Habari za Punde

Maafisa Ustawi na Maendeleo Watakiwa Kubuni Mbinu Kuzuia Ukatili Kwa Watoto.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungmza na Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Songwe katika kikao kazi cha kujadili changamoto walizonazo, kilichofanyika Mkoani hapo.
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt. Seif Shekalaghe akimkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu kuzungumza na Maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Songwe katika kikao kazi kilichofanyika Mkoani hapo kwa lengo la kujadili changamoto za kada hiyo. 
Baadhi ya Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Songwe wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu katika kikao kazi kilichofanyika Mkoani hapo kwa lengo la kujadili changamoto za kada hiyo.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WAMJW)


Na Mwandishi Wetu, Songwe 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu amewataka Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii nchini kuhakikisha wanakuwa wabunifu ili Jamii itambue umuhimu wa majukumu yao.

 

Akizungumza na Maafisa wa Mkoa wa Songwe katika kikao kazi chenye lengo la kujadili changamoto wanazokutana nazo, Dkt. Jingu amesema Maafisa hao wana jukumu kubwa la kutatua  migogoro ya familia pamoja na kubadili fikra na mila potofu zinazochangia ukatili hususani kwa watoto

 

Jingu amesisitiza kuwa, Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wahakikishe wanatumia ujuzi, weledi na utaalamu wao hasa katika kulinda na kutetea maslahi ya watoto.

 

"Chanzo kikubwa cha ukatili dhidi ya watoto ni migogoro katika familia, lazima sisi kama wataalamu katika jamii, tuone namna gani tunaweza tukaboresha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya familia ili watoto wetu wakue vizuri na waweze kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote" alisema Jingu. 

 

Ameongeza pia Maafisa Maendeleo ya Jamii ni wataalamu wa kushughulikia na kubadilisha Jamii kwenye fikra, mila na desturi zinazoendeleza ukatili huku Maafisa Ustawi katika eneo hilo wana jukumu la kutatua migogoro na kuhakikisha haki inatendeka, ndiyo sababu wanatakiwa kuwepo wakati wa kusikiliza kesi za watoto.

 

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt. Seif Shekalaghe akimkaribisha Dkt. Jingu kuzungumza na Maafisa hao amemshukuru kwa uamuzi huo kwani utawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

 

Baadhi ya Maafisa wakimueleza Katibu Mkuu jinsi wanavyohakikisha wanapunguza tatizo la ukatili wamesema wanashirikiana na wadau mbalimbali kama vile viongozi wa Dini ambapo hivi sasa matukio ya ukatili yamepungua.

 

"Elimu zimeendelea kutolewa kuanzia ngazi ya chini hususani Viongozi wa Dini na Viongozi wa mila ili wakawaelimishe wananchi katika maeneo yao" alisema Mariam Daniel Afisa Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.

 

Aidha, Ritha Kamenya na Daud Mdaki wamesema kikao na Katibu Mkuu kimekuwa na manufaa kwao kwani kimewapa nguvu ya kuendelea kufanya kazi kwa juhudi zaidi.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.