RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi leo
amejumuika na wananchi, viongozi wa Serikali pamoja na viongozi wa madhehebu
mbali mbali ya Dini katika dua ya kumbukumbu ya muasisi wa Zanzibar, marehemu
mzee Abeid Amani Karume.
Katika hafla hiyo iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alihudhuria, ambapo viongozi na wananchi hao walishiriki katika kisomo maalum na hatimae viongozi wakuu wakapata fursa ya kuzuru kaburi la marehemu na kumuombea dua.
Katika Hitma hiyo iliyoongozwa na Sheikh Mohamed Abass, Mufti wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab aliomba dua na kusema wakati wa uhai wake marehemu alileta neema kubwa kupitia Nyanja tofauti ikiwemo ujenzi wa majengo ya kisasa katika maeneo mbali mbali nchini, akilenga kuboresha maisha ya wananchi.
Alisema Marehemu mzee Abeid Amani Karume alisisitiza umoja na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari pamoja na kuhakikisha kila mwananchi anaishi maisha mazuri katika Nyanja zote, ikiwemo upatikanaji wa chakula, malazi na makaazi.
Aidha, Sheikh Kaab alimuombea dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kumuomba Mwenyezi Mungu aithibitishe azma yake inayolenga kuwepo umoja na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari wote.
Mapema, Mjumbe wa Baraza la Maulamaa Zanzibar Sheikh Salum Batashi alimsifia Marehemu Karume kuwa ni kiongozi alieifanyia mambo mengi mazuri Zanzibar, jambo linaloendelezwa na viongozi wanaomfuatia.
Aliwataka waumini na wananchi kwa ujumla kumkumbuka na kumuombea dua marehemu Karume, kuyaenzi yale aliyoyaanzisha pamoja na kuwatakia rehema viongozi waliotangulia mbele ya haki , sambamba na kuwapa pole viongozi waliopo kwa misiba mbali mbali iliolikumba Taifa.
Katika hatua nyengine, Viongozi wa serikali, viongozi wa dini kutoka madhehebu mbali mbali nchini pamoja Mwakilishi wa Vyombo vya ulinzi na Usalama walipata fursa ya kuweka mashada ya maua juu ya kaburi la Marehemu pamoja na kumuombea dua..
Dua ya kumbukumbu ya Marehemu Abeid Amani Karume, ambayo hufanyika kila ifikapo April 7 ya kila mwaka, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali, akiwemo Rais wa Jamuhuri ha Muuungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassimu Majaliwa pamoja na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.
Wengine, ni Rais mstaafu wa Zanzibar Abeid Amani Karume, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla,Mawaziri wa SMZ na SMT pamoja na Mabalozi wadogo wanaoziwakilisha nchi zao waliopo Zanzibar.
Aidha, wengine ni Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji, Mwakilishi wa Familia ya Marehemu Balozi Ali Karume, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Sadalla ‘Mabodi’.
Vile vile hafla hiyo Viongozi mbali mbali wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini walihudhuria.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal
Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment