Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Amewatembelea Wahanga wa Tukio la Kupigwa Wilaya ya Micheweni Pemba, Waliolazwa Hospitali ya Micheweni.o ya Kupigwa [

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiangalia picha ya X-ray  ya mmoja wa Majeruhi wa Wahanga wa Matukio ya Kupigwa yaliotokea katika eneo Kwale Wilaya ya Micheweni Ndg.Khatib Said Khatib, wakati akipata maelezo kutoka kwa Daktari Dhamana wa Hospitali ya Micheweni Dr. Mbwana Shoka Salim, alipofika leo kuwatembelea na kuwapa pole na kuwafariji 
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amefika hospitali ya Micheweni kwa ajili ya kuwapa pole wanachama wa CCM waliovamiwa na kupigwa huko katika kijiji cha Kwale, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Rais Dk. Shein alifika Hospitalini hapo mnamo majira ya saa tano za asubuhi na kupokewa na viongozi mbali mbali wa Mkoa na Wilaya hiyo pamoja na madaktari wa Hospitali hiyo ya Micheweni wakiongozwa na Daktari dhamana wa hospitali hiyo Dk. Mbwana Shoka Salum.

Akitoa maelezo ya wahanga hao, Daktari huyo dhamana alisema kuwa wagonjwa hao walipokewa mnamao majira ya saa moja za usiku wakiwa na majeraha makubwa na mmoja kati ya hao Khatib Said Khatib (43) alikuwa katika hali mbaya.

Kwa mujibu wa uongozi wa Jeshi la Polisi viongozi wa Mkoa na Wilaya walieleza kuwa  tukio hilo limetokea wakati wafuasi wa chama kimoja cha upinzani cha siasa  walipokuwa wakirudi katika mkutano wao wa kampeni huko Chamboni, Wilaya ya Micheweni, na kupita katika kijiji cha Kwale na ndipo walipowashambulia kwa kuwapiga wanachama hao wa CCM.

Miongoni mwa wahanga hao ni Khamis Hamad Haji umri wa miaka (70), Yassir Hemed Abdi (18), Hassan Khamis Hamad(33), Juma khatib Rajab(34), Abdalla Khamis Mbarouk (30), Khatib Said Khatib (43) na Raya Khamis Hamad (24).

Kwa mujibu wa maelezo ya Daktari dhamana wa Hospitali hiyo Dk. Mbwana Shoka Salum alisema kuwa mhanga Khatib Said Khatib (43) ndiye aliyekuwa hali mbaya wakati alipofika hospitalini hapo kutokana na majeraha ya kupigwa kisu cha tumbo na mbavu.

Aliongeza kuwa wahanga wengine nao walipata majeraha yakiwemo kupigwa na vitu vyenye ncha kali sehemu ya vichwa, tumbo na miguu huku Raya Khamis Hamad(24) ambaye ni mjamzito mtoto wa Khatib Said Khatib(43) alipigwa mateke ya tumbo wakati akimuombea baba yake.

Rais Dk. Shein akiwapa pole waathirika hao aliwaeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko pamoja na wao na itahakikisha inawakamata wahusika wote na baadae kuwachukulia hatua husika za kisheria.

Akitoa pole hiyo, Rais Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali ya Mapainduzi ya Zanzibar itahakikisa anaendelea kuzilinda familia zao, makaazi yao na vipando vyao pamoja na mali zao zote.

Daktari dhamana huyo alitoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuiimarisha Hospitali hiyo na kueleza kwua wananchi wa Micheweni na vitongoji vyake wanaridhika na huduma zinazotolewa na hospitali hiyo zikiwemo huduma za upasuaji.

Dk. Dhamana huyo alipongeza mashirikiano makubwa yaliyooneshwa na viongozi wa Mkoa, Wilaya na wengineo katika kuwasaida wananchi hao waliopigwa katika muda wote wakiwa hospitalini hapo.

Nae Kamishna wa Polisi Zanzibar Mohammed Hassan Haji alimueleza Rais Dk. Shein kuwa tayari watuhumiwa 57 wa tukio hilo wameshakamatwa na bado Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka zaidi wahusika wengine.

Raya Khamis Hamad akimueleza Rais Dk. Shein maswahiba yaliyomkuta na kupelekea kupigwa mateke ya tumbo, alisema kuwa ipo haja kwa vyama vya siasa kuheshimiana kwani si jambo la busara kufanyiana matukio kama hayo hasa ikizingatiwa kwamba wao wanachama chao cha CCM na hawamchokozi mtu lakini wao wanachokozwa.

Nae Khatib Said Khatib alimueleza Rais Dk. Shein kuwa imekuwa jambo la kawaida kwa wafuasi wa chama hicho cha upinzani wanapokwenda ama kurudi mikutanoni mwao kufanya vitendo visivyofaa wakati wakipita katika kijiji chao.

Alisisitiza kwamba ipo haja kuzidishiwa ulinzi katika eneo lao kwani mbali ya kipigo alichokipata yeye na wenziwe pia, mazao yake yote yamekatwa huko shambani kwake.

Aliongeza kuwa ni kawaida kwa wafuasi hao wa chama hicho cha upinzani wanapokwenda katika mikutano yao huchukua silaha za jadi ndani ya gari zao.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.