Habari za Punde

Mgombea Urais wa Zanzibar Kwa Tiketi ya CCM Dk.Hussein Mwinyi Amesema Atahakikisha Kila Kiongozi Anawajibika na Wanaolega lega Watachukuliwa Hatua Juu Yao.

 

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa Chama Cha Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Hassan Mwinyi akiwahutubia Wananchi katika mkutano wake wa Kampeni  uliofanyika katika viwanja vya mpira Chwaka Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja leo na kuwaombea kura  na kuwaombea kura Wagombea wote wa CCM na kujiombea kura yeye mwenye wakati wa mkutano huo. 

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Mwinyi kwa upande wake alimpongeza Rais Dk. Shein kwa Utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa upande wa Zanzibar kwa zaidi ya asilimia 90.

Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Saba imefanya mengi ikiwemo ujenzi wa skuli za kisasa katika Wilaya hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa elimu ndio msingi wa maisha na kumpongeza Rais Dk. Shein kwa jitihada zake hizo.

Pia, alimpongza Rais Dk. Shein katika uongozi wake kwa kujengwa skuli za ghorofa 26 zenye zana zote za kujifunzia, madawari, na vifaa vyote muhimu.

Kwa upande wa sekta ya afya, alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuanza kwa  mradi wa hospitali ya Binguni na kuahidi kuwa Awamu ya Nane ijayo itaulamilisha mradi huo.

Alisema kuwa Hospitali ya Binguni atahakikisha ujenzi wake unakamilika na wananchi wanapata huduma zote za afya.

Kwa upande wa mradi maji km. 7.6 kutoka Bambi hadi Uroa mradi uliowaondoshea wananchi adha ya kupata maji  huku akieleza kuwa kwa upande wa na miundombinu, Dk. Hussein alisema kuwa kazi iliyofanywa ni kubwa na kila mtu anaona kwani nchi yote imefunguka kwa barabara za lami.

Kwa upande wa sekta ya kilimo, alisema kuwa kilimo cha mpunga ni kikubwa katika Wilaya hiyo, hivyo alisema kuwa kilimo cha umwagiliaji maji kimeimarishwa kutoka  hekta 110 hadi hekta 892 mradi ambao unaendelea na utekelezaji wake.

Alisema kuwa licha ya mafanikio hayo pia, zipo changamoto ambazo Awamu ya Nane itazitatua na kuziondoa kabisa ikiwemo migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi, maeneo ya kufanyia shughuli, pamoja na kuyatenga maeneo ya wafugaji na wakulima.

Aliongeza kuwa katika sekta ya ardhi, Awamu ya Nane itaangalia namna ya matumizi ya ardhi na kuahidi kuweka mipango mizuri ya ardhi.

Alisema kuwa baadhi ya matatizo yanasababishwa na wawekezaji na kusema kuwa Awamu ijayo inataka viongozi watakaowajibika kwa wananchi na kuhakikisha kila kiongozi anawajibika na wanao lega lega hatua zitachukuliwa juu yao.

Dk. Hussein alisema kuwa kunatakiwa kuwepo na maeneo maalum ya uvuvi, na utalii, kwani lengo ni kuhakikisha rasimali za nchi haziharibiki.

Akieleza kuhusu uvuvi haramu katika maeneo tengefu alisema kuwa doria zitaendelea kufanyika kwani tatizo kubwa ni ukosefu wa vyombo vya kisasa jambo ambalo litawezeshwa ili uvuvi uwe na tija.

Alieleza kuwa tatizo la ajira kwa vijana litapatiwa ufumbuzi kwani Serikali ijayo inataka kujenga uchumi mpya wa kisasa ambao utatatua tatizo la ajira kwa vijana ambao uchumi wnyewe utakuwa ni uchumi wa buluu.

Kwa upande wa ajira alisema kuwa tayari ajira laki tatu zimetengwa kwa hivyo hana wasiwasi na kusema kuwa uchumi unaokuja ni uchumi wa kisasa wa utalii wa kisasa, uvuvi mkubwa ukiwemo wa bahari kuu, ufugaji wa samaki na usindikaji wa samaki katika viwanda sambamba na bandari maalum za uvuvi.

Akieleza kuhusu ukosefu wa soko la matunda na mboga, Dk. Hussein alisema kuwa  wajasiriamali wa aina zote Serikali ijayo itahakikisha wanasaidiwa kupitia mfuko maalum wa uwezeshaji ambao utakuzwa ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ili wafanye kazi kwa weledi, zana, masoko na mazingira ya kazi.

Hivyo, aliwataka wajasiriamali wa aina zote kuondoa hofu kwani mambo mazuri yanakuja. “Yajayo yanafurahisha na ni neema tupu kwa Wazanzibari”,alisema Dk. Hussein.

Alisema kuwa kwa upande wa viwanda kadhaa vitajengwa kwa ajili ya kuwapatia wajasiriamali soko zuri pamoja na ajira.

Kwa upande wa miundombinu, alisema kuwa barabara zilizobaki zitamalizwa lakini kazi kubwa itafanywa katika kuzijenga barabara za ndani.

Alieleza kuwa kwa upande wa malisho ya mifugo kutakuwa na mipango mizuri ya ardhi hasa ikizingatiwa kuwa nia na dhamira ya serikali ya Awamu ya Nane ni kuhakikisha tija inapatikana.

Alisisitiza kuwa kwa upande wa soko atahakikisha Wilaya ya Kati inapata soko lake huku akieleza kuwa kwa upande wa changamoto ya Maji, Jumbi, Ungujaa, Charawe na Ukongoroni na kuahidi kuwa atahakikisha kwamba huduma hiyo inapatikana kwa wananchi wote kwani serikali ya awamu ya saba imefanya kazi.

Kwa upande wa kulinda misitu ambayo inakatwa alisema kuwa juhudi zitafanywa ili waweze kufanya kazi mbadala kwa kuwaoa mtaji, masoko na kuwapa kazi nyengine ili kuilinda misitu hiyo.

Sambamba na hayo, kwa upande wa uwezeshaji, Dk. Mwinyi alisema kuwa eneo hilo atalipa kipaumbele na kuwaondoa watu katika umasikini unaowakabili.

Kwa upande wa amani alisisitiza ni lazima kuilinda amani, na kusisitiza kuwa amani na utulivu iliyopo ni pamoja na kuwepo kwa Muungano uliopo na vikosi vya Muungano vimekwua vikifanya kazi kubwa ya kulinda Amani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.