Habari za Punde

Ushirikiano Mzuri Uliopo Kati ya Zanzibar na Oman Kuongeza Zaidi Katika Sekta ya Biashara.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa Tanzania Nchi Oman Mhe.Abdalla Abbas Kilima, alipofika Ikulu kwa mazungumzo na kujitambulisha, mazungumzo hayo yamefanyika katikia ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Zanzibar na Oman na kueleza haja ya kuongeza ushirikiano zaidi katika sekta ya biashara.

Rais Dk. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Oman Abdalla Abbas Kilima aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha na kusalimiana na Rais.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Zanzibar inahistoria nzuri kati yake na Oman na tayari kumekuwa na mahusiano na mashirikiano mazuri katika nyanja mbali mbali lakini ni vyema mashirikiano hayo pia, yakaimarishwa kwenye sekta ya biashara.

Alieleza kuwa Oman ni mdau mkubwa wa maendeleo kwa Zanzibar hivyo, ni vyema uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliopo ukaimarishwa zaidi.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Serikali ya Oman kwa kuonesha utayari wa kusaidia ukarabati wa majengo ya kale yakiwemo Beit al Ajaib pamoja na jumba la wananchi Forodhani ambapo mchakato wake unaendelea.

Alisema kuwa tayari kwa upande wa ujenzi wa Bandari, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini Hati ya Maelewano naMamlaka ya Uwekezaji ya Omaninayohusu mpango mkuu wa ujenzi wa bandari ya Mangwapwani/Bumbwini pamoja na kuigeuza Bandari ya Malindi kuwa ya Kitalii ambapo Serikali iko tayari katika ushirikiano huo na Serikali ya Oman.

Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa utayari wa Kampuni hiyo kwa kufanya upembuzi yakinifu kwa fedha zao wenyewe pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya ndege ya Oman kwa kuonesha nia ya kushirikiana na Zanzibar kwa azma ya kuja kuekeza katika viwanja vya ndege Unguja na Pemba.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa Serikali ya Oman kutoa fursa katika kupata soko la bidhaa za Zanzibar nchini humokwani soko  la ‘Gulf’ ambalolimekuwa na uzoefu na historia kubwa ya bidhaa za Zanzibar.

Alieleza haja ya kuwepo kwa soko la uhakika la bidhaa za Zanzibar nchini Oman zikiwemo bidhaa za matunda, mwani, viungo na karafuu hasa ikizingatiwa kwamba bei ya dunia ya karafuu imekua ikishuka hivi sasa.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua ya mashirikiano yaliopo kati ya Zanzibar na Oman na kueleza jinsi Mamlaka ya Uwekezaji wa Oman ilivyotiliana saini na Zanzibar katika Mpango Mkuu wa Ujenzi wa Bandari ya  Magapwani/Bumbwini.

Nae Balozi wa Tanzania nchini Oman alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi sambamba na kazi nzuri ambazo ameanza kuzifanya katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Balozi Kilima alieleza kwamba Serikali ya Oman imekuwa na uhusiano mwema na wa kihistoria na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar na kueleza hatua ambazo Oman inaendelea kushirikiana na Zanzibar ikiwemo ukarabati wa majengo hayo ya kihistoria.

Hivyo, ameahidi kulifanyia kazi suala zima la biashara kati ya Zanzibar na Oman hasa ikizingatiwa kwamba tayari kuna Baraza la Biashara ambalo liliundwa kwa ajili ya mashirikiano katika sekta hiyo kati ya Tanzani na Oman.

Aidha, alieleza azma ya Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Oman kukutana na kuimarisha mashirikiano na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.