwenyekiti huyo wa Makampuni ya ZAT na Royal Group alielezea faraja yake kutokana na usimamizi mkubwa wa Serikai kwenye utekelezaji wa huduma pamoja na Miradi ya Ustawi wa Jamii ambao umekuwa chachu kwa Wafanyabiasha  na Makampuni kujitokeza kuunga mkono jitihada hizo.
Mh. Raza alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Makampuni hayo yenye uzoefu wa Miaka mingi katika kutoa huduma  utazidi kuendelea kushirikiana na Serikali  katika Sekta mbali mbali Nchini.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi, Watendaji wa Idara ya Watu wenye Ulemavu pamoja na Watu wenye Mahitaji Maalum, Afisa Jinsia Maendeleo wa Idara hiyo Nd. Foum Shaaban alisema milango bado iko wazi kwa Mtu au Taasisi yoyote ndani na nje ya Nchi kusaidia kundi hilo la Watu wenye Mahitaji Maalum.
Nd. Foum alisema msaada huo wa Baskeli za Walemavu, Vyarahani pamoja na Fimbo Maalum za kuwaongoza Watu wasioona zitagaiwa kwa wahusika Unguja na Pemba kwa mujibu wa taratibu zilivyopangwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.