Habari za Punde

Wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili ya Rais Wamuaga Balozi Seif Ali Iddi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar BalozizanzSeif Ali Iddi Kulia akipokea Picha ya kuchora yenye sura yake kutoka kwa Katibu wake Nd. Mohamed Ali Abdulla {Muha} ili iwe kumbukumbu atakayoikumbuka katika uhai wake.
Katibu wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Mohamed Ali Abdulla { Muha} Kati kati na Msaidizi wake Bibi Sahrifa Abeid wakimkabidhi Balozi Seif zawadi ya kasha kama Kumbukumbu yake baada ya kufanya kazi nao pamoja.
Naibu Katibu wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Bibi Sharifa Abeid Salum akimkabidhi zawadi Bosi wake hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake Kisiwani Pemba hapo katika Ukumbi wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais Pagali Chake chake Pemba katika kikao cha kuwaaga.
Baadhi ya Wakuu wa Vitengo katika Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakiwa makini kusikiliza anasaha za Kiongozi wao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mara baada ya kuikamilika kwa hafla ya kuagwa rasmi.

Na.Othman Khamis.  OMPR. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mfanyakazi wa Taasisi ya Umma na hata ile Binafsi katika  ngazi yoyote anapaswa kuzingatia dhima ya kutekeleza wajibu wake katika kuutumikia Umma ili pale atakapoondoka aache athari itakayoendelea kuleta tija na kukumbukwa muda wote.

Alisema zipo sifa za baadhi ya Watumishi wa Umma katika sehemu za Kazi ambazo hubakia kuwa kielelezo cha Utumishi uliotukuka na wakati mwengine husaidia hata jamii yake pale inapohitaji huduma katika sehemu hizo au fursa za ajira jambo ambalo humjengea Historia ya kudumu katika nyoyo za Jamii.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake kwa upande wa Pemba huko Pagali Chake chake Pemba na Wasaidizi wake wa Idara ya Faragha kwa upande wa Unguja hapo Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni akiwaaga baada ya kufanyakazi nao pamoja katika kipindi cha Utumishi wake wa Miaka Kumi akiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Alisema jamii imekuwa ikishuhudia vituko vya baadhi ya Watumishi wa Umma katika ngazi tofauti wanaolalamikiwa kutokana na tabia yao mbaya katika kuwahudumia Wananchi na matokeo yake Watu hushangiria na wengine kudiriki hata kupita chakula kitamu kujipongeza kutokana na kuondoka kwake katika jukumu husika.

Balozi Seif aliwakumbusha Watendaji hao licha ya mabadiliko ya Uongozi wa juu yanayofanyika kutokana na Sheria, kujiepusha na tabia ya majungu, dhana mbaya, fitina na hata kusengenyana mambo yanayochangia kuzorotesha uwajibikaji wao unaohitajiwa na Wananchi wakati wote.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wote wa Idara ya Faragha kutokana na mchango mkubwa waliompa uliomuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa jambo ambalo hana haja ya kulalamika kutokana na mafanikio hayo.

Balozi Seif alisema wakati tayari ameshaamua kustaafu baada ya kutoa mchango wake mkubwa ndani ya Serikali zote mbili na Chama cha Mapinduzi tokea Mwaka 1965 aliwaomba Watendaji hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kiongozi mwengine mpya atakayewasimamia ili ile kiu ya Wananchi iweze kufikiwa vyema.

“ Nimeamua kustaafu baada ya kutoa mchango mkubwa wa Serikali na CCM kwa muda mrefu tokea Mwaka 1965 nilipoanza na Kazi ya Ualimu, baadae Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, nafasi ya Diplomasia na hatimae siasa. Kiongozi mzuri Mtu asisubiri kufukuzwa”. Alisisitiza Balozi Seif.

Katika Risala yao Watendaji  na Wasaidizi hao wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Pemba na Unguja walisema mambo mengi ya mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha Miaka Kumi ni msingi mzuri wa  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Walisema kipindi chake hicho cha Awamu mbili za Miaka Mitano mitano kimemuwezesha  kusimamia mambo mengi yaliyoleta Tija na hatimae Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar zikatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Watendaji na Wasaidizi hao wa Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Serikali wameahidi kuendelea kufanya Kazi kwa uadilifu na ufanisi mkubwa huku wakiridhika kumuona Kiongozi wao mpendwa Balozi Seif Ali Iddi anastaafu akiwa na Afya yake kamili.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed amewaomba Watendaji na Wasaidizi hao kuendelea kupendana na hiyo ndio sifa ya ufanisi mzuri wa majukumu ya Watumishi katika kutumikia Umma.

Waziri Aboud alisema yapo mapungufu mdogo yanayomkumba Mtumishi wakatui wa utekelezaji wa majukumu yake  lakini kinachozingatiwa na kutiwa maanani ni suala la uvumilivu likiwa chachu ya kupata Maendeleo ya haraka.

Alibainisha kwamba kusameheyana ndani ya uwajibikaji baina ya Watendaji  katika sehemu za Kazi ni sifa na falsafa inayofuta chuki, kero na maonevu mambo yanayonyoosha Ustawi wa Jamii.

Katika hafla hizo za kuagana Watendaji na Wasaidizi hao wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar walimkabidhi Balozi Seif Ali Iddi zawadi mbali mbali kama ukumbusho wa kufanya kazi nae pamoja kwa muda mrefu.

Zawadi hizo ni pamoja  Makasha, Picha, Milango, vyakula na hata vitu vya mapambo ya ndani kwa Wake zake wote Wawili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.