Habari za Punde

Dkt.Ndungulile Afungua Mafunzo ya Uongozi Kuijengea Uwezo Menejimenti na Watumishi wa Wizara Yake.

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na Menejimenti na watendaji wa Wizara hiyo (hawapo pichani) katika mafunzo ya uongozi kwa Menejimenti ya Wizara hiyo, yaliofanyika jijini Dodoma, wa kwanza kulia ni Naibu wake, Mhandisi Kundo Mathew akifuatiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndenjembi, kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndenjembi akizungumza katika mafunzo ya uongozi kwa Menejimenti na watendaji wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yanayofanyika jijini Dodoma, wa pili kulia ni Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile na Kushoto ni Naibu wake Mhandisi Kundo Mathew na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Zainab Chaula.

S ehemu ya Menejimenti na Watendaji wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakimsikiliza Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi yanayotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, jijini Dodoma

Na Faraja Mpina - WMTH

Waziri  wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe.Dkt. Faustine Ndugulile ameiagiza Menejimenti na watendaji wa Wizara hiyo kuhakikisha wanafanya maamuzi na kutoa ushauri wenye tija kulingana na nafasi zao ili kufikia malengo ya Wizara hiyo na kuharakisha michakato ya Serikali.

Dkt. Ndugulile amezungumza hayo akifungua mafunzo ya uongozi kwa wajumbe wa Menejimenti na watumishi wa Wizara hiyo, yanayotolewa na Chuo cha Utumishi wa umma Tanzania kwa muda wa wiki mbili.

Amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwa sababu Wizara hiyo ni mpya, yenye muundo mpya, majukumu mapya inataka kwenda na viwango vipya kwa kufanyakazi zenye ubora.

Ameongeza kuwa kuna baadhi ya watumishi wanajisahau kuwa wanawatumikia wananchi wa Tanzania na kudhani dhamana walizopewa ni kwa manufaa yao binafsi, na kusisitiza watendaji wa Wizara hiyo wafanye kazi kwa kufuata miiko na maadili ya watumishi wa umma.

“Ninatarajia kuona mabadiliko na maboresho katika utendaji kazi na utoaji wa huduma zetu kwa wananchi”, Dkt. Ndugulile

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa mafunzo hayo yanatoa mwanga wa kwenda kutekeleza vema ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuikumbusha Menejimenti ya Wizara hiyo kurudi katika misingi ya utumishi wa umma.

“Tukumbuke kwamba tumeaminiwa katika dhamana tulizopewa, tufanye kazi kulingana na matakwa ya nafasi zetu, kwa kila mtu kutimiza wajibu na kutambua mipaka yake kama sehemu ya maadili katika utumishi wa umma”, Mhandisi Kundo Mathew

Kwa upande wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndembeji aliyehudhuria ufunguzi wa mafunzo hayo amesema kuwa Chuo cha Utumishi wa umma ni wakala wa Serikali katika kunoa, kuandaa, kushauri na kuboresha utendaji kazi katika utumishi wa umma.

Ndembeji ameupongeza uongozi wa Wizara kwa kukitumia Chuo hicho kupiga msasa watendaji wa Wizara hiyo, ikiwa ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine za Serikali.

 ImetolewanaKitengo cha MawasilianoSerikalini

WizarayaMawasilianonaTeknolojiaya Habari

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.