Habari za Punde

DKT. MPANGO: SIJARIDHISHWA NA ENEO LILIPOJENGWA SOKO LA KIMATAIFA KIGOMA

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isodor Mpango (Mb), akitoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya kuhusu soko la Mnanila lililopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma alipotembelea ujenzi wa mradi wa soko hilo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina na kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Rashid Mchata.
Wananchi wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo pichani), alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Soko la Kimkakati Mnanila, lililopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

Na Josephine Majura, Peter Haule-KIGOMA
WAZIRI wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kutafuta eneo jipya, kubwa, lenye hadhi ya kujengwa soko la Kimataifa badala ya eneo linapojengwa Soko la Kimkakati la Kimataifa la Mnanila, lililoko katika mpaka wa Burundi na Tanzania.
Maagizo hayo ameyatoa wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa soko hilo la Kimkakati la Kimataifa akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayopatiwa fedha na Serikali.
Dkt. Mpango alisema kuwa hajaridhishwa na ubora wa ujenzi wa soko hilo ambalo linatarajiwa kuwa la kimataifa kutokana na kujengwa katika eneo dogo, na ujenzi wake uko chini ya kiwango ikilinganishwa na kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kilichotumika kujenga miundombinu ya mradi huo uliolenga kuchochea shughuli za biashara na kiuchumi kati ya wananchi wa Tanzania na Burundi.
Alisema kuwa atatuma timu ya wataalamu kuchunguza na kufanya ukaguzi maalaum ili kubaini watu waliohusika kushauri soko hilo lijengwe katika eneo lisilokuwa na hadhi pamoja na kuchunguza matumizi ya fedha za mradi huo zilivyotumika.
Aidha, Dkt. Mpango alisema iwapo utabainika udanganyifu wa matumizi ya fedha hizo hatua kali zitachukuliwa na kwa kuanzia ataanza na ofisini kwake kujua vigezo vilivyotumiwa na wataalam wake walioishauri Wizara iidhinishe matumizi ya kiasi hicho cha fedha huku wakijua kuwa eneo linalojengwa mradi huo halina sifa ya kujengwa miundombinu
“Mtafute eneo lingine tofauti ambalo linaweza kweli  kubeba dhana ya Soko La kimataifa ili tukuze biashara  na wananchi wetu wapate kipato na Halmashauri iweze kulipa na kugharamia maendeleo ya nchi yetu lakini kwa mawazo madogo hivi hatuta sogea” alisema Dkt. Mpango.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina, amesema atashughulikia kwa haraka dosari zilizobainika katika ujenzi wa Soko la Mnanila. Ambalo malengo yake ni kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza kipato cha Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe na mkoa wa Kigoma kwa ujumla ili iweze kujitegemea.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilayaya Buhigwe Bw. Anosta Nyamwoga, alimuahidi Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), kwamba Halmashauri yake itatafuta eneo jipya kwa ajili ya ujenzi wa soko kubwa la kimataifa kwa haraka.
Awali, baadhi ya wakazi wa Kata ya Mnanila, akiwemo Bw. Amon Ndabita, walieleza kutoridhishwa na ujenzi wa soko hilo na kwamba hawajashirikishwa katika kupendekeza eneo linalofaa kwa ujenzi wa soko hilo la kimkakati la kimataifa ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu shilingi bilioni 2.3 zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango chini ya radi wa kuziwezesha Halmashauri kujitegemea kimapato.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) alimpa muda wa siku 15 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Bw. Anosta Nyamwoga, kuwalipa mamalishe, vibarua, mafundi waliojenga Soko hilo la Kimkakati la Kimataifa Munanila ambao wamelalamika mbele yake kutolipwa fedha zao tangu mwezi Julai mwaka 2019.
“Nakuagiza uwalipe fedha zao zote wanazodai na utajua utakako zitoa fedha hizo, uwalipe na wewe utawadai wakandarasi wakulipe fedha zako kwani ulitakiwa kuhakikisha wananchi hawa wanapata haki zao” alisisitiza Dkt. Mpango
Dkt. Mpango yuko katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma kukagua miradi ya maendeleo inayopewa fedha na Serikali ambapo ametembelea Miradi ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Munzeze, Ujenzi wa Jengo la Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe na Ujenzi wa Soko la Kimkakati la Kimataifa Mnanila.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.