Habari za Punde

MAJALIWA: TUJITAFAKARI TUNATAKA KIONGOZI WA AINA GANI

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi   nakala ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 mgombea ubunge wa CCM wa jimbo la Singida Kaskazini, Ramadhan Ighondo, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika kwenye viwanja vya Ilongero
Aliyekua Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Justine Monko, akimnadi mgombea mpya wa jimbo hilo, Ramadhan Ighondo, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika kwenye viwanja vya Ilongero, Septemba 15, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Singida watafakari ni aina gani ya kiongozi wanamtaka aiongoze nchi hii.

Ametoa wito huo leo (Jumanne, Septemba 15, 2020) wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano wa kuwanadi wagombea wa CCM uliofanyika kwenye viwanja vya CCM, kata ya Ilongero,  wilayani Singida.

"Uongozi wa nchi siyo jambo la mchezo, siyo jambo la kujaribiwa wala haliendi kwa upepo na ushabiki. Ni lazima mkae na kutafakari ni nani anafaa kuongoza nchi hii," amesema na kuongeza: “Tukae tuangalie tulipo na tunapotaka kwenda. Tujiulize je, ni nani anaweza kutupeleka huko?”

Amewataka wakazi hao wajihadhari na wagombea ambao wanatumia majukwaa kuanza kuwatukana wenzao. "Huu siyo wakati wa kutukanana bali ni wakati wa kuelezea sera na mambo gani atawafanyia."

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wakazi hao wamchague Dkt. John Pombe Magufuli ili aongoze tena kwa miaka mitano na aweze kumalizia kazi zilizopangwa na CCM kwenye Ilani yake.

"Nawaomba wana-Ilongero, wana-Singida Kaskazini na wana-Singida wote ikifika tarehe 28 Oktoba mchagueni Dkt. Magufuli. Sababu za kumuombea kura ni nyingi hasa kutokana na kazi kubwa aliyoifanya kwa nchi hii. Wote mmeona na kusikia yaliyofanyika kwenye maeneo yenu."

"Yeye ni mzuri wa kutabiri na kuyapangilia na kuyafuatilia. Yeye ni mzuri wa kutambua kero za wananchi wake na kuzitatua. Amejipambanua sana na kuwasihi wasaidizi wake wazingatie kuwatumikia Watanzania. Sote tumeona, maendeleo yaliyopatikana ndani ya miaka mitano hayajapata kutokea," amesema. 

Pia alitumia fursa hiyo kuwaombea kura, mbunge mteule wa jimbo la Singida Kaskazini, Bw. Ramadhani Ighondo na mgombea udiwani wa kata ya Ilongero, Bw. Issa Mwiru.
Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amempokea aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Singida, Bw. Frank Petro Akunay ambaye ameamua kuhamia CCM.

Bw. Akunay amehamia CCM akiambatana na mkewe, Betina Ibrahim pamoja na mdogo wake Bw. Daniel Petro Akunay. 

Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Akunay alisema ameamua kurudi nyumbani kwa sababu zamani alikuwa CCM lakini alipotea njia.

"Nimeamua kurudi nyumbani na nitachanja mbuga kuhakikisha CCM inashinda sababu mimi ni mtu wa field. Hapa Singida Kaskazini tuna vijiji 84, vitongoji 435 na kata 21. Ninavijua vyote. Nakuhakikishia tutashinda kwa asilimia 98 sababu sijarudi kwa bahati mbaya," alisisitiza.

"Tuna uhakika wa kupata ubunge kwani anayegombea hatusumbui kabisa. Kwa madiwani, tumebakiza kata 19 kwani wawili walishapita bila kupingwa."
   
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, SEPTEMBA 15, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.