Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi akutana na Ujumbe wa Jumuiya ya Maimamu (JUMAZA) Ikulu leo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk.Hussei Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Jumuiya ya Maimamu (JUMAZA) waliofika Ikulu Jijini Zanzibar leo kwa ajili ya kumpongeza kutokana na ushindi alioupata katika uchaguzi Mkuu uliopita Mwaka 2020.[Picha na Ikulu] 28/12/2020.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk.Hussei Ali Mwinyi (katikati) akiwasikiliza Uongozi wa Jumuiya ya  Jumuiya ya Maimamu (JUMAZA) wakati wa mazungumzo yao  Ikulu Jijini Zanzibar leo waliofika  kumpongeza kutokana na ushindi alioupata katika uchaguzi Mkuu uliopita Mwaka 2020.[Picha na Ikulu] 28/12/2020.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk.Hussei Ali Mwinyi (katikati) akisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Ujumbe wa Jumuiya ya Maimamu (JUMAZA) waliofika Ikulu Jijini Zanzibar leo   kumpongeza kutokana na ushindi alioupata katika uchaguzi Mkuu uliopita Mwaka 2020.[Picha na Ikulu] 28/12/2020.

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

 Zanzibar                                                          28.12.2020

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali anayoiongoza itahakikisha inashirikiana vyema na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) katika kujenga misingi ya dini ya Kiislamu hapa nchini.

 

Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Wajumbe wa Jumuiya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) wakiongozwa na Kaimu Katibu Sheikh Ali Abdalla  Amour.

 

Wajumbe wengine kutoka (JUMAZA) waliofika Ikulu kuzungumza na Rais ni Dk. Moh’d Hafidh Khalfan, Sheikh Masoud Hemed Nassor, Sheikh Yussuf Khamis, Sheikh Abdalla  Issa Makame, Sheikh Muhiddin Zubeir Muhiddin na Ukhti Halima Qasim Moh’d.

 

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Hussein mwinyi alisema kuwa miongoni mwa mambo makubwa ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele katika kujenga misingi ya dini ya Kiislamu ni umoja, amani na mshikamano.

 

Hivyo, alieleza kuwa kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa hapa Zanzibar kumetoa nafasi nzuri ya kuimarisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa viongozi, wananchi pamoja na kuamsha ari ya kushirikiana.

 

Alisema kuwa hatua hiyo, imesaidia kuweka pembeni kasoro zilizokuwepo hapo siku za nyuma hali ambayo itapelekea kupata maendeleo makubwa hivyo, ni jukumu la viongozi wa siasa, viongozi dini pamoja na wananchi kuhakikisha hilo linafanikiwa.

 

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza juhudi za makusudi zinazokusudiwa kufanywa na Serikali katika kupambana na udhalilishaji wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuwaita wadau na kukaa nao pamoja na kujadili hatua za kuchukuliwa katika kupiga vita janga hilo wakiwemo viongozi hao wa dini ambao wako katika jamii.

 

Rais Dk. Mwinyi alieleza jukumu kubwa la viongozi wa dini katia kuielewesha jamii juu ya athari za janga hilo ambalo hivi sasa limeshika kasi katika jamii.

 

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi pia, alieleza haja ya kutafutiwa ufumbuzi changamoto za Hijja huku akieleza umuhimu wa kuwepo Mfuko wa Hijja ambao umeweza kuzinufaisha nchi nyingi duniani ambazo zimeuanzisha.

 

Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuwekwa kwa utaratibu maalum kwa ajili ya walimu wa madrasa ikiwa ni pamoja na kuwepo miongozo ya utoaji elimu wa madrasa kwa mashirikiano ya viongozi wa dini, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Ofisi ya Mufti pamoja na Wadau ambao ni walimu hao wa Madrasa.

 

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza azma ya Serikali ya kuwaangalia kimaslahi walimu pamoja na madaktari kutokana na kazi kubwa wanazozifanya katika kutoa huduma katika jamii.

 

Nao Wajumbe wa Jumuiya hiyo ya (JUMAZA) walimpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar na kuweza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

 

Katika maelezo yao walimpongeza kwa kasi yake aliyoanza nayo katika kuwaletea maendeleo wananchi ikiwa ni pamoja na kuona umuhimu wa kuwepo amani, umoja na mshikamano katika jamii na kuamua kusimamia maridhiano.

 

Walieleza kuwa hatua zake za kurudisha mshikamano nchini na kuleta umoja ni jambo kubwa na la kuungwa mkono na kupongezwa  kwani bila ya kuwepo amani, umoja na mshikamano maendeleo hayawezi kupatikana.

 

Aidha, viongozi hao wa (JUMAZA), walieleza haja ya kutafatwa hatua za makusudi za kupambana na udhalilishaji katika jamii kwani janga hilo limekuwa likipoteza haiba ya nchi.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.