Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Wajumbe wa Baraza la Biashara Zanzibar.


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia Jukwaa la Kumi na Moja (11) la Biashara Zanzibar katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kwa makusudi kushirikiana na sekta binafsi kwani sekta hiyo ndio injini ya uchumi wa nchi.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Jukwaa la 11 la Biashara lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar ambalo lilitanguliwa na Baraza la Taifa la Biashara lililofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa uchumi unakuwa kutokana na kuwepo kwa sekta binafsi na Serikali imeamua kwa makusudi katika kuhakikisha  hilo linafanikiwa na tayari mafanikio makubwa yameshaanza kupatikana.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa umoja uliojengwa na ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi ni lazima uimarishwe zaidi kwani faida kubwa itaendelea kupatikana.

Rais Dk. Shein ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Jukwa hilo alisema kuwa kukutana huko ni ahadi yake ya kukutana kwa lengo la kuagana baada ya kufanya kazi nzuri kwa kipindi cha karibu miaka 9.

Aliupongeza uongozi wa Wizara Biashara na Viwanda kwa kuiongza Wizara hiyo kwani imekuwa ikisimamia suala zima la biashara, ni kituo cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati tokea karne ya 16.

Rais Dk. Shein alieleza historia ya Zanzibar katika suala zima la biashara ambapo biashara zilitoka nchi za nje zikiwemo Uingereza, India, Hongkong na nchi neynginezo huku akisisitiza kuwa Zanzibar si mwanagenzi wa biashara.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa changamoto ya kibiashara hivyo, ni vyema biashara ikatangazwa kwani biashara itangazwayo ndio itokayo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa vikao vya Baraza hilo vilivyokuwa vikifanyika vilikuwa vikieleza suala zima la biashara na uchumi pamoja na uwekezaji.

Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa wajumbe wa Baraza la Taifa la Biashara, wafanyabiashara pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara ambapo chombo hicho kimeweza kuwa imara zaidi kuliko kilivyokuwa wakati alipoingia madarakani.

Alisema kuwa chombo hicho kimekuwa na mabadiliko makubwa na hivi sasa mashirikiano makubwa yampatikana kati ya Serikali na wafanyabiashara ambapo hivi sasa kumekuwa na mwelekeo mmoja katika kuendeleza biashara hapa nchini.

Alisisitiza haja ya kuzingatia nidhamu ya biashara na kueleza kuwa sekta ya umaa na sekta binafsi zote zilikuwa kitu kimoja hali ambayo imepelekea mafanikio na mazungumzo mazuri.

“Tulikuwa tukijadili kwa hoja na kila mmoja aliweza kutoa maoni yake hali ambayo ilisaidia kuimarisha biashara....na leo hakuna tofauti ya sekta ya biashara na sekta ya umma, sote watu wamoja ndivyo tulivyofanya miaka tisa iliyopita”alisema Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa lengo la juhudi hizo ni moja ambalo ni la kuinua uchumi na kueleza matarajio yake kuwa sekta ya biashara imebadilika ambapo taarifa za biashara za Benki ya dunia zinasema hivyo.

Aliongeza kuwa kwa kawaida biashara imekuwa ikitegemea sekta nyengine na ndio maana Serikali ikaanzisha Wizara ya Biashara na Viwanda na kusema kuwa serikali imekuwa ikihakikisha biashara ya vyakula inaimarika siku hsdi siku hapa nchini.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wafanyabiashara wa Zanzibar kwa kuingiza bidhaa kwa wingi nchini ambapo bidhaa zote zimekuwa zikipatikana kwa wingi hapa Zanzibar  na kupelekea hali ya chakula kuwa nzuri ”Miaka yote tulikuwa tukijadili na hatukuwa tukipiga stori na ndio maana tumepata mafanikio”, alisema Dk. Shein.

Katika hafla hiyo pia, Rais Dk. Shein pia, alizindua kitabu cha “Zanzibar Business enabling Environment 2020”.

Nae Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali alipongeza mafanikio yaliopatikana katika kuimarisha sekta ya Biashara chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein.

Alisema kuwa Serikali imeweka Jukwaa la Biashara ambalo limekuja na Kauli mbiu isemayo “Mazingira rafiki ya ufanyaji biashara kwa maendeleo ya Zanzibar” kauli mbiu ambayo imekuja baada ya kufanyika taratibu zilizowekwa na Serikali kutokana na mazingira ya Dunia.

Alisema kuwa Serikali imefanya tafiti za mwaka 2020 ambapo pia, hivi sasa Zanzibar imekuwa ya 101 katika eneo la urahisi wa biashara.

Alisema kuwa ndani ya miaka kumi mambo mengi yamefanywa ambapo katika eneo la baishara na viwanda mambo mengi ya msingi yamefanyika ila juhudi zaidi zitafanyika katika kuhakikisha Zanzibar inakuwa kituo cha biashara.

Alitoa pongezi kwa kuliendesha Baraza pamoja na Jukwaa lake kwa kupelekea kukuza uchumi sambamba na mashirikiano yaliopo kati ya sekta ya umaa na sekta binafsi.

Alisema kuwa Wizara anayoiongoza imefanya kazi kubwa katika kushirikiana na wafanyabiashara ambapo pia, uongozi wa Rais Dk. Shein umeweka mazingira bora ya wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na kutunga sheria kwa lengo la kuwawekea mazingira bora wafanyabiashara hapa nchini. 

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa madumuni makubwa ya kikao hicho ni cha kuagana na kutakiana kheir na kuwapongeza mahudhurio makubwa ya waalikwa wote. 

Nae Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar,Taufiq Turky alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kusimamia vyema uchumi wa nchi hasa katika kipindi cha janga la Corona ambapo licha ya bidhaa kupanda bei duniani lakini kwa upande wa Zanzibar haikuwa hivyo.

Alisema kuwa katika historia kiongozi msikivu, mwenye hekima, busara na kuweza kuwasiliza wananchi wake huku akisema kuwa Rais Dk. Shein amefanya mambo mengi na wafanyabiashara wataendelea kumkumbuka.

Kiongozi huyo alieleza kuwa tayari Jumuiya hiyo ya Wafanyabiashara wa Zanzibar imeweza kushirikiana na Jumuiya kadhaa za Kimataifa pamoja na kuweza kushirikiana na Jumuiya kadhaa kutoka nchi mbali mbali duniani zikiwemo Uturuki, China, Dubai, Qatar, Moroco na nyenginezo.

Alipongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali anayoiongoza Rais Dk. Shein kwa kupunguza utitiri wa kodi kwa wafanyabiashara na kueleza mafanikio yaliopatikana katika kuhakikisha kodi nyingi zinaondoshwa.

Kiongozi huyo wa Jumuiya ya Wafanyabiashara alipongeza juhudi za makusudi zilizochukuliwa  katika kuongeza watalii ambao ulivuka malengo mapema ya kufikia watalii laki tano mnamo mwaka 2020 ambapo hali hiyo ilifikiwa mapema mwaka 2019.

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara (ZNBC), Bakari  Haji Bakari aliwasilisha taarifa ya Mkutano wa Nne wa Baraza la Taifa la Biashara la Zanzibar alieleza tathmini ya mazingira ya biashara ya kila mwaka itakayochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuweza kujipima na Zanzibar kuweza kuingia katika nafasi 50 bora.

Rashid Ali Salim ambaye ni Katibu Mtendaji wa Baraza la kusimamia Mfumo wa utoaji  wa Leseni za Biashara (BLRC), alisema kuwa Serikali itatoa elimu zaidi na kuchapisha gharama za uungaji na bei ya umeme kwa jamii na wafanyabiashara na kuimarisha miundombinu ya umeme.

Nao wajumbe wa Jukwa hilo walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa mashirikiano yake kwa Wafanyabiashara pamoja na Jumuiya yao na kueleza mafanikio yaliopatikana katika uongozi wake hasa kwa kuiacha Zanzibar ikiwa ya amani na utulivu.

Alisema kuwa hakuna mfanyabishara yoyote aliyoonewa kwa kabila yake, dini ama jinsia yake katika uongozi wa Rais Dk. Shein huku wakimpongeza kwa kuanzisha Benki ya Kiislamu (Islamic Bank) kupitia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), kuanzisha sheria ambayo imeweza kuzipa nafasi Kampuni za ujenzi za wazawa chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.