Habari za Punde

ZAECA Yapewa Siku Saba Uchunguzi wa Pampu Saba za Kusukumia Maji Zilizonunuliwa na ZAWA.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akitoa wiki moja kwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar kufanya uchunguzi wa mashine Saba za kusukumia Maji zilizonunuliwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA}

Alitoa agizo hilo baada ya kufanya ziara ya ghafla Makao Makuu ya Mamlaka hiyo yaliyopo Kinazini jirani na Msiki Mabuluu.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na.Othman Khamis OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ametoa Wiki moja kwa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar {ZAECA} kukamilisha uchunguzi juu ya Pampu Saba za kusukumia Maji zilizonunuliwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} hivi karibuni.

Akifanya ziara ya ghafla Makao Makuu ya Mamlaka ya Maji iliyopo Kinazini jirani na  Msikiti Mabuluu Mjini Zanzibar Mheshimiwa Hemed alisema amefikia uamuzi wa kutoa agizo hilo ili Serikali Kuu ipate kujiridhisha kama hakuna dalili yoyote ya harufu ya rushwa kwenye manunuzi hayo.

Mh. Hemed alisema Serikali kamwe haitovumilia kuona  Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} ambayo ni Taasisi muhimu inayogusa moja kwa moja maisha ya viumbe inazunguukwa na uzembe unaoweza kuleta athari pamoja na kupungua kwa Mapato ya Serikali.

Alionya kwamba kuanzia sasa Mtumishi ye yote wa Taasisi za Umma anayeharibu na kushindwa kuwajibika katika eneo lake la Kazi huo utakuwa ndio mwisho wa Utumishi wake na Serikali haitathubutu kumuhamisha sehemu nyengine ambayo anaweza kufanya uzembe wa mara nyengine.

Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi wa Mamlaka ya Maji kujisafisha kwa kuondoa hitilafu za migogoro ya Uongozi ndani ya kipindi cha Mwezi Mmoja vyenginevyo Serikali italazimika  kusafisha safu hiyo ya Uongozi kwa maslahi ya Umma.

Mheshimiwa Hemed alisema Wahandisi wa Taasisi hiyo wanapaswa kurekebisha miundombinu sambamba na kuweka utaratibu utakaoharakisha Watendaji wa Mamlaka hiyo kuwajibika ipasavyo ili kuwapa fursa Wananchi kupata huduma za maji safi na salama muda wote.

Alisema wazi kwamba hali ya uwajibikaji kwa Watendaji wa Mamlaka ya Maji haiko vizuri kutokana na tabia ya muhali inayochukuwa nafasi kubwa na matokeo yake hata makusanyo ya Mapato yatokanayo na Huduma za Maji hayafikii lengo halisi lililokusudiwa.

Aliwataka Wafanyakazi hao kuendelea kufuatilia muenendo wa upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama katika maeneo yote ya Unguja na Pemba Mijini na Vijijini ili kuondoa au kupunguza kabisa malalamiko ya Wananchi yanayosikika kila wakati kwenye vyombo vya Habari.

Alisema suala hilo ni vyema likaenda sambamba kwa Watendaji hao kuhakikisha kwamba Wananchi na Taasisi zote zinazotumia huduma hiyo zinawajibika kulipa huduma hiyo ili Taasisi hiyo iweze kujiendesha badala ya kuendelea kupeleka maombi ya kupatiwa fedha Serikali Kuu.

Mheshimiwa Hemed alishauri kwamba Mteja atakayeendelea kusumbua katika ulipaji wa Huduma hiyo wataposhindwa kuwasiliana naye kwa njia ya kawaida ni vyema wakatoa taarifa Serikali kuu kwa kuchukuliwa hatua nyengine zinazofaa.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Nd. Mussa Ramadhan Haji alisema hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba  kwa sasa imefikia asilimia 80% hadi 85% kutegemea matumizi yaliyopo.

Nd. Mussa alisema wakati mwengine hali hiyo hushuka hadi asilimia 75% kutokana na baadhi ya Visima kukumbwa na hitilafu za Umeme lakini pia baadhi ya mashine za kusukumia Maji huharibika  kutokana na kutumika kwa muda mrefu hasa katika baadhi ya maeneo yasiyo na Matangi ya kuhifadhia Maji.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mamlaka ya Maji Zanzibar alibainisha kwamba katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na huduma za usambazaji Maji Wataalamu wake wameanza kufanya Utafiti wakianzia eneo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja ili kubaini kasoro zinazochangia uwepo wa changamoto hizo.

Alisema kwa hatua ya awali wamebaini uwepo wa baadhi ya Watu kuamua kuunga Maji kinyume na utaratibu, uchimbwaji wa mahodhi makubwa ya kuhifadhia Maji wakati wengine wanaendelea kutumia huduma hiyo bila ya malipo.

Nao kwa upande wao Wakurugenzi wa vitengo mbali mbali vya Mamlaka hiyo walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba muitiko wa Wananchi kuendelea kulipa huduma za Maji ni mdogo wakitoa sababu za kutokupata huduma hiyo kwa uhakika.

Walisema hivi sasa wapo katika utaratibu wa kujiandaa kufunga Mita kwa watumiaji wote wa Huduma hiyo mpango ambao utatoa uhalisia wa upatikanaji wa maji kwa wateja licha ya kwamba wapo baadhi yao hulalamikia ukosefu wa huduma hiyo wakati majumbani mwao yamejaa.

Walieleza kuwa ongezeko la upatikanaji wa huduma ya Maji litaimarika Zaidi mara baada ya kukamilika kwa Mradi wa huduma za Maji ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi uliopata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika sambamba na uingizaji wa Pampu za kusukumia Maji kwa visima Saba ndani ya Mkoa huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.