Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Azungumza na Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (ZNCC)

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa  akizungumza na ujumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabiashara (ZNCC)ukiongozwa na Kaimu Mwenyekiti Nd.Ali S.Amour katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabishara (ZNCC) wakimsikiliza  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakati wa mazungumzo yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.[Picha na Ikulu] 14/12/2020. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyiamesisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itashirikiana vyema na sekta binafsi ili kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaimarika zaidi.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na Ujumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), kufuatia muendelezo wa mkutano mkuu wa Wafanyabiashara wa Zanzibar, uliofanyika huko ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar mnamo Disemba 5, 2020.

Katika maelezo yake Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa azma yake ni kuimarisha  mashirikiano na sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira mazuri wafanyabiashara.

Aliwataka kutoa ushauri juu ya Mamlaka za Udhibiti zipo nyingi ambazo zimekuwa zikileta mkanganyiko katika ulipaji wa kodi na kusisitiza haja ya Mamlaka hizo kuwa  pamoja na kuwa katika eneo moja ili kuondosha usumbufu.

Alisisitiza azma yake kwa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA)katika kuhakikisha inajumuisha masuala yote muhimu kwa wawekezaji  ambapo wahusika wote ni lazima wawepo pamoja ili kurahisisha shughuli zao ikiwa ni pamoja na utoaji wa vibali kwa wawekezaji.

Hivyo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza haja ya sekta binafsi kutoa ushirikiano wake kwa kutoa ushauri ili kuhakikisha Mamlaka hiyo ya (ZIPA), inafanya kazi vyema katika kuwasaidia wawekezaji.

Alieleza haja ya kuwepo kwa mawasiliano kati ya sekta binafsi na Serikali kwa kujadiliana pamoja katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo na kueleza haja kwa Bodi hiyo kutafuta uwezo wa kuondoa matatizo katika sekta ya biashara kwa kupanga mambo vizuri.

Alieleza umuhimu kwa kufanyakazi kati ya sekta binafsi na sekta ya umma na kuwekwa watu wenye utaalamu katika kazi wanazozifanya.

Kwa upande wa uimarishaji wa viwanda vya ndani, Rais Dk. Hussein alieleza haja ya kuvilinda viwanda vya ndani ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ili kupatikana uwezo wa kuviendeleza na hatimae kuweza kuwasaidia wananchi wa Zanzibar hasa katika sekta ya ajira.

Aidha, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisisitiza haja katika kuwasaidia Wakandarasi wa Kizalendo ili kampuni zao ziweze kufanya kazi vyema hapa Zanzibar badala ya kuyatumia Makampuni kutoka nje hata kwa kazi ndogo hasa ikizingatiwa kwamba Wakandarasi Wakizalendo walio wengi Kampuni zao hazina uwezo mkubwa.

Alieleza umuhimu wa Vyuo Vikuu vyote kuweka mitaala inayohusiana na suala zima la ‘Uchumi wa Buluu’, ili kuwepo kwa matayarisho ya kuelekea katika uchumi huo kama vile Sera zinavyoelezea kwani watendaji wakuu wa uchumi huo wanatarajiwa kutoka huko.

Halikadhalika Rais Hussein Mwinyi alisema kuwa elimu ya kutosha inahitajika katika kuuelezea na kuufahamu ‘Uchumi wa Buluu’, hivyo muongozo unahitajika hasa kwa upande wa wanawake ili nao wajijue kuwa ni sehemu ya uchumi huo.

Alieleza azma yake ya kuanzisha utaratibu maalum wa kupokea changamoto kutoka kwa wananchi na hatimae changamoto hizo kupatiwa ufumbuzi kwa utaratibu maalum utaowekwa.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliahidi kufanya mikutano na sekta zote za biashara na kuwataka wajiandae ili watakapokutana waweze kutoa changamoto zao ambapo Serikali kwa upande ake itaangalia namna ya kuzitafutia ufumbuzi hatua ambayo alisema ni nzuri kuliko kufanya kazi kwa makongamano na semina ambazo hazina tija.

Aliwasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi huku akisema kuwa kodi maalum zimewekwa Zanzibar ili kuwasaidia Wazanzibari kupata unafuu katika bidhaa zao licha ya kuwa bado wananchi wa kawaida hawanufaiki.

Kwa upande wa pili alisema kuwa kwa upande mwengine kodi kwa Zanzibar imeshushwa hivyo ni vyema viongozi hao wakawataka wafanyabiashara kulipa kodi kwani kodi hiyo ndio inayosaidia kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo elimu, afya na nyenginezo huku akiwataka wafanyabiashara kuwahurumia wananchi wa Zanzibar.

Aliwataka wafanyabiashara wazungumze juu ya kuwasaidia wanyonge sambamba na kufikia malengo katika kujenga nchi.

Alisema kuwa ipo haja ya kuangaliwa tena katika suala zima la mikataba kwani kuna baadhi ya mikataba serikali haipati mapato yanayostahiki.

Aliipongeza azma ya sekta binafsi kuwasaidia vijana walioko vyuoni kufanya mazoezi ya masomo katika sekta binafsi zikiwemo hoteli na kampuni nyengine za ujenzi.

Sambamba na hayo, Rais Hussein Mwinyi aliahidi kukutana na wafanyabiashara wa kila sekta, Alieleza kuwa changamoto zao ni nini na ufumbuzi unatokana na nini na hiyo ni mwanzo wa majadiliano kati ya Serikali na wafanyabiashara huku akisisitiza haja kwa wafanyabiashara kushauri juu ya ukusanyaji na ulipaji wa kodi.

Mapema wajumbe hao walieleza azma yao ya kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya biashara hapa Zanzibar na kupongeza hotuba ya Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyoitoa katika mkutano wa wafanyabiashara uliofanyika Disemba 5, mwaka huu 2020 huko katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kiwkajuni Jijini Zanzibar.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) Ali Amour alieleza jinsi wafanyabiashara walivyofarajika na utayari wa Serikali anayoiongoza Rais Dk. Hussein mwinyi katika kushirikiana pamoja kuuinua uchumi wa Zanzibar.

Alisema kuwa Rais Dk. Hussein Mwinyi ameonesha azma ya mashirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma huku akieleza kwamba wataitumia hotuba hiyo katika vikao vyao kama dira ya kuwapeleka kwenye lengo lililokusudiwa.

Alieleza jinsi hapo siku za nyuma walivyokuwa wakifanya mikutano mingi ambayo haikuwa na tija hata kidogo huku akiahidi kuwa Jumuiya hiyo itafuata nyayo za Rais Dk. Hussein Mwinyi katika suala zima la ufuatiliaji na utekelezaji katika sekta ya biashara hapa nchini.

Nao wajumbe wa Bodi hiyo walieleza haja ya wafanyabiashara kulipa kodi na kuahidi kufanya makongamano ili kuhamasisha ulipaji wa kodi huku wakieleza haja kwa sekta binafsi kushirikishwa katika upangaji wa kodi.

Sambamba na hayo viongozi hao wa (ZNCC) walieleza matumaini yao kwa Rais Dk. Hussein Mwinyi na kuahidi kuendelea kumuunga mkono kwa lengo la kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaimarika na wananchi wake nao wanaimarika zaidi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.