Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ametoa Salamu za Rambirambi Kwa Mama Janeth Magufuli,Familia na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za rambirambi kwa Mama Janeth Magufuli, familia pamoja na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na wananchi wote wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 17.2021 Jijini Dar-es-Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Salamu hizo za Rais Dk. Mwinyi zilieleza kuwa huu ni msiba mzito sana kwake na kwa taifa la Tanzania, hivyo aliwaomba wananchi kuwa na subira na utulivu katika kipindi hichi kigumu cha msiba huu mzito wa kitaifa.

Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wananchi wote wa Zanzibar Rais Dk. Mwinyi alitoa salamu hizo za rambirambi na kumuomba  Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi, Amin.

“Kwa masikitiko makubwa kabisa nimepokea taarifa ya kifo cha Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyefariki jana Jumaatano tarehe 17 Machi, 2021 majira ya saa 12 jioni kwa maradhi ya moyo katika hospitali ya Mzena Jijini Dar-es-Salaam alipokuwa akipata matibabu”, zilieleza salamu hizo  za rambirambi Rais Dk. Mwinyi.

Katika taarifa yake, Mama Samia Suluhu Hassan alisema kuwa Rais Magufuli aliaga dunia katika hospitali ya Mzena iliyopo Jijini Dar es Salaam mnamo majira ya saa kumi na mbili jioni kwa saa za Afrika Mashariki kutokana na matatizo ya moyo.

Akithibitisha kifo hicho Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alisema kwamba Rais Magufuli alianza kuugua mnamo tarehe 14 Machi na kulazwa katika Hospitali hiyo ambapo alifariki.

Rais Magufuli ambaye ni Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefariki  dunia akiwa na umri wa miaka 61 ambapo Tanzania hivi sasa inaomboleza kifo cha kiongozi huyo kwa muda wa siku 14 kama ilivyotangazwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.