Na.Mwandishi Wetu.
Asasi za Kiraia
zinazopambana na ukatili wa kinjisia kwa wanawake na watoto Zanzibar, zimetiwa
moyo na hatua zilizochukuliwa na Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuifungia Madrasa ya Ridhwaa Al Rasuul iliyopo Jangombe Jijini Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, baada
ya kutuhumiwa kuwafanyia udhalilishaji
wanafunzi wa Madrasa hiyo.
Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kupitia kwa Katibu wake Sheikh. Khalid Ali Mfaume pia imepiga marufuku walimu wa Madrasa hiyo
kusomesha katika madrasa nyengine yeyote ile.
Asasi za Kiraia
zimekuwa zikifuatilia kwa makini mwenendo wa makosa ya udhalilishaji nchini
ikiwemo kutoa elimu na kusaidia hatua za kisheria wahanga ambapo kwa muda mrefu
imegundua baadhi ya walimu wa madrasa kuhusika kwa namna moja ama
nyengine.
Asasi za Kiraia
zinaamini kuwa walimu wa madrasa ni watu wazuri sana na wenye maadili mazuri na
wanaoamrisha matendo mema kwa watoto na jamii kwa ujumla lakini bahati mbaya
kuna walimu ambao wanatumia vibaya nafasi zao, hivyo ni muhimu kuwafungia na
kuwapeleka katika vyombo husika ili kuendeleza mustakbali mwema wa taifa letu.
Hivyo, Asasi zinaomba Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kuendelea kuzipitia na kuzikagua Madrasa nyengine ambazo bado
zinaendelea kufanya vitendo vya udhalilishaji Unguja na Pemba.
Pia zinaiomba Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kuweka mikakati maalum kuhakikisha kuwa walimu hao hawaajiriwi katika
madrasa nyengine zozote na jamii pia inakuwa na uelewa wa walimu hao.
Zinaomba pia tuhuma
hizo zifikishwe katika vyombo husika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na
kukomesha vitendo hivyo ya udhalilishaji dhidi ya watoto wadogo ambavyo
huathiri mpangilio mzima wa maisha yao.
Zaidi ya watoto 20
wameripotiwa katika matukio mbali mbali kuwa walifanyiwa vitendo vya
udhalilishaji na walimu wa madrasa wa vyuo mbali mbali vya Unguja na Pemba
katika kipindi cha miaka miwili
Kwa mujibu wa taarifa
zilizotolewa katika kipindi maalum cha redio Jamii ya Micheweni Kisiwani Pemba
na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba hivi karibuni Bi Salama
Mbarouk Khatib ni kwamba katika shehia ya Chimba kisiwani Pemba watoto 15
wameharibiwa na walimu wa Madrasa mbali mbali ziliyopo katika Kisiwa hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Micheweni.Bi.Salma Mbarouk Khatib amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Walimu wa Madrasa ya Konde,Matangatuani,Viamboni,Kiwandani na Kijiji cha Chanjani Konde.
Kwa upande wa Unguja, Asasi za Kiraia zimerikodi matokeo zaidi ya matano ya udhalilishaji
ambayo walimu wa madrasa wamehusishwa katika maeneo tofauti ikiwemo eneo la
Kisauni, Magogoni na Kitope.
Hivi karibuni kesi
mbili za udhalilishaji zimetolewa hukumu zilizokuwa zikiwakabili walimu wa
madrasa. Mahakama ya Mkoa Vuga, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja imetoa adhabu kwa
Mwalimu Abdulkadir Rajab Miraji (19) aliyehukumiwa kwenda jela kwa kipindi cha
miezi sita.
Pia Mahakama ya Mkoa Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba, imemhukumu
Mwalimu wa Madrasa Abubakar Juma Kombo (18) kwenda jela miaka 12.
Asasi za Kiraia
zinaunga mkono jitihada za taasisi na watu binafsi waliohusika kufuatilia
udhalilishaji huu na kuomba taasisi nyengine kuchukua mfano wake.
Tamko
hili limetolewa na Chama cha wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuia ya
Wanawake Wenye Ulemavu (JUWAUZA), Mtandao wa Jinsia Zanzibar (ZGC), na Chama
cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania, (TAMWA, ZNZ.
Mkurugenzi
wa ZAFELA, Jamila Mahmoud
Mwenyekiti
wa JUWAUZA, Salma Saadat
Mwenyekiti
ZGC, Asha Aboud
Mkurugenzi
TAMWA, ZNZ, Dkt Mzuri Issa
No comments:
Post a Comment