Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Maswala ya Ulemavu Vijana, Sera na Uratibu wa Shughuli za Bunge Jenista Mhagama akitoa historia ya mwenge wa uhuru na kutolea ufafanuzi faida zinazopatikana katika mbio za Mwenge huko Ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya kale Kikwajuni Zanzibar.
Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Rashid Makame Shamsi, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kesho siku ya Jumatatu Mei 17 katika Uwanja wa Mwehe Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Hayo aliyasema katika Uwanja huo wakati wa harakati za ukamilishaji wa Maandalizi ya upokeaji wa Mwenge wa Uhuru ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmin katika wilaya hiyo.
Alisema katika ukimbizwaji wa Mwenge huo utazindua miradi mitatu ya maendeleo katika mkoa wa Kusini Unguja ikiwemo mradi wa maji safi na Salama ambao utazinduliwa katika shehia ya Mtende, uwekaji wa jiwe la msingi Ukumbi wa mitihani katika Skuli ya Jambiani, na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa kijamii pamoja na nyumba maalum inayohusiana na masuala ya maadili.
Hata hivyo alisema Uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru utaufanya Mkoa wa Kusini kutambulika kimataifa na kupatikana fursa za uwekezaji kwa wageni ambao watafika hapo na kuvutika na hali halisi ya mazingira jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wa nchi
Kwa upande wa Mkuu wa Itifaki Fakih Kombo Faki amesema taratibu zote zimeshaandaliwa ikiwemo utaratibu wa usafiri ambao utawachukua wananchi wote wanatarajiwa kufika katika uwanja huo.
"Tumeweka gari katika vituo vyote ambavyo wananchi watakuwepo, pia kwa watu wenye mahitaji maalum nao wamezingatiwa kwa sababu hii ni tunu ya watu wote"alisema.
Nae Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kasini Abdul Aziz Hamad Ibrahim, wanafurahia Mwenge huo kuzinduliwa katika Mkoa wa Kusini kwa sababu ndiko alikotoka Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Alisema wanatarajia wananchi wengi watahudhuria katika sherehe hizo wakiwemo wanachama wa vyama vyote vilivyopo nchini ,
Nao Wananchi wa Mkoa huo baadhi yao wamesema wamefarajika sana kupata tunu hiyo ambayo wamezowea kila mwaka kufanyika Dare es salam.
Walisema watahakikisha wanatoa ushirikiano kwa wageni na wenyeji wote ambao watafika wilaya ya Kusini.
Nae Kijana Asha Makame Ali alisema Mwenge huo umekuwa ukiwafungulia fursa mbali mbali ambapo mwaka 2001 walipata kufunguliwa soko kubwa la biashara maeneo ya Kitogani.
Mwenge wa Uhuru ni Chombo kilichoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961, ikiwa ni tunu na ishara ya kuwepo kwa Taifa huru la Tanganyika ,
Kauli Mbiu ya mwaka huu ni “TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu; itumie kwa usahihi na uwajibikaji ”
No comments:
Post a Comment