Habari za Punde

Serikali Yazindua Mwongozo wa Taifa wa Uendshaji wa Shughuli za Utalii Nchini Tanzania Wakati Huu wa Janga la Corona.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Wadau wa Sekta ya Utalii na Waandishi wa Habari leo jijini Arusha wakati wa Uzinduzi rasmi wa Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji wa shughuli za Utalii nchini Tanzania wakati huu wa janga la CORONA.

Serikali imezindua rasmi mwongozo wa uendeshaji wa Shughuli za Utalii nchini Tanzania wakati huu wa janga la Corona na kuwataka wadau sekta hiyo kuzingatia matakwa yaliyo katika mwongozo huo ili kulinda usalama wa Watanzania na watalii wanaowasili nchini kutembelea vivutio vilivyopo.

Akizindua mwongozo huo leo jijini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amewataka wadau wote wa Sekta watimize wajibu wao kwa kuhakikisha wageni wote wanaoingia nchini wanakuwa salama na wanaondoka salama pasipo kuambukizwa au kuambukiza wengine virusi vya Corona.

Dkt. Kigwangalla amesema Serikali imeamua kuzindua rasmi mwongozo huo ili kuilinda Sekta ya Utalii pamoja na afya za wadau wote wanaohusika na sekta hiyo na kuongeza kuwa hatua hiyo itaongeza na kujenga imani ya wageni wanaoitembelea Tanzania kutokana na masharti ya kiafya yaliyoainishwa katika mwongozo huo ambayo watoa huduma za utalii wanatakiwa kuyazingatia.

Ameongeza kuwa mwongozo huo huo utaisaidia biashara  ya Utalii kuanza upya wakati huu wa janga la CORONA ambapo Tanzania imeamua kufuangua  mipaka yake kufuatia baadhi ya nchi zikiwemo za Ulaya kuanza kufungua anga kwa  kuruhusu  mashirika makubwa ya ndege kuanzisha safari za ndege za abiria kutua  katika nchi hizo kuanzia mwezi Juni mwaka huu.

 Amebainisha kuwa Tanzania imeondoa masharti mengi ambayo yalikuwa yakikwamisha watalii wengi kuja nchini Tanzania likiwemo lile la mtalii kukaa Karantini kwa muda wa siku 14.

Dkt. Kigwangalla amewahakikishia wageni mbalimbali wanaopanga safari zao kuja nchini Tanzania waje bila hofu yoyote kwa kuwa Tanzania ni nchi salama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.