Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amezungumza na Wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wafanyabiasha wa Zanzibar  katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar , kusikiliza Changamoto zinazowakabili katika Biashara.

WAFANYABIASHARA na wadau mbali mbali kutoka  sekta binafsi nchini wameiomba Serikali kuongeza ushirikiano na  sekta hizo kwa msingi kuwa zina mchango mkubwa katika uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar.

Hayo yameelezwa na wafanyabiashara kutoka sekta mbali mbali nchini katika salamu zao walipozungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi,  katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni Jijini hapa.

Viongozi walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na sekta ya Kilimo na Ufugaji,  Viwanda, TEHAMA, Usafirishaji, ZATO, ZATI Ujenzi, sekta ya Fedha, Usafiri, sekta ya Wanawake, Mafuta pamoja na Mafuta ya Ndege

Wamesema kuna umuhimu wa Serikali kuongeza mashirikiano na kufanya juhudi ili kuhakikisha taasisi hizo zinaondokana na changamoto mbali mbali zinazokabili,huku zikibainisha kuwa kuimarika kwake kutachochea ukuaji wa uchumi.

Mkurugenzi Mtendaji  kutoka MD-QBC Khamis Ali Said alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta hiyo ni hali iliopo hivi sasa ambapo  hakuna utaratibu wa kurudishiana kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Alisema   kuna umuhimu  kwa serikali zote mbili kukaa pamoja na kulipatia ufumbuzi wa kudumu  suala hilo kwa msingi kuwa lina athari kubwa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar.

Alisema upatikanaji wa rasilimali ya mchanga kwa ajili ya ujenzi, hususan katika  miradi mikubwa nao hauko sawa kiasi ambacho huwalazimu wakanadarasi kusitisha shughuli za ujenzi baadhi ya nyakati kutokana na ukosefu wa rasilimali hiyo.

Alisema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha mchanga unaopatikana nchini unafaa kwa matumizi sahihi ya miradi inayoendelezwa.

Aliiomba Serikali kufuatilia na kuhakikisha sheria ya manunuzi iliopo inatekelezwa na watendaji wake pamoja na kufuata kikamilifu vifungu vilivyoainishwa, sambamba na kuwataka watendaji hao kuacha utamaduni wa kutoa visingizio kuwa baadhi ya vifungu havijawekewa kanuni.

Aidha, aliiomba Serikali kuondoa mazingira yanayowanyima fursa  wakandarasi wazalendo  kutekeleza miradi mikubwa inayotangazwa , pamoja na kutaka kufanyike marekebisho ya viwango vya chini  vya miradi vya shilingi Bilioni mbili.

Nae, Meneja wa Benki ya Afrika Juma Burhan, alisema sekta ya Fedha inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ya kutokuwepo sera na sheria za usajili wa mali zinazohamishika.

Alieleza kuwa mbali na Benki ya Tanzania (BOT) kutoa katazo la kutokuwepo sehemu ‘bubu’ za kubadilishia fedha za kigeni nchini , lakini maeneo hayo yameendelea kuwepo na hivyo kuhusika katika biashara haramu.

Alisema kuna umuhimu kwa serikali kujenga ushirikiano na Benki binafsi ili ziweze kutoa mikopo na kuchochea uimarishaji w auchumi, wakati huu ambapo serikali haijazipa kipaumbele  benki za ndani.

Nae, Mkurugenzi wa ‘Rahisi Solutions’ Abdulrahman Hassan, alisema kuna  changamoto mbali mbali zinazoikabili Zanzibar katika sekta ya TEHAMA  ambazo zinaweza kutatuliwa na Wanzanibari wenyewe kwa kuwepo mashirikiano na serikali.

Alisema kinachohitajika ni kuwajengea uwezo vijana kwa kuamini kuwa Wazanzibari wanaweza kwa vile  wana ujuzi na uzoefu.

Aidha, Mwenyekiti wa UWAMWIMA Salum Rehani alisema Zanzibar imefanikiwa kuzalisha asilimia 50 ya mahitaji ya bidhaa za mboga mboga na matunda na kuuza katika soko la Utalii.

Alisema pamoja na mafanikio hayo ya uzalishaji wa bidhaa zilizo bora na salama, bado wakulima wanakabiliwa na changamoto kubwa ya soko la la kuuzia bidhaa hizo, kwani hivi sasa hupata fursa hiyo kwa asilimia 12 pekee, kwa vile wamiliki wa hoteli huagiza bidhaa za aina hiyo kutoka Tanzania Bara.

Alisema bado taasisi za fedha hazijafanya vyema katika kuwawezesha  na kuwawekea mazingira mazuri wakulima hao ili kupata mikopo na kuongeza uzalishaji.

Vile vile, alisema soko la maziwa yanayozalishwa Zanzibar bado limekuwa la mashaka, na kubainisha kuwa wafugaji huuza maziwa yao katika Kiwanda cha Bakharesa kiliopo Mtoni, wakati ambapo zaidi ya lita 8,000 ya bidhaa hiyo hukosa soko.

Rehani alisema sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu ni eneo muhimu na  mhili  wa uchumi wa Zanzibar kuliko eneo jengine lolote lile, akibainisha uwepo wa fursa za kutosha za ajira, na hivyo akaiomba Serikali kuwekeza nguvu zake katika kufanya tafiti na kuweka  mikakati ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwapatia vijara vijana.

Akigusia sekta ya usafiri wa anga, Mwenyekiti wa ZAT Mohamed Raza aliiomba serikali kuongeza juhudi kukamilisha matengenezo ya ‘terminal 3’ ili kuondokana na changamoto mbali mbali za usafiri kwa wageni.

Alisisitiza umuhimu wa wafanyabiAshara kulipa kodi kwa kigezo kuwa ndio inayoongoza nchi na kusadia upatikanaji wa huudma mbali mbali za kijamii, ikiwemo Afya.

Nae, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watembeza Watalii Zanzibar (ZATO) Hassan Ali Mzee aliomba kuwepo ushirikiano wa pekee kati ya Jumuiya hiyo  na Serikali  akibainisha utayari wa ZATO  katika kukabiliana na changamoto  mbali mbali inayokabili sekta hiyo.

Alisema ZATO ina jukumu kubwa katika uimarishaji wa sekta ya Utalii nchini kwa kuingiza watalii wengi zaidi, ikizingatiwa utajiri mkubwa wa vivutio vya utalii viliopo nchini.

Aidha, Mwenyekiti wa ZATI Seif Mirskry alisema ugonjwa wa Covid-19 ulioikumba Dunia umeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii, hivyo akaishauri Serikali kuwa sio wakati muafaka wa kufikiria kuongeza viwango vya kodi na kusema huu ni wakati wa wafanyabiashara kupata tahfif.

Katika hatua nyengine, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Fatma Khamis, alitaka kuwepo ushirikishwaji na uwezeshaji kwa wafanyabiashara hao ili kuboresha biashara zao na hatimae  kuinuwa uchumi wao .

Alisema wajasiriamali wanawake  wana changamoto mbali mbali ikiwemo ya upungufu wa elimu za biashara.

Aidha, Mkurugenzi wa ‘Purma Enery’ inatoa huduma ya  Mafuta ya Ndege, Rehema Migambile alimhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa Kampuni hiyo itaendelea kuwa kinara katika upatikanaji wa nishati hiyo ikilenga  kuhakikisha safari za ndege zinafanyika bila vikwazo.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.