Habari za Punde

Mungu ameweka kusudi jema kwa Rais Samia atatufikisha nchi ya asali na maziwa, tumuombee- Nabii Joshua

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

WATANZANIA wametakiwa kumuunga mkono, kumtia moyo na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Mungu ameweka kusudi jema kwake ili kuipeleka Tanzania katika nchi ya asali na maziwa.

Hayo yamesemwa na Rais wa New Covenant Unity International (NCUI) ambaye pia ni Kiongozi wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala katika ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Mlima wa Mungu uliopo Mkundi kwa Lung'wawa Morogoro Mjini kwa Nabii Joshua.

"Hii ni siku maalumu ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya maisha na uongozi wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na kumuombea Mama yetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan ili Mungu amuongoze katika kuliongoza Taifa letu kwa mafanikio makubwa. Ibada hii inafanyika hapa Mlima wa Mungu uliopo Mkundi kwa Lung'wawa Morogoro Mjini kwa Nabii Joshua.

"Huu ni mwendelezo wa maono makubwa ambayo Mungu amenipa kupitia huduma ya Sauti ya Uponyaji ambayo ina makao yake Yespa, Kihonda mjini Morogoro. Tutaendelea kuliombea Taifa letu na viongozi wake kupitia Kampeni ya Ombea Taifa (Pray for Nation),"amesema Nabii Dkt.Joshua.

Amesema, kuwa licha ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli ambaye alikuwa Rais wa vita na mapambano kwa ajili ya kupambania maslahi ya Tanzania ikiwemo kuwavusha Watanzania katika Bahari ya Shamu, hakuna kukata tamaa kwa sababu, Mungu amempa maono ya kuyaendeleza aliyoyaacha Dkt.Mgufuli.

"Huu ni muda wa kufanya kazi kwa bidii na kufanya maombi maana Mungu ameweka jambo jema kwa Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo hakuna kurudi nyuma, yatupasa kufanya kazi kwa bidii, kulipa kodi na kuiombea Serikali. Kwa hatua hizo, neema tele tutazishuhudia kwa Taifa letu,"amesema Dkt.Nabii Joshua.
 
Aidha, Dkt.Nabii Joshua alisema kuwa, Watanzania wana matumaini makubwa kwa Rais Samia na watazidi kumuombea.

"Mungu amjalie afya tele, nguvu na ujasiri na aweze kuwa mjumbe wa kuleta habari njema za matumaini mapya kwa Taifa letu la Tanzania.Hakika Mungu ameweka kitu cha kipekee ndani ya Rais wetu,"amesema Nabii Dkt.Joshua na kuwataka kuwa jasiri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.