Na. Jaala Makame Haji- ZEC
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
(ZEC), itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na wadau wa Uchaguzi ili
kuhakikisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 27 na 28 Octoba mwaka huu unafanyika
kwa salama na Amani.
Kauli hiyo ilitolewa na
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid wakati akizungumza
na Viongozi wa Dini mbali mbali kisiwani Pemba katika Ukumbi wa kiwanda cha
mafuta ya Makonyo Wawi Pemba
Mwenye Hamid Mahmoud alisema,
tokea kuanza kwa zoezi la matayarisho ya
hatua mbali mbali za Uchaguzi ZEC, imekuwa karibu na wadau wake kwa
kufanya mikutano mbali mbali inayohusiana na suala hilo ikiwa na dhamira hiyo
ya kuwepo amani na utulivu .
Aliwataka viongozi wa
dini waendelee katika kuhamasisha kampeni na hatua nyengine za uchaguzi kwa
utulivu na amani ili nchi iendelee kutajika kuwa visiwa vya amani.
Alifahamisha kuwa, katika
kuzingatia nafasi ya viongozi hao katika jamii iliyowazunguuka Tume imeona kuwa
wao ni wadau muhimu wa Uchaguzi na inatambua umuhimu wao kwa vile wanaongoza
kundi kubwa katika jamii.
Jaji Mahamoud,
aliwaomba Viongozi hao kuendelea kuhubiri amani kwa wananchi wote wakati, kabla na baada ya Uchaguzi pia kuendelea
kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii ili iweze kushiriki kikamilifu katika
masuala ya Uchaguzi.
Mwenyekiti huyo
alifahamisha kuwa, utunzaji wa amani ni wajibu wa kila mwananchi katika Taifa
hili, hivyo kila mmoja wetu atumie muda wake kuitunza amani iliopo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Uchaguzi (ZEC) Thabit Idarous Faina, akiwasilisha mada juu ya matayarisho ya
Uchaguzi Mkuu 2020, alieleza kwamba Tume hiyo tayari imeshafanya mambo mengi na
kuchukuwa hatuwa mbali mbali juu ya mchakato wa uchaguzi ambazo zitawezesha
kukamilisha uchaguzi huo kwa mafanikio makubwa.
Alifahamisha kuwa,
miongoni mwa mambo hayo ambayo tayari yamekamilika ni uandikishaji wa wapiga
Kura Wapya na uhakiki wa taarifa za wapiga kura ambapo jumla ya wapiga kura
566,352 waliandikishwa na wanatarajiwa kuwa Wapiga Kura katika uchaguzi mkuu wa 2020.
Aliendelea kueleza
kuwa, Tume ya Uchaguzi imefanya uteuzi wa Wagombea 17 wa ngazi ya Uraisi wa
Zanzibar, Wagombea 252 Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa majimbo mbali mbali
ya Uchaguzi na Wagombea wa Udiwani 360 kwa Wadi zote.
Aidha, akizungumzia
kuhusu Waangalizi wa Uchaguzi Mkurugenzi Faina alifafanua kuwa, Tume imeruhusu
kuwepo kwa waangalizi wa Uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu 2020 na jumla ya taasisi
61 za ndani ziliomba kupatiwa vibali na zilizokidhi vigezo ni 35.
Alifahamisha kuwa jumla
ya taasisi 15 za kimataifa ambazo zimepatiwa vibali na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi NEC zimeomba pia kupatiwa kibali kuangalia Uchaguz wa Zanzibar.
Sambamba na hayo, pia
Mkurugenzi alibainisha kuwa kwa mara ya Kwanza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imetumia bajeti yote ya Uchaguzi kwa ukamilifu bila hata kutumia pesa za
wafadhili.
Alisema Tume ili
kuhakikisha inaendesha uchaguzi huo bila ya kuwepo malalamiko , ilipitia upya
matakwa ya sheria mpya ya Uchaguzi , maelekezo ya miongozo juu ya majukumu kwa
Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na vituo pamoja na majukumu yao.
Hata hivyo wadau wa
Uchaguzi wanalojukumu la kuhakikisha uchaguzi na harakati zake unakamilika kwa
amani na Tume itakuwa karibu kufanya kazi nao kwa mashirikiano makubwa ili kukamilisha kazi ya uendeshaji wa
uchaguzi kwa salama na amani.
No comments:
Post a Comment