Habari za Punde

Mgombea Urais wa Zanzibar Kwa Tiketi ya CCM Mhe Dkt. Hussein Mwinyi Anguruma Kisiwani Pemba na Kuomba Kura kwa Wananchi wa Pemba.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Mhe.Dkt. Hussein Mwinyi akihutubia katika mkutano wake wa kampeni katika viwanja vya Kiwani Wilaya ya Mkoani Pemba na kuomba kura kwa Wananchi wa Pemba na kuwaombea Kura wagombea wote wa CCM.

Na.Is-haka Omar -Pemba.

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ana uhakika wa ushindi katika uchaguzi mkuu wa octoba 28,mwaka huu na   hivyo anajiandaa kushona suti mpya kwa ajili ya kuapishwa

Dk,husseibn, alisema hayo katiksa mkutano wa mwisho wa kampeni za CCM kwenye mkutano uliofanyika uwanja wa mpira jimbo la kiwani Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba.

Dk.Hussein , alijenga hoja ya ushindi katika uchaguzi huo kutokana na kuungwa mkono makundi mbalimbali yakiwemo ya vijana, akina mama,wavuvi,wazee ,wafanyabiashara,wakulima na wana CCM kwa ujumla.

Alisema kukubalika kwake kunatokana na kampeni zake za kisayansi anazozifanya,ahadi zinazotekelezeka na Ilani bora ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ukilinganisha na vyama vingine.

“Ushindi wa chama cha mapinduzi hauna shaka na sasa najiandaa kushona suti mpya kwa ajili ya kuapishwa maana chama hiki kinaungwa mkono na makundi mbalimbali ya wananchi”, alisema Dk.Hussein.

Akizungumza kuhusu ahadi zake amesema iwapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kushika nafasi hiyo, ataimarisha huduma za afya, ili wananchi wapate uhakika wa matibabu.

 Alisema, hayo ndio kipaumbele chake cha kwanza mara atapomaliza kuapishwa, kwani mambo hayo ni miongoni mwa mambo muhimu kwa wananchi.

Alisema moja ya dhamira yake ya kugombea nafasi hiyo, ni kuwatumikia wananchi kwa moyo wa dhati, na ndio maana anakusudia kuimrisha huduma za afya.

Alisema atakchokifanya ni kuendeleza pale alipoishia rais wa sasa wa awamu ya saba, Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, ambapo anatarajia kuimarisha miundombinu ya afya.

Dk. Mwinyi aliahidi kuwa katika kuimarisha huduma hizo, atajenga nyumba za kisasa za madaktari, ili wapate mahala pazuri na salama pakufanyia kazi zao.

‘’Kama madaktari wetu wakipata nyumba za kisasa za mkaazi inakuwa rahisi sasa kutoa huduma za afya kwa ubora na hilo nalikusudia kulifanya nikiwa rais,’’aliahidi.

Aidha mgombea huyo wa urais aliahidi kuwa, dawa zitapatikana kwa uhakika sambamba na kuajiri kwa wingi madaktari bingwa ili watoe huduma za tiba kwa ufanisi.

Jengine alilowahidi wananchi wa Zanzibar kuwa iwapo atapata ridhaa ni kuimarisha sekta ya elimu, kwa kuwepo maabara za masomo ya sayansi na vifaa vyake.

‘’Elimu ndio msingi wa kila jambo, hivyo kama nikipata ridhaa nitahakikisha hakuna usumbufu wa upatikanaji wa vifaa vya masomo kwa madarasa yote,’’alieleza.

Hata hivyo Dk. Mwinyi ameahidi ujenzi wa nyumba za waalimu sambamba na kuwaendeleza kielimu, mafunzo kwa waalimu ili wawe na ufanisi wa kazi zao.

Katika hatua nyingine Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, amesema anakusudia kuinuwa uchumi wa wazanzibari, kwa kuanzisha viwanda mbali mbali vikiwemo vya kusarifia mwani.

Alisema, pamoja na viwanda hiyo mwani huo utaongezwa thamani kwa kuyashawishi makampuni mengi zaidi, ili kununua mwani wa wakulima wa Zanzibar.

“Kilio cha wakulima wa mwani na wavuvi nimeshaskia wakati nakutana na makundi mbali mbali kwenye kampeni zangu, sasa nikichaguliwa kuwa rais, ntahakikisha naimarisha sekta hiyo,’’alihidi.

Katika eneo jingine Dk. Mwinyi alisema mafanikio ya Zanzibar yanategemea sana utendaji kazi wa kila mmoja, hivyo suala la uwajibikaji ni jambo la lazima.

Alisema kuwa, serikali atakayoiongoza hatopenda hata kidogo kuona ndani yake, mna watendaji wasiopenda kuwajibika, kwani wanakuwa kikwazo kufikia maendeleo yaliokusudiwa.

Alisema, jambo hilo ni adui mkubwa wakufikia maendeleo ya  Zanzibar, na kuendelea kudumaa kwa baadhi ya sekta, jambo ambalo halikubaliki na atalisimamia kwa dhati.

“Mkinichagua kuwa rais wa Zanzibar, pamoja na mambo kadhaa ambayo ntawafanyia, lakini suala la uwajibikaji ndio kipaumbele cha kwanza, na akitokezea mtendaji kushindwa kuwajibika, ntamuwajibisha,’’alieleza.

Mapema rais wa Zanzibar wa na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema CCM imewaletea kiongozi mchapakazi kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema sifa za Dk. Mwinyi za nidhamu, uhodari wa kazi, kuwajali watu wote na ubobevu wa uongozi, hanazo mgombea mwengine yeyote kwa nafasi yoyote kutoka vyama upinzani.

Alieleza kuwa, Dk. Miwnyi amekuwa anajali sana shida za watu na kupelekea kushika nafasi mbali mbali, kuanzia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‘’Kazi iliyofanywa na mikutano yote ya CCM na kisha kupatikana kwa mgombea huyo Dk. Hussien Miwnyi haikukosea, maana uchapakazi wake unaonekana na kila anapokabidhiwa madaraka,’’alieleza.

Hata hivyo rais huyo wa Zanzibar, alisema kutokana na kuelewa vyema majukumu ya urais kutokana na ugumu wake, na jinsi anavyomfahamu Dk. Mwinyi, basi anauweza bila ya wasi wasi.

Alieleza kuwa, Dk. Mwinyi ndio mgombea pekee ambae anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais wa Zanzibar, hasa kwa busara zake na utii wa kazi.

‘’Dk. Mwinyi anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais, maana mimi nauwelewa sana na sijaona kiongozi mwengine anaeuweza baada ya mgombea aliyetuliwa na CCM,’’alifafanua.

Hivyo, amewataka wananchi wa Zanzibar kuhakikisha wanawapigia kura viongozi wa majimbo na wadi pamoja na mgombea huyo, ili aendelea kuwatumikia wananchi.

Alifahamisha kuwa, dhamira ya CCM kila siku ni kuona wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu, hivyo ili hilo litekelezeke ni kuwapigia kura wagombea wa CCM.

“Siku ya tarehe 28, Oktoba mwaka huu, siku hiyo ya kupiga kura ikifika, muhakikishe hamfanyi makosa, na muwapigie kura rais John Pombe Magufuli, Dk. Hussein Mwinyi, wabunge, wawakilishi na madiwani wetu wote,’’alieleza.

Pamoja na hayo amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa ulinzi utaimarishwa na hivyo kila mwananchi mwenye sifa atapata haki yake ya kupiga kura .

Alisema vitendo vya kuwashambuliwa kwa wana CCM kisiwani Pemba visiwape woga wengine kwani serikali iko imara haiyumbishwi na makundi machache ya kihalifu.

Naibu Katibu mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, alisema, ushindi wa CCM hauna shaka, kutokana na kuitekeleza vyema ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

‘’Leo kutoka mjini Wete hadi kijiji cha Gando, unatumia dakika zisizozidi 20, maana barabara imejengwa tena kwa kiwango cha lami, hayo ndio mambo ya CCM,’’alisema.

Wakati huo huo wagombea ubunge, uwakilishi wa Jimbo la Kiwani pamoja na madiwani, wamewaomba wananchi hao kuwapigia kura ili kuimarisha maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.