RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa muda wa miezi mitatu kwa uongozi wa
Wizara ya Afya kurekebisha kasoro za kiutendaji zinazosababisha kutokuwepo ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa
wagonjwa.
Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja, alipofika kuangalia utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika maeneo na vitengo tofauti vya Hospitali hiyo.
Alisema kwa kiwango kikubwa mambo mengi yanahitaji kufanyiwa marekebisho, akibainisha kuwepo changamoto mbali mbali za kiutendaji na hivyo kuzorotesha uapatikanaji wa huduma bora kwa wagonjwa.
Alisema analenga kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watendaji wasiowajibika kazini na kusababisha wananchi kulalamika kutokana na ukosefu wa huduma, pamoja na kupewa lugha zisizordhisha kutoka kwa wauguzi na watendaji wengine wa Hospitali hiyo.
Aidha, Dk. Mwinyi alisema pamoja na Serikali kuipatia fedha za kutosha Hospitali hiyo kila mwezi, kumekuwepo changamoto za ukosefu wa vifaa muhimu kwa wagonjwa ikiwemo magodoro, dawa na vifaa vya maabara, hivyo akautaka Uongozi wa Hospitali hiyo kubadilika na kuondokana na utendaji wa mazowea.
Alisema pale Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na hatimae wagonjwa wakakosa dawa hizo, ni dhahiri kuwa kuna tatizo mahala hapo.
Alieleza kuwa kumekuwepo matatizo madogo madogo katika uendeshaji wa Hospitali hiyo na kubainisha kuwa; kama yangelishuhulikiwa ipasavyo , ni wazi kuwa huduma bora zingepatikana.
Aidha Rais Dk. Mwinyi , aliahidi kufanya ziara nyingine katika siku zijazo na kuzungumza na wafanyakazi kwa lengo la kuimarisha utendaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alisema wafanyakazi wana wajibu wa kuwatumikia wagonjwa kikamilifu sambamba na kupata haki wanazostahili.
Aliwataka madaktari na wauguzi kuvaa vitambulisho ili kuondokana na urasimu kwa wagonjwa ambao hatimae huzaa rushwa.
Katika ziara hiyo Dk. Mwinyi alipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali ya Hospitali, ikiwemo OPD , MRI, Jengo la kuhifadhia Dawa, Kitengo cha Macho pamoja na kusikiliza changamoto mbali mbali zinazokwamisha na kuzorotesha utendaji kazi, sambamba na kuwajuilia hali wagonjwa, ikiwemo wale waliopata ajali.
Mapema, Mkurugenzi Uuguzi wa Hospitali ya rufaa ya Mnazi mmoja Dk. Haji Nyonje alisema Uongozi wa Hospitali hiyo ulilazimika kujenga Bohari mpya ya kuhifadhia dawa kutokana na ongezeko la upatikanaji wa Dawa hospitalini hapo.
Alisema changamoto kubwa llinaloikabili hospitali hiyo hivi sasa ni kuwa mashine za kufulia ambazo baadhi ya nyakati hushindwa kufanya kazi.
Dk. Nyonje aliahidi kuyafanyia kazi malalamiko ya wagonjwa wanaolazwa na kulazimika kwenda na mashuka yao wenyewe, mbali na Uongozi wa Hospitali hiyoo kununua mashuka ya kutosha katika kipindi cha hivi karibuni.
Nae, Daktari Mkuu Kitengo cha Macho, Dk. Slim Mgeni alisema pamoja na juhudi za Serikali kuimarisha upatikanaji wa vifaa, bado kunahitaji vifaa zaidi hususan katika suala zima la kufanyia Operesheni.
Alisema katika kitengo hicho kuna changamoto ya upungufu wa vitanda vya kulazia wagonjwa na hivyo kulazimika baadhi ya wagonjwa waliopata nafuu kuwapa ruhusa ya kwenda nyumbani baada ya kufanyiwa Operesheni.
Aidha, alisema kuna changamoto ya dawa , sambamba na ‘theatre’ mpya iliojengwa kutokukamilika, mbali na Mkandarasi aliepewa zabuni kukamilishiwa fedha zote za ujenzi.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment