Habari za Punde

Kidimni wapongeza uongozi wa Jimbo kuanza kuwatatulia kero zinazowakabili

Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Haji Shaaban Waziri akitoa maelezo kwa waandishi wa habari wakati wa kutandaza kifusi katika barabara za ndani katika kijiji cha Kidimni Jimbo la Uzini. 

Mbunge wa Jimbo la Uzini Khamis Hamza Chilo (alieshika pauro) akishiriki katika utandazaji wa fusi kwa barabara za ndani huko Kidimni Jimbo la Uzini.

Picha na Bahati Habibu.


Bahati Habibu, Maelezo Zanzibar


WANANCHI wa kijiji cha Kidimni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini, wameupongeza uongozi wa jimbo la Uzini kwa kuanza kuwatatulia kero zinazowakabili muda mfupi baada ya kuapishwa.

Wakishiriki katika kazi ya kutandaza kifusi kwenye barabara za ndani za kijiji hicho, wamesema hatua hiyo inawapa imani ya kuondokana na usumbufu wanaoupata wakati wa kutumia njia hizo.

Mbunge wa jimbo hilo Khamis Hamza Khamis (Chilo), amewataka wananchi kutokuharibu miundombinu kwani serikali inatumia gharama kubwa kuitengeneza kwa lengo la kuwarahisishia shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Alisema hatua ya kutengeneza barabara hizo, ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo, ambayo imelenga kuwaondoshea wananchi kero zote zilizomo kwenye maeneo yao na kuwaletea  maendeleo.

Nae Mwakilishi wa jimbo la Uzini Haji Shaaban Wazir, alieleza kufurahishwa na ushirikiano uliopo baina ya viongozi wa jimbo na wananchi, na kuongeza kuwa hiyo ni njia itakayosaidia kutatua matatizo kwa haraka.

Alifahamisha kuwa, ndani ya mwezi mmoja, wamekusudia kuhakikisha barabara zote za ndani ambazo zina mashimo, zinatandazwa kifusi ili wananchi waweze kuendelea na shuguli zao za kila siku bila usumbufu.

Kwa upande wao, Madiwani wa Wadi tatu zilizomo jimboni humo, wamesema jimbo lao ni mfano wa kuigwa kwa namna wanavyofanya kazi kwa ushirikiano kati ya Mbunge, Mwakilishi na wananchi.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.