Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia katika hafla ya Maadhimisho ya Miaka Mitano ya Kituo cha Wanawake cha Utengenezaji Vifaa vya Nishati ya Umeme wa Jua Kinyasini Wilaya ya Kaskazini"A" Unguja leo 8/8/2020.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Wizara ya Kazi, Uewezeshaji,
Wazee, wanawake na watoto ina jukumu la kukaa pamoja na Uongozi wa Kituo cha Wanawake
kinachotengeneza Vifaa vya Umeme wa Jua
“Barefoot Callege’ ili kuandaa mwelekeo wa kituo hicho baada ya
kukamilika kipindi cha miaka mitano tangu kIfunguliwe.
Dk. Shein amesema hayo leo huko
Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja katika sherehe za kutimiza miaka mitano
tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, hafla iliyokwenda sambamba na ufunguzi wa jengo
jipya la dakhalia kwa ajili ya wanafunzi
Alisema kwa kuzingatia sera na
maelekezo ya Serikali, Wizara hiyo
inapaswa kukaa pamoja na Uongozi wa kituo hicho na kuanza kufikiria mahitaji ya
baadae ya kituo, ikiwemo eneo la ardhi litakalotumika kwa ajili kuongeza
majengo na baadhi ya nyenzo muhimu zitakazohitajika.
Alisema kuwepo kwa changamoto mbali
mbali, ikiwemo uhaba wa madarasa na mabara ya kufundishia, ukosefu wa mahala pa
kusalia kwa ajili ya washiriki wengi wa mafunzo pamoja na ukosefu wa lami
katika eneo dogo la barabra inayoingia kituoni hapo ni mambo yanayohitaji
kutafutiwa ufumbuzi na Wizara hiyo.
“Nauagiza Uongozi wa Wizara uchukue
hatua ya kuzitatua changamoto hizo, zile ziliomo ndani ya uwezo wao moja kwa
moja na zile zinazohitaji mashirikiano na taasisi nyeingine wazishughulikie”,
alisema.
Alisema kuna umuhimu wa kukiendeleza
kituo hicho kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira ya Zanzibar na mabadiliko
ya dunia.
Aidha, Dk. Shein aliuagiza uongozi wa kituo
hicho kuunda jumuiya ya Wanafunzi wanaomaliza mafunzo kituoni hapo pamoja na
kutoa mialiko ya kufika kituoni ili kueleza namna walivyofaidika na mafunzo,
jinsi wanavyoitumia taaluma waliyoipata na mafanikio yao.
Alieleza kuwa kuna mafanikio makubwa
yaliopatikana na kituo hicho ndani ya kipindi cha miaka mitano na kuwashukuru wale
wote waliochangia katika kufanikisha uendeshaji mzuri wa kituo hicho.
Alisistiza umuhimu wa viongozi wa kituo
hicho kuwa na utaratibu mzuri wa kutunza na kuweka kumbu kumbu za historia ya
kituo hicho.
Alisema ni jambo la kujivunia kuona
kituo hicho kinapokea wanafunzi kutoka Tanzania Bara na nchi za jirani, na
kubainisha kuwa hilo ndio lengo la serikali tangu kituo hicho kilipoanzishwa.
“Hili lilikuwa ndio lengo la serikali tangu
mwanzo kituo hiki kiwe kwa ajili ya nchi za Afrika Mashariki na kati, sina
shaka washirki kutoka nchi mbali mbali watakuja miaka ijayo na kituo hiki kuwa
na hadhi ya Kimataifa”, alisema.
Alieleza ni vyema kituo kikawa na uatartibu
wa kutunza vyema takwimu na kumbukumbu za usajili wa wanafunzi wapya na taarifa
zao muhimu zinazohusiana na usajili huo ikiwemo mahali wanapotoka na kuzihifadhiwa
vizuri.
Aidha, Dk. Shein aliutaka Uongozi wa
kituo hicho kufuatilia kwa karibu maendeleo
ya wahitimu wote baada ya kumaliza
mafunzo yao pamoja na kuziwekea kumbukumbu taarifa zao.
“Mnahitajika kuwa na mawasiliano na
wanafunzi wanaomaliza mafunzo na kuwaalika katika hafla zenu muhimu, wanafunzi
hao ‘Alumn’ ni kiungo muhimu katika kukiendeleza na kukikuza kituo hiki kwa
kukitangaza na kukipa msukumo”, alisema.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza kwa
dhati Serikali ya India kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukiendeleza
kituo hicho na kusema ufunguzi wa jengo hilo ni uthibitisho wa ushirikiano
mwema wa nchi mbili hizo na dhamira ya kukifanya kituo hicho kuwa maarufu na chenye kupendwa katika ukanda wa Afrika
Mashariki.
Akigusia mipango na mikakati ya
serikali katika kutafuta vianzio mabadala vya umeme, badala ya kutegemea
kianzio kikuu kimoja, Dk. Shein alisema serikali imepata mafanikio makubwa
katika kuiendeleza miundombinu mikuu ya
umeme na usambazaji wake kupitia nishati ya jua,
Alisema Serikali na Jumuiya ya Umoja
wa Ulaya zimeshrikiana kufanya tafiti juu ya uwezekano wa kupata nishati hiyo, huku
matokeo yakionyesha kuwepo uwezekano mkubwa wa kupata kiwango kikubwa cha umeme
kupitia chanzo hicho.
“Benki ya Dunia imeonyesha nia ya
kutuunga mkono kwa kuanza na Megawati 35, ambapo zaidi ya wawekezaji 30
wamevutwa na mipango yetu na kuonyesha dhamira njema ya kushirikiana nasi”,
alisema.
Alieleza pale umeme wa uhakika
utakapopatikana kazi ya kusambaza umeme huo kwa wananchi itakuwa rahisi, kwa kuzingatia
miundombinu ya umeme ipo katika shehiya zote za Unguja na Pemba..
Vile vile, alisema kuna kila sababu ya
kukiendeleza kituo hicho Barefoot College kwa kuzingatia hali ya hewa iliopo
nchini inayotoa fursa nzuri ya kuendeleza umeme wa jua.
Aidha, Dk. Shein alibainisha juhudi
mbali mbali zinazochukuliwa na serikali katika kuwawezesha na kuimarisha ustawi
wa wanawake, kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na ule wa
Vijana unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana
na Uongozi wa Mfuko wa Khalifa Fund.
“Teknolojia hii ya umeme wa jua
inaendana vizuri na mazingira pamoja na Jiografia ya nchi yetu na ndio maana
utafiti uliofanyika umependekeza kwanza tuendeleze umeme wa jua kuliko vianzio
vyengine vya nishati ya umeme”, alisema.
Rais Dk.Shein aliwataka akinamama
kuongeza ari katika kujifunza teknolojia hiyo ili iweze kuwanufaisha wao pamoja
na watu mbali ,mbali wanaohitaji.
“Ni fahari kubwa kuona mama anaweza
kutatua tatizo la umeme nyumbani yeye mwenyewe bila kumsubiri baba au kutafuta
fundi kutoka nje”, alisema.
Dk. Shein alionyesha matumaini yake na
kusema pale akinamama hao watakapoongeza ari na kujituma, kutafuta utaalamu
zaidi na kubuni mbinu mbali mbali za kuendeleza ujuzi huo, kituo hicho kitaweza
kuwa kituo kikubwa na maarifu sana katika Ukanda wa Afrika Mashariki na
Ulimwenguni.
Katika hafla hiyo Dk. Shein alipata
fursa ya kutembelea na kuangalia kazi za ujasiriamali zinazoendeshwa na
washriki wa mafunzo ya kituo hicho pamoja na kupokea zawadi mbali mbali kwa
ajili yake na Mama Mwanamwema Shein.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein
alipongeza uongozi wa kituo hicho kwa kubuni nyanja mpya za mafunzo yahusuyo
ujasiriamali, ukiwemo ufugaji wa nyuki
na ufumaji , hatua aliyosema itakuza
uchumi wa familia na nchi kwa ujumla.
Aidha, alibainisha juhudi mbali
mbali zinazochukuliwa na Serikali za
kuwawezesha na kuimarisha ustawi wa wanawake, kupitia Mfuko wa Uwezeshaji
wananchi Kiuchumi pamoja na ule wa Vijana unaotekelezwa na Serikali kwa
mashirikianao na Uongozi wa Khalifa Fund.
Mapema, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji,
Wazee, Wanawake na watoto, Moudline Castico, alisema Wizara hiyo itaendelea na
juhudi za kukiendeleza kituo hicho ili kufanikisha dhamira ya kuanzishwa kwake.
Nae, Balozi Mdogo wa India nchini,
Bhagwant Singh alisema Serikali ya India itaendelea kuunga mkono juhudi za
kukiimarisha kituo hicho ili kuweza kupata mafanikio makubwa.
Alisema ana matumaini makubwa kuwa ushirikiano
uliopo kati ya India na na Zanzibar na Tanzania
kwa ujumla utaendelea kuimarika kwa maslahi ya watu wa nchi mbili hizo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kazi,
Uwezeshaji, Wazee, wanawake na watoto Fatma Gharib Bilali alisema jumla ya
akinamama 45 wameweza kunufaika na kutokana na mafunzo ya utengenezaji wa vifaa
vya umeme wa jua, ikiwemo 13 waliopata mafunzo hayo nchini India, ambapo sasa
ni wakufunzi wa kituo hicho.
Alisema jumla ya nyumba 958 kutoka
shehiya mbali mbali za Unguja na Pemba
tayari zimeunganishwa umeme wa jua kupitia washiriki wa mafunzo ya kituo
hicho.
Aidha, alisema kituo hicho kimekuwa
kikiendesha mafunzo ya ujasiriamali, ikiwemo ushoni wa nguo na ufugaji nyuki,
ambapo katika kipindi cha maradhi ya COVID 19 kiliweza kushona Barakoo 30,000
na kusambazwa katika maeneo mbali mbali ya nchi, ikiwemo Wizarani, Manispaa,
Wilaya za Mkoa Kusini Unguja na baadhi ya taasisi za Serikali.
Mkuu wa kituo cha Barefoot College,
Pendo alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliopatikana katika uendeshaji wa
kituo hcho, kuchelewa kupatikana vifaa vya umeme wa jua ni miongoni mwa
changamoto zinazokikabili kituo hicho.
Kituo cha Barefoot College,
kilizinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Ali Mohamed Shein mnamo Augosti 6, 2015.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment