Habari za Punde

Imarisheni vitengo vya Habari kurahisisha mfumo wa kupokea Malalamiko : Dk Mwinyi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Sera,Uratibu na Baraza la Wawakilishi, wakati wa kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatowa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wakati wa kuwaapisha, mkutano huo umefanyika katiuka ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezitaka Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha inaviimarisha vitengo vyao vya Habari ili kurahisisha mfumo wa kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi “Sema na Rais Mwinyi” unatekelezeka.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo, ikiwa ni mkutano kwa  ajili ya kuripoti utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Rais kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wakati alipowaapisha.

Katika maelezo yake hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba kuna haja ya kuhakikisha vitengo hivyo vya habari katika Mawizara ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vinaimarishwa ili kuhakikisha malengo yaliokusudiwa ya mfumo huo yanafikiwa.

Katika mkutano huo ambapo Makamu wa Pili alihudhuria, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa ni vyema pale wananchi watakapoanza kutoa malalamiko yao wakawa wanapata majibu kwa uhakika kutoka Taasisi husika.

Alisisitiza haja ya kuwepo kwa mtu maalum  atakaehusika na kazi hiyo katika vitengo hivyo Mawizarani  ambaye atakuwa anaripoti na kupeleka sehemu husika malalamiko hayo na hatimae kuweza kupatikana majibu kwa haraka.

Rais Dk. Mwinyi alieleza umuhimu wa utekelezaji wa mfumo huo ambao utawasaidia wananchi na kusisitiza kwamba hatua zote zinazoendelea yeye atakuwa akiziona.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alipongeza juhudi zilizochukuliwa na uongozi wa Wizara hiyo katika kutekeleza maagizo aliyoyatoa na kusisitiza haja ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo.

Rais Dk. Mwinyi pia, alieleza umuhimu wa Mifuko ya Uwezeshaji kuwa pamoja hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwarahisishia walengwa kunufaika kirahisi.

Pia, Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi huo kwamba vikao hivyo vitakuwa endelevu kwa lengo la kuweza kupata mafanikio na changamoto ambapo hatimae kutafuta ufumbuzi wa utatuzi wa changamoto hizo kwa azma ya kupata ufanisi mzur zaidi.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais , Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Mohamed Salum alianza kwa kutoa pole kwa Rais kufuatia kifo cha Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea hivi karibuni.

Waziri Khalid Mohamed Salum alimueleza Rais Dk. Mwinyi historia ya kuanzishwa kwa Ofisi hiyo huku akieleza kwamba Ofisi hiyo ni kiungo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dk. Khalid alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Mwinyi hatua zilizochukuliwa na Ofisi  hiyo katika utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu mara baada ya kuapishwa Novemba 21, 2020 na Januari 25,2021.

Aidha,  alieleza kwamba Ofisi hiyo ndiyo mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Serikali, hivyo kama zilivyo Wizara na Taasisi nyengine inahitaji mazingira mazuri ya kazi na nyenzo za uhakika ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Sambamba na hayo,  alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa namna alivyoanza na kuendelea kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kumpongeza Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa miongozo yake na ushauri anaowapa.

Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said alieleza haja ya kuwepo elimu zaidi kwa wananchi katika kuhakikisha malengo ya mfumo wa “Sema na Rais Mwinyi” yanafikiwa kwani mfumo huo umepokewa vizuri.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi Thabit Idarous Faina alieleza jinsi Wizara hiyo ilivyotekeleza maagizo ya Rais aliyoyatoa wakati alipowaapisha Mawaziri na Makatibu Wakuu ambapo miongoni mwa utekelezaji huo ni pamoja na Waziri kutembelea Taasisi zilizokuwemo katika Ofisi hiyo, kulipa madeni ya Serikali pamoja na mambo mengineyo.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alieleza kwamba katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025, jumla ya miradi 12 imeibuliwa na kuwasilishwa Tume ya Mipango ambayo inaitarajiwa kutekelezwa ndani ya miaka mitano kuanzia 2021/22 hadi 2025/26 baada ya kuidhinishwa katika ngazi husika.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.