Habari za Punde

Zaidi ya Barua 100 Zawasilishwa Ofisi ya (DPP) Kutaka Kufutwa Kwa Kesi za Udhalilishaji

Naibu Mrajis wa Mahakama kuu Zanzibar Salum Hassan Bakari akisisiza jambo wakati wa mkutano uliowakutanisha wadau mbali mbali wa sharia  kwa lengo la kuangalia changamoto za kisheria dhidi ya matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.Mkutano huo ulifanyika katika ofisi za TAMWA-ZNZ zilizopo Tunguu Wilaya ya kati.
Wakili wa Serikali kutoka afisa ya Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) Omar Makungu Omar akieleza ni kwanamna gani wanakabiliana na changamoto katika kesi za udhalilishaji hususani jamii inapoandika barua kufuta kesi zao,wakili huyo aliyaeleza hayo katika mkutano uliofanyika ofisi za TAMWA-ZNZ zilizopo Tunguu wilaya ya kati Unguja.
Wajumbe kutoka taasisi mbali mbali za kusimamisha sheria wakiendelea na kikao cha siku moja chenye lengo la kujadili changamoto ya sheria katika matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto Zanzibar,ambapo mkutano huo wa siku moja ulifanyika katika ukumbi wa  ofisi za TAMWA-ZNZ zilizopo Tunguu wilaya ya kati Unguja.

Na.Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ.
Zaidi ya barua ( 100 ) zimewasilishwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka (DPP) zenye lengo la kutaka kufutwa kwa kesi za udhalilishaji wanawake na watoto visiwani hapa katika siku za hivi karibuni.
Hayo yamesemwa na Wakili wa Seikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) Mkoa wa Mjini Magharib Unguja Omar Makungu Omar wakati alipoka akieleza jinsi wanavyokabiliana na chanagamoto dhidi ya kesi hizo katika mkutano maalumu uliofanyika ofisi za TAMWA-ZNZ huko Tunguu Wilaya ya kati Unguja.
Alisema inasikitisha sana kuona kuna juhudi kubwa zinaendelea kufanyika kila leo kupambana na matendo hayo lakini kuna baadhi ya watu kwenye jamii kwa sababu wanazozijua wao wamekua wakiwatakatisha tamaa pale wanapotaka kuchukua hatua zaidi za kisheria.
Alifahamisha  kuwa wakati mwengine baadhi ya kesi zinakua na udhahidi mzuri ambaop ungeweza kumtia mshtakiwa  hatiani lakini ghafla wahusika hujitokeza na kuandika barua kutaka kesi hio iondolewa mahakamani au hata wakati mwengine ikawa bado haijafikishwa kwenye chombo hicho.
Alisema iwapo jamii haitakua tayari na kutaka kubadilika ikiwemo kuziachia kesi ziendelee Mahakamani basi ni wazi kuwa matukio ya udhalilishaji wa kijisnia kwa wanawake na watoto yataendelea kuwepo siku hadi siku kwa kuwa wafanyaji wanaendelea kulindwa na jamii husika.
Nae Afisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Khamis Juma alisema suala la ushahidi uliokidhi vigenzo vyote kwenye kesi za aina hio ni muhimu sana ili kuifanya kesi iweze kuendelea.
Alisema kikawaida iwapo kesi itakosa hoja ndogo ya ushahidi inaweza kupelekea kesi hio kupoteza uzito hatimae kuondolewa Mahakamani na wakati mwengine udhaifu wa aina hio ndio unaotumiwa na mawakili wenye kuwatetea watu wanaoshtakiwa kwa kesi za aina hio.
Hata hivyo alisema anafahamu uwepo wa changamoto za ushahidi ikiwemo baadhi ya wahusika kushindwa kufika Mahakamani au hata kukataa kusema jambo mara kesi zao zinaposomwa na wengine kwenda mbali zaidi kubadilisha maneno kwa lengo la kumtetea mfanyaji.
‘’Ni mara kadhaa tumekutana na kesi za aina hii mwanamke anamlinda mtu aliemfanyia tenda na wengine husema kabisa kwamba ni mtu wake asingekua tayari kuona anapata matatizo’’aliongezea.
Akiendelea kufafanua zaidi  alisema kifungu cha 101(1) cha sharia kimeweka wazi iwapo shahidi ataitwa Mahakamani bika ya kufika au kukataa kutoa ushahidi anatakiwa kuwekwa ndani kwa muda wa siku nane hatimae kuitwa tena na akiendelea kukataa basi atatakiwa kurudi tena ndani mpaka pale atakapokubali kutoa ushahidi.
Awali Naibu Mrajis wa Mahakama kuu Zanzibar Salum Hassan alisema kuna tatizo kwa baadhi ya wanajamii katika maeneo mbali mbali ambao wanapaswa kubadilika.
Alisema kwenye familia imekua kama ni kitu cha kawaida mtu kumuita mwanaume bamkwe wakatu watoto wake wakiwa hapo hapo jambo ambalo alisema ni kutengeneza mazingira ambayo yanaweza kusababisha watoto kufanyika wamatendo mabaya.
Akizungumzia kuhusu uzito wa ushahidi kwneye matukio hayo alisema nako pia kuna mazingira ambayo si rafiki sana ikiwemo pamoja na kutoshirikishwa kikamilifu kwa wahanga wa matukio.
Alieleza kuwa kuna baadhi ya kesi wakati mwengine hadi zinakwenda Mahamani mfanywaji wa tendo hajachukuliwa taarifa za kina na hua hana uelewa wa kutosha kuhusu kesi yake jambo ambalo humpa wakati mgumu hata wa kujieleza.
Akiendelea kufafanua zaidi Mrajis huyo alitoa rai kwa maafisa mbali mbali wenye kusimamia sharia kuhakikisha tangu hatua ya awali wanashirikisha ipasavyo wahusika ili kuweza kupata ushahidi wa kina na wenye kujitosheleza.
Akizungumzia kuhusu kukosekana kwa sharia ya kumlinda shahidi katika kesi za udhalilishaji Zanzibar alisema ipo haja kufanyiwa mabadiliko ya sharia mabyo itawawezesha mamlaka husika kumlinda shahidi nuda wote ili asiweze kubainika jambo ambalo alisema anaamini litaweza kumuweka huru na kutoa ushahidi wake.
Nae Mkurugenzi wa Chama cha wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mohamed alisema wapo baadhi ya watu kwenye jamii wamekua wakiyachukulia matukio  ya udhalilishaji kama vitu vya kawaida visivyokua na madhara.
Alisema kuendelea kutendeka kwa matukio hayo ni kukosekana kwa utu na ubinadamu kwa watendaji na kwamba ipo haja zaidi sharia kali kuchukuliwa dhidi ya wafanyaji wanapotiwa hatiani.
Huku hayo yakijiri Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari wanawak TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa alisema jamii kubadilika na kuthamini utu wao pamoja na watoto wao.
Alieleza kuwa inasikitisha kuona licha ya uwepo wa jitihada mbali kuendelea kufanyika lakini baadhi ya watu wanapo mstari wa mbele kuhakikisha kesi za matendo hayo zinaodolewa kwenye vyombo vya sheria.
Akiendelea kufafanua zaidi alisema ni lazima jamii ibadilike na kufahamu kuwa kuna madhara makubwa ya matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto,hivyo wakiendelea kuyaachia yatabaki kuwaathiri siku hadi siku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.